Instagram yaja na mbinu mpya kudhibiti uzalilishaji mtandaoni

July 10, 2019 8:33 am · Daniel
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeanzisha kipengele kinachomuwezesha mtoa maoni kwenye mtandao huo kufikiria mara mbili kabla ya kutuma maoni yake kwa watu wengine.
  • Pia inakusudia kuanzisha kipengele kimya kuwaficha watumiaji wake dhidi ya wazalilishaji.

Katika kukabiliana na unyanyasaji na lugha za kuudhi miongoni mwa watumiaji mtandaoni,  Instagram wiki hii umeanzisha mfumo utakaosaidia kupunguza athari za lugha hizo ambazo zimekuwa zikisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii. 

Instagram imefanya marekebisho kwa kuweka kipengele kipya kitachokuwa kinatokea pale mtumiaji wa mtandao huo atakapotaka kutoa maoni yake dhidi ya jambo fulani au mtu fulani kwa kumpa nafasi ya pili ya kujiuliza kabla ya kutuma ujumbe wake. 

Taarifa iliyotolewa na Instagram juzi (Julai 8, 2019) na Mkuu wa mtandao huo, Adam Mosseri imesema kwa muda mrefu wamekuwa wakipambana na udhalilishaji wa kimtandao kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo akili bandia (Artificial Intelligence-AI) ili kugundua maoni, picha na video zisizofaa. 

Lakini wamepiga hatua zaidi, ambapo AI kupitia kipengele kipya cha maoni inafanya kazi ya kumjulisha mtumiaji kutafakari au kufuta maoni kabla ya kusambaza kwa watu wengine na kuhakikisha hapokei maoni ya uzalilishaji. 

Taarifa hiyo inaeleza kuwa wakati Instagram ikitumia teknolojia kukabiliana na udhalilishaji wa mtandaoni, kuna kila sababu ya kuwajengea uwezo watumiaji wa mitandao ya kijamii wakiwemo vijana kufahamu madhara ya vitendo hivyo. 


Zinazohusiana: 


Katika mipango yake ya baadaye, Instagram inakusudia pia kutengeneza kipengele kingine kumsaidia mtumiaji kudhibiti matumizi ya mtandao huo, pasipo kuingiliwa na mtu mwingine mwenye nia ovu. 

Mosseri amesema kipengele hicho cha kudhibiti akaunti  dhidi ya wazalilishaji hao wa kimtandao kinatapewa jina la  ‘Restrict’ ambapo mtumiaji wa mtandao huo atakuwa na uwezo wa kuzuia maoni ya kudhalilisha ya mtumiaji mwingine kuonekana au kutokaoneka kwa wafuasi wengine kwenye akaunti yake hivyo kupelekea maoni hayo kubaki kwa aliyetoa bila kusambaa.

Kipengele hicho pia kitamzuia mzalilishaji kumuona mtumiaji wakati akisoma jumbe kwenye mtandao huo. 

Hatua hizo zinazochukuliwa na Instagram, huenda ikawa ni njia ya kuimarisha uhusiano na watumiaji wake na kuwalinda dhidi ya hatari yoyote ya mtandaoni. 

Mitandao ya mingine kama Facebook na Twitter nayo inafanya jitihada mbalimbali kuzuia udhalilishaji wa mtandaoni ili kuhakikisha matumizi ya intaneti yanaleta manufaa katika jamii. 

Enable Notifications OK No thanks