Jeshi la Polisi lathibitisha mauaji ya MC Pilipili, lawasaka waliohusika

November 19, 2025 5:34 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Watakaobainika kuhusika na tukio hilo la mauaji sheria itachukua mkondo wake.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limethibitisha rasmi mauaji ya msanii na mshehereshaji maarufu Emmanuel Mathias, (MC Pilipili) likiahiidi kuwasaka waliohusika ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Taarifa za kifo cha MC Pilipili zilianza kusambaa jioni ya Novemba 16, 2025 bila kufahamika kwa chanzo halisi hatua iliyoibua simanzi na maswali mengi miongoni mwa wanafamilia na mashabiki wa msanii huyo.

Taarifa ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ACP William Mwamamfupa iliyotolewa leo Novemba 19, 2025  imebainisha kuwa kifo hicho kilitokea katika Kituo cha Afya Ilazo mkoanni Dodoma.

Majira ya saa nane mchana, msaidizi wake Hassan Ismail alipigiwa simu na mtu asiyefahamika na kuombwa akutane naye. Baada ya kufika, aliwakuta watu watatu asiyowafahamu wakiwa na MC Pilipili ndani ya gari dogo jeupe. Walimkabidhi MC Pilipili akiwa na hali mbaya kisha wakaondoka,” inaeleza taarifa ya ACP. 

ACP Mwamamfupa amebaianisha kuwa uchunguzi wa awali  uliofanywa na jeshi hilo kwa kushirikiana na wataalamu wa afya, umebaini kuwa MC Pilipili alifariki dunia baada ya kushambuliwa maeneo mbalimbali kwenye mwili wake.

Aidha, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea kufanya uchunguzi na kuwasaka wale wote watakao bainika kuhusika na tukio hilo ili utaratibu wa kisheria uendelee dhidi yao.

Mc Pilipili mchekeshaji na mshehereshaji alikatishwa uhai wake na watu wasiojulikana. Picha/ Mwananchi.

Mc Pilipili ni nani?

Mc Piipili alizaliwa Oktoba 1, 1985, katika Mtaa wa Airport mkoani Dodoma, akiwa mtoto wa pili wa Mathias na Mariam Matebe. 

Kutoka utotoni, alionyesha vipaji vya kipekee vya uchoraji, kuimba, muziki na ucheshi na elimu yake ya msingi aliipata katika Shule ya Uwanja wa Ndege hadi darasa la nne, kisha akaendelea na shule ya Ipagala  na kuhitimu darasa la saba mwaka 2000.

Baada ya kuingia sekondari, MC Pilipili alichagua kusomea Sanaa za Jukwaani, jambo lililoendeleza kipaji chake cha uchekeshaji na kuongoza matukio. 

Aliibuka kama mshereheshaji na mchekeshaji mashuhuri, akiongoza harusi, maadhimisho, na onyesho mbalimbali nchini na nje ya mipaka ya Tanzania.

Mbali na kazi yake ya ucheshi,aliwahi kushirikia katika siasa na jamii, ikiwa ni pamoja na kujaribu kushiriki katika uchaguzi wa udiwani Kata ya Tambukareli.

MC Pilipili enzi za uhai wake alifanikiwa kumuoa Philomena Thadey, maarufu kama Cute Mena na walikuwa na mtoto mmoja aitwaye Elphina. 

Ukiachilia mtoto wa kwenye ndoa yake pia alikuwa na watoto wengine wa kike ambao ni Mariam na Brianna. 

Licha ya taarifa ya Jeshi la Polisi, kwa sasa swali la nani amehusika na sababu za tukio hili bado linabaki wazi, huku familia, marafiki na mashabiki wakilia kifo cha mshereheshaji huyu ambaye anatarajiwa kuzikwa kesho Novemba 20,2025 jijini Dodoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks