ILO: Watu 7,500 hufariki kila siku duniani wakiwa kazini
Mamlaka za ajira zimeshauriwa kupitia upya mabadiliko ya utendaji wa kazi yanayoruhusu watu wengi kuajiriwa na wakati huo huo wanafanya kazi zinazowaletea shinikizo na hofu ya kupoteza kazi na kuingiliwa kwa faragha zao. Picha|Mtandao.
- Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) imebainisha kuwa vifo hivyo vinasababishwa na mazingira yasiyo salama na afya katika maeneo ya kazi duniani.
- Kila mwaka watu zaidi ya 374 milioni wanajeruhiwa au wanaugua kwa sababu ya ajali kazini ikiwemo kufanya kazi muda mrefu bila kupumzika.
- ILO yapendekeza tathmini ifanyike kwa sera, teknolojia na matumizi ya mifumo ya kidijitali, maroboti inayotumiwa na wafanyakazi.
Dar es Salaam. Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) imebaini kuwa kila siku watu 7,500 hufariki dunia ulimwenguni kutokana na mazingira yasiyo salama na afya katika maeneo ya kazi, jambo linalopunguza nguvu kazi inayohitajika katika maendeleo ya kiuchumi.
Pia kila mwaka watu zaidi ya 374 milioni duniani wanajeruhiwa au wanaugua kwa sababu ya ajali kazini ikiwemo kufanya kazi muda mrefu bila kupumzika.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyopewa jina la Usalama na Afya kama Kitovu cha Mustakabali wa Kazi (Occupational Safety and Health (OSH) imeeleza kuwa mabadiliko ya mazingira ya kazi, teknolojia za kisasa na watu kufanya kazi popote pale na wakati wowote pamoja na ukosefu wa usalama kazini ni sehemu ya mambo yanayosababisha vifo hivyo kila siku duniani.
Katika taarifa yake wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo jana (Aprili 18,2019) New York Marekani, Mtaalam wa ILO kuhusu usalama kazini, Manal Azzi amesema katika mazingira hayo wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi zaidi na zaidi na hawana muda wa kupumzika hali inayoweza kusababisha magonjwa ya akili, msongo wa mawazo na hata magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile saratani na moyo.
“Watu mbalimbali wanafanya kazi kwa njia mbalimbali ikiwemo simu, kompyuta mpakato unazoweza kwenda nazo kila pahali. Intaneti inapatikana kwa kila mtu, simu za kimataifa zinafanya mtu aweze kupatikana wakati wowote,” amesema Azzi katika taarifa hiyo.

Katika mapendekezo ya ripoti hiyo, ILO inaeleza kuwa ili kukabiliana na hali hiyo zinatakiwa ziwepo sera bunifu za ajira zinazojali afya ya umma na kuimarisha sheria za viwango vya kazi kimataifa na kitaifa.
Pia tathmini ifanyike kwa teknolojia na matumizi ya mifumo ya kidijitali, maroboti ambazo zinaweza kuathiri afya ya kisaikolojia ya mfanyakazi kama hazitatumiwa kwa usahihi.
Soma zaidi:
Mamlaka za ajira zimeshauriwa kupitia upya mabadiliko ya utendaji wa kazi yanayoruhusu watu wengi kuajiriwa na wakati huo huo wanafanya kazi zinazowaletea shinikizo na hofu ya kupoteza kazi na kuingiliwa kwa faragha zao.
Ripoti hiyo imetolewa wakati wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwa katika maandalizi ya Siku ya Usalama Kazini itakayofanyika Aprili 28, 2019.