Hulka ya upole inapobadilika kuwa umafia

September 6, 2021 12:28 pm · Herimina
Share
Tweet
Copy Link
  • Filamu ya ‘The Devil Judge’ inaeleza kisa chote.
  • Inaomhusu kijana mpole na kuwa mtu anayeogopwa zaidi.
  • Anatumia cheo chake cha uhakimu kulipiza kisasi.

Dar es salaam. Baadhi wamekuwa wakisema hawavutiwi na filamu za Kikorea, kwa kisingizio cha kwamba zimejaa maudhui ya mahaba kupitiliza. 

Kwa leo, sijui watasingizia nini kwa sababu nimewasogezea filamu ambayo mapenzi ni punje moja ya mchele kwenye gunia la mahindi.

Bila shaka umekutana na watu ambao wanasifika au kupendwa kutokana na tabia zao za kupendeza.

Upole, uchapa kazi na pengine uaminifu lakini ulishawahi kukutana na mtu anaesifika kwa kutokuwa na huruma au Waswahili tunapenda kusema ‘mafia’?

Filamu hii ya “The Devil Judge” yaani hakimu shetani inakukutanisha na hakimu ‘mtata’ kuwahi kutokea katika ardhi ya wana filamu.

Ni kijana Kang Yo Han, anaebadilika kutoka kwenye hulka ya upole na kuwa mtu asiye na huruma wala kukubali kushindwa.

Han alizaliwa katika familia yenye kipato cha wastani na siku zote alikuwa akipendwa kwa upole wake na kupenda kushirikiana na wenzie.

Wenzake, walifarijika kuwa naye kwenye kutazama filamu, kushiriki kwenye michezo ya kufurahisha, na hata katika shughuli za kusaidia watu wenye uhitaji. Ilikuwa ni kawaida ya Han na rafiki zake kufanya shughuli hizo pamoja.

Yote hayo yanabadilika baada ya familia ya Han kuteketezwa kwenye siku ambayo ilipaswa kuwa ni ya furaha kwake.

Khan aliamua kufanya kila liwezekanalo kuwa jaji ili alipize kisasi. Picha| Ikigai Pop.

Mwanzo wa umafia wa han 

Umafia  wa Han, unatokana na mrundikano wa maumivu. 

Kwenye jamii ya watu ambao wanakuchukulia poa, kuna namna fulani hivi wanakuumiza na wanaona ni sawa tu huku wakitegemea hakuna kitu unaweza kufanya.

Lakini kwa Han haikuwa sawa, hasa baada ya walimwengu kumchukua ndugu aliyekuwa moyoni mwake. 

Siku hiyo inapowadia, upole wa Han unayeyuka na maumivu yaliyopo moyoni yanaanza kumwagikia. Inapofika siku hiyo, ulimwengu haupo tayari na haukutarajia.

Baada ya mpendwa wake kuuwawa, Han anatafuta kisasi kwa kupambana ili apate mamlaka ya kuwakomesha maadui zake. Ni mamlaka ipi isipokuwa uhakimu?

Ngazi hiyo ndiyo hatua pekee ya kutoa hukumu itakayowafaa maadui zake hivyo anapambana kuifikia na hakubali chochote kije mbele yake na malengo yake.

Safari hiyo inamkutanisha na mwanadada Jung Sun Ah, binti mwenye ndoto za kuwa polisi maarufu nchini Korea ya kusini. Wawili hawa wanajikuta wakishirikiana kwenye mambo mbalimbali ya kisheria.

Baniani mbaya kiatu chake dawa

Siku zote jamii haipendi baadhi ya mambo yajulikane na pale anapopatikana mtu wa kuyachimba mambo hayo na kuyaweka hadharani, basi ataonekana adui wa jamii.

Bila shaka mahakimu, wanasheria na waandishi wa habari wanaweza kuelewa ninachozungumza.

Kwa Han ambaye ni hakimu, ufukunyuku wake na hukumu zake zinasababisha wengine kupoteza maisha, vyeo na kazi.  Jambo hilo linampa maadui wengi ikiwemo viongozi wakubwa kwani hawafurahishwi na mambo yao kuwekwa hadharani.

Maadui zake wanafikia hatua ya kumuwekea mitego na vikwazo vikali  ili atolewe kwenye nafasi hiyo na ikishindikana, basi maisha yake yarudi kwa muumba wake.

Hata hivyo, umakini wa hali ya juu wa kijana huyu unasababisha juhudi zao kutozaa matunda na badala yake dawa yao iliyopo jikoni inazidi kutokota ikiwangoja.

Licha ya kuwa vigogo wanatetema, wanyonge wa kwenye jamii wanamuona  kama mkombozi wao, huku wakivutiwa na mtindo wa Han wa kutoa hukumu kali  bila kujali urafiki, undugu, cheo wala pesa. 

Nikiyasema yote, huenda nikawamalizia uhondo, kwanini usipate muda wa kukutana ana kwa ana na wahusika wababe katika filamu hii?

Kutana na Park Ji Sung aliyeigiza kwenye filamu ya “Kill me Heal me”, na nyota wengine wakali akiwemo Kim Min Jung, Park Gyu Young, na wengine wengi ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye uigizaji.

“Kamsahamnida” kwa kuendelea kufuatilia “Nukta the Podcast’’.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW