Huyu ndiye bilionea mpya wa madini Tanzania

June 24, 2020 12:47 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Haniniu Laizer, moja ya wachimbaji wadogo wadogo wa madini Mirerani mkoani Manyara.
  • Amepata mawe mawili ya Tanzanite yenye thamani ya Sh7.44 bilioni. 
  • Serikali imeamua kuyanunua kwa bei inayoendana na thamani yake. 

Dar es Salaam. Haniniu Laizer, moja ya wachimbaji wadogo wadogo wa madini Mirerani mkoani Manyara, ameukata. 

Ndani ya sasa chache, licha ya kuwa shughuli yake ni uchimbaji mdogo mdogo wa madini, kwa sasa ameongeza sifa nyingine: Bilionea.

Ubilionea wa Laizer unakuja siku chache baada ya kufanikiwa kupata mawe mawili ya madini ya Tanzanite, yakiwa na ukubwa kuwahi kurekodiwa tangu shughuli za uchimbaji madini zianze kufanywa katika eneo hilo wilayani Simanjiro miaka kibao iliyopita.

Jiwe la kwanza alilofanikiwa kulipata Laizer katika mgodi wake lina uzito wa kilo 9.27 na thamani ya Sh4.368 bilioni wakati jiwe la pili alilotia kibindoni lina uzito wa kilo 4.1 na thamani ya Sh3.75 bilioni.

Kwa pamoja, kwa lugha ya vijana mtaani, Laizer ameotea mzigo wenye thamani ya Sh7.44 bilioni.

Mafanikio hayo ya Laizer yamefanya Serikali ya Tanzania kumwekea hafla maalum ya kuyatambua.

“Moja ya mambo tutakayofanya katika tukio la leo ni kuyatambua mawe makubwa ya Tanzanite ambayo hayajawahi kutokea tangu uchimbaji wa madini Mirerani uanze. Pia, kuweka historia mawe haya mawili yananunuliwa na Serikali,” amesema Prof Simon Msanjila, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini.

Vipande viwili vya madini ya Tanzanite anavyomiliki Haniniu Laizer. Picha|Wizara ya Madini. 

Kwa kawaida wachimbaji wa madini huchimba hadi wastani wa mita 100 chini ya mgodi lakini kwa mujibu wa Waziri wa Madini, Dotto Biteko, Laizer alipata madini hayo ndani ya mita 1,800.

Hata hivyo, Biteko hajaweka bayana namna bilionea huyo mpya alivyofika umbali huo mrefu kwa kuwa mara nyingi wachimbaji wadogo huwa na vifaa duni vya kuchimbia madini jambo linalowapunguzia ufanisi.

“Huyu tunataka awe salama, isije tukawa tumemdisplay hapa tukarisk maisha yake. Tumefanya hivi ili kuonyesha Watanzania kuwa wachimbaji wadogo wanaweza kufanya makubwa kuliko tulivyokuwa tumeaminishwa siku za nyuma,” Biteko ameeleza katika hafla hiyo iliyofanyika Mirerani, Kaskazini mwa Tanzania.


Soma zaidi:  Rais Magufuli awaweka kitanzini wakuu wa mikoa wasiojenga vituo vya kuuzia madini


Kutokana na madini hayo kuwa ni historia, Biteko amesema Serikali imeamua kuyanunua kwa bei inayoendana na thamani yake bila kumdhulumu kiasi cha fedha mchimbaji huyo.

“Tulipoomba aiuzie Serikali hakuwa na neno la kusema…akasema mimi nipo tayari kuiuzia Serikali na msiache kukata hata shilingi moja ya Serikali. Huyu hata mbinguni atafika kwa sababu ya uaminifu,” amesema.

Katika hafla hiyo, Laizer amekabidhiwa hundi ya mfano ya Sh7.44 bilioni baada ya kukamilisha taratibu za mauzo ya kuiuzia Serikali.

Rais John Magufuli amempongeza Laizer na wachimbaji wenzie kwa mafanikio hayo wakati akiongea moja kwa moja na simu na Biteko katika hafla hiyo.

“Hii ndiyo faida ya wachimbaji wadogo wadogo na hili ni kudhihirisha kuwa Tanzania sisi ni matajiri,” amesema Rais Magufuli. 

Enable Notifications OK No thanks