Hukumu kifo cha mwanahabari Jamal Khashoggi yachukua sura mpya
- UN yasema walioamuru mauaji hayo yatokee wameachwa bila kuchukuliwa hatua.
- Mahakama nchini Saudi Arabia imewahukumu watu watano adhabu ya kifo kwa mauaji ya mwana habari huyo wa gazeti la Washington Post la Marekani.
- Aliuawa mwaka jana katika ubalozi wa Saudi Arabia mjini Instabul, Uturuki.
Mtaalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu mauaji ya kiholela, Agnes Callamard amesema ameshtushwa sana na hukumu ya kifo waliyopewa wanaodaiwa kumuua mwandishi wa Habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi huku walioamuru mauaji hayo wakiachwa bila kuguswa.
Tamko la Callamard limekuja baada ya Desemba 23, 2019, Mahakama nchini Saudi Arabia kuwahukumu watu watano adhabu ya kifo kwa mauaji ya mwana habari huyo wa gazeti la Washington Post la Marekani.
Pia watu wengine watatu walihukumiwa kifungo cha pamoja cha miaka 24 huku Wasaidizi wawili wakuu wa Mwanamfalme, Mohammed bin Salman walifutiwa mashtaka kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha katika kesi hiyo ya mauaji.
Katika taarifa iliyotolewa na UN jana (Desemba 26, 2019), Callamard amesema amepigwa na mshtuko mara mbili baada ya watu watano kuhukumiwa kifo juma hili kwa mauaji ya Khashoggi kufuatia kesi iliyoendeshwa kwa siri.
”Wauaji walikutwa na hatia na kukatiwa hukumu ya kifo. Nikipinga hukumu ya kifo huu ni mshituko wa kwanza kwangu. Hata hivyo, wale walioamuru mauaji hayo siyo tu kwamba wameachwa huru lakini hawakuguswa kabisa na uchunguzi wala kesi, huu ni mshtuko wa pili kwangu, huu ni ukiukaji wa haki na dharau isiyokubalika kwa waathirika,” amesema Callamard katika taarifa hiyo.
Amesema chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu kifo cha Khashoggi yalikuwa ni mauaji ambayo ufalme wa Saudi Arabia ulipaswa kuwajibishwa.
“Kesi hii inahitaji uchunguzi katika mnyororo wa maamuzi, ili kubaini muandaaji, pamoja na waliochochea, walioruhusu au kufumbia macho mauaji hayo kama vile mwana mfalme” amesema mtaalam huyo.
Soma zaidi:
- UN yatoa neno hukumu kifo cha mwanahabari Jamal Khashoggi
- Uhamiaji waeleza sababu za kuendelea kumshikilia Mwanahabari Kabendera
- Mwanahabari Erick Kabendera ashitakiwa kwa utakatishaji fedha, uhujumu uchumi
Callamard amesisitiza kwamba hakuna wakati wowote katika kesi hiyo uliofikiria wajibu wa serikali kwa sababu maafisa 18 wa Saudia waliokuwepo kwenye ubalozi wa Saudia Arabia mjini Instanbul, Uturuki kwa zaidi ya siku 10 walisafisha eneo la uhalifu.
Katika tathmini yake ya hukumu hiyo, Callamard amesema jaji anaonekana kuhitimisha kwamba mauaji ya Khashoggi ilikuwa ni ajali kwa kuwa inaonekana hakukuwa na dhamira , lakini bado amewahukumu washitakiwa kifo katika ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa za haki za binadamu.
“Hukumu ya kifo itolewe tu ambapo mazingira ya kesi yalifuata haki mojawapo katika mauaji ya kimataifa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mtaalam huyo pia amekosoa mwenendo wa usikilizaji wa kesi hiyo ambao ulifanyika kwa faragha huku watuhumiwa walirejelea kusema mara kadhaa wakati wa kesi hiyo kuwa walikuwa wanatekeleza amri.
Amesema mwendesha mashtaka katika kesi hiyo alinukuliwa hadharani kuwa Saud al-Qahtani ambaye ni mshauri binafsi wa mwana mfalme alitaka Khashoggi atekwe kwa madai kuwa alikuwa tishio la usalama wa Taifa.
Hata hivyo, mshauri huyo hakushitakiwa kwa lolote na yuko huru huku balozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Mohammad al-Otaibi, aliyeruhusu ofisi ya ubalozi wake kuwa sehemu ya uhalifu hakukutwa na hatia yoyote.
Mtaalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu mauaji ya kiholela, Agnes Callamard (pichani) amesema ameshtushwa sana na hukumu ya kifo waliyopewa wanaodaiwa kumuua mwandishi wa Habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi huku walioamuru mauaji hayo wakiachwa bila kuguswa. Picha|UN.
Juni 2019, Callmard alitoa ripoti kufuatia uchunguzi wa miezi sita wa mauaji ya Khashoggi. Ripoti hiyo ilitathmini ushahidi kwa misingi ya sheria za kimataifa za haki za binadamu na kufikiria hatua za kuchukuliwa ambazo zingezuia mauaji hayo.
Khashoggi aliyekuwa mkosaji wa familia ya kifalme ya Saudi Arabia, aliuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul mwaka jana na wanaodaiwa kuwa ni timu ya majasusi wa Saudia.
Mauaji ya Khashoggi yaliishangaza dunia na pia raia wengi wa Saudia, ambao walishtushwa na tukio la raia wa nchi hiyo kuuliwa na mawakala 15 wa serikali ndani ya mojawapo ya balozi za ufalme huo.