Instagram yazidi kujivua gamba, kuja na mfumo mpya wa mawasiliano
- App hiyo itakua na jina la “Threads” kama ilivyo Messenger kwa Facebook.
- Lengo kuu la kuleta mabadiliko hayo katika mtandao huo ni pamoja na kuleta ujamaa kati ya marafiki.
Mtandao wa kijamii wa Instagram unatarajia kufanya mabadiliko katika mfumo wake wa mawasiliano ambapo watumiaji wake watakua na uwezo wa kuwasiliana kwa njia ya ujumbe mfupi nje ya mfumo uliozoeleka.
Mfumo huo wa mawasiliano, utakaokuwa katika programu tumishi (app), utaitwa “Threads”.
Katika huduma hiyo mpya, watumiaji wa Instagram hawatakuwa na uwezo wa kuwajulisha marafiki zako katika mtandao huo baadhi ya taarifa muhimu kuhusu mtumiaji, mahali walipo kwa wakati fulani, ujumbe mfupi kuhusu chaji iliyobaki kwenye simu, au hata picha na video.
Lengo kuu la kuleta mabadiliko hayo katika mtandao huo ni pamoja na kuleta ujamaa kati ya marafiki na ukaribu zaidi ya ule uliokuwepo awali katika njia iliyokua ikitumika katika kuwasiliana baina ya marafiki, mtandao wa masuala ya teknolojia wa Marekani wa The Verge umedokeza.
Lengo kuu la kuleta mabadiliko hayo katika mtandao huo ni pamoja na kuleta ujamaa kati ya marafiki. Picha|Mtandao.
Mfumo huo utakua na uwezo wa kumjulisha mtu pale rafiki yake anapokua kwenye intaneti kwa kuona alama ya kijani pembeni ya jina la rafiki yake kama vile ilivyo katika mfumo wa ujumbe wa moja kwa moja maarufu kama DM kwa sasa.
Bado haijajulikana ni lini mfumo huu utaanza kutumika japokuwa ni mpango uliopo katika mabadiliko yanayotarajiwa kufanyika hivi karibuni katika mtandao huo wa Instagram.
Zinazohusiana:
- Instagram yazindua akaunti maalumu ya kuuza bidhaa mtandaoni
- Facebook, Instagram ‘kufichua’ kiwango cha muda unaotumika mtandaoni
Mabadiliko haya yamekuja baada ya mtandao wa Instagram kuona ushindani mkubwa kutoka Snapchat. Inaelezwa kuwa kuna idadi kubwa ya watumiaji katika mtandao wa Snapchat na watu wengi hukaa katika mtandao huo kwa muda mrefu. Hata hivyo, Snapchat haina watumiaji wengi kama ilivyo kwa Instagram na Facebook.
Kuletwa kwa programu hiyo tumishi ya Instagram kama ilivyo kwa Facebook Messenger itasaidia kuongeza muda utakaotumiwa na watu katika mtandao wa Instagram kuliko ilivyo sasa.