Jack Ma aanza kukabidhi mikoba ya Alibaba kwa washirika wake
- Daniel Zhang apewa jukumu la kuongoza Bodi ya Wakurugenzi ya Alibaba.
- Mkakati uliopo ni kumpunguzia Ma majukumu ya kiutendaji na kuwaachia watu wengine kuongoza kampuni hiyo.
Dar es Salaam. Kampuni mama ya Alibaba imemteua Daniel Zhang kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ambaye amechukua nafasi ya Jack Ma ikiwa ni sehemu ya kumpunguzia madaraka ya kiutendaji na kuwapa nafasi watu wengine kuongoza kampuni hiyo.
Awali Zhang alikuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Alibaba amepanda chati ya uongozi katika kampuni hiyo kubwa duniani inayojihusisha na uuzaji wa bidhaa mtandaoni.
Jack Ma anayeshika nafasi ya 21 katika orodha ya mabilionea duniani, anachukua nafasi ya Zhang ya Mwenyekiti Mtendaji ambapo atashika nafasi hiyo kwa miezi 12 kabla ya kumpa nafasi hiyo mtu mwingine na yeye kubaki kama mjumbe wa bodi wa kampuni hiyo ifikapo 2020.
“Hii ni ishara kuwa Alibaba inavuka kwenda hatua nyingine ya kiutawala kutoka ngazi ya kampuni inayotegemea mtu binafsi, kwenda juu ya mifumo ya ubora wa shirika na utamaduni wa maendeleo ya talanta. ” amesema Ma kwenye barua yake kwa Alibaba.
Kitendo cha Ma kukabidhi kiti kwa Zhang kimempa matumaini makubwa kutokana na uamininifu alionao kwa watu wake. “naamini maamuzi haya yamefanyika kwa wakati muafaka kutokana na kampuni niliyonayo na uaminifu nilionao kwa watu wangu” amesema Ma.
Jukumu alilonalo Ma ni kuendelea kuwa kiongozi msaidizi katika kuimarisha uhusiano katika kampuni hiyo yenye viongozi waandamizi 36.
Kustaafu kwa Jack Ma ni pigo kubwa kwa Alibaba |Picha na TechCircle.
Pamoja na majukumu aliyonayo Ma amezidi kuonesha shauku ya kujifunza mambo mbalimbali kwasababu ndicho kitu anachopenda kufanya zaidi katika maisha yake.
Kulingana na ripoti mbalimbali, Ma ni mwalimu mstaafu na mmoja ya waanzilishi wa Alibaba mwaka 1999. Ripoti ya jarida la biashara la “Fobes” mwaka 2018 linamtaja kama mmoja wa mabilionea nchini China mwenye utajiri unaofikia Dola za Marekani 36.6 bilioni.
Wiki iliyopita gazeti la New York Times lilipoti kuwa bilionea huyo angestaafu jana (Septemba 10, 2018) ikiwa ni sehemu ya kumpunguzia majukumu ya kuiongoza kampuni hiyo kubwa ya biashara mtandaoni duniani.