Hizi ndizo shule zinazong’ang’ania mkiani matokeo kidato cha sita

April 25, 2019 11:08 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Shule hizo ni Al-Ihsan Girls na Ben Bella za Mjini Magharibi, Zanzibar na Meta ya mkoani Mbeya ambazo zimeingia kwenye orodha ya 10 za mwisho zaidi ya mara moja katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. 
  • Ben Bella imekuwa kinara kwa kukaa muda mrefu katika orodha hiyo. 
  • Sababu za shule hizo kufanya vibaya zatajwa ikiwemo ukosefu wa walimu na mabweni kwa wanafunzi.

Dar es Salaam. Ni kipindi cha lala salama kwa watahiniwa wa kidato cha sita ambao wanajiandaa kufanya mtihani wa kitaifa kukamilisha safari ya elimu ya sekondari. 

Wakati huu wanafunzi na shule mbalimbali wako katika maandalizi kuhakikisha wanafanya vizuri katika mitihani hiyo. Shule zinazotamba 10 bora zinahakikisha hazitoki kwenye kundi hilo ili kuendelea kujipatia sifa njema katika utoaji wa elimu bora hapa nchini. 

Hata zile shule zinazoning’inia mkiani yaani kwenye orodha ya shule 10 za mwisho kitaifa, zinafanya kila linalowezekana kutoka ili kuepuka aibu na kujijengea heshima  nzuri itakayosaidia ziendelee kuwepo katika ushindani wa kutoa elimu bora nchini. 

Licha ya jitihada hizo za walimu na shule katika ufundishaji, zipo baadhi ya shule ambazo zimeng’ang’ania mkiani kwa muda mrefu na huenda zikaendelea kubaki katika orodha hiyo ya shule 10 za mwisho kitaifa iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.

Uchambuzi uliofanywa na www.nukta.co.tz wa matokeo ya mtihani wa kidato cha sita kwa miaka mitano iliyopita yanayotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) umebaini kuwa shule tatu za Al-Ihsan Girls na Ben Bella za Mjini Magharibi, Zanzibar; na Meta ya mkoani Mbeya zimekaa kwa muda mrefu katika orodha ya shule 10 za mwisho kitaifa ndani ya kipindi hicho. 

Tangu mwaka 2014 hadi 2018, shule hizo tatu zimejitokeza zaidi ya mara moja katika orodha hiyo, jambo linaloacha maswali mengi kuhusu elimu inayotolewa katika shule hizo huku shule nyingine zikiingia mara moja na kutoka. 

Shule ya wasichana ya Ben Bella ndiyo imekuwa kinara wa kukaa kwa muda mrefu katika orodha ya shule 10 za mwisho kitaifa  ambapo katika miaka mitano iliyopita ilifanikiwa kutoka kwenye orodha hiyo mwaka 2015 tu. 

Shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1924, miaka minne iliyobaki ileendelea kuwepo kwenye orodha hiyo ambapo katika matokeo ya mwaka jana ilishika nafasi ya pili kutoka mwisho juu kidogo ya Golden Ridge ya mkoani Geita.

Shule nyingine 10 za mwisho mwaka 2018 ni Forest Hill ya Morogoro, Jang’ombe (Mjini Magharibi), Jangwani (Dar es Salaam), St James Kilolo (Iringa) na White Lake ( Dar es Salaam). Nyingine ni Aggrey ya Mbeya, Nyailigamba (Kagera) na Musoma Utalii ya Mara.

Wanafunzi wa shule wa wasichana ya Ben Bella wakati wa miaka 90 ya shule hiyo mwaka 2014. Picha|Mtandao.

Wakati Ben Bella inayofundisha michepuo ya PCB (Fizikia, Kemia na Biolojia), PCM (Fizikia, Kemia na Hisabati) na CBG (Kemia, Biolojia na Geografia) ikiongoza kukaa kwa muda mrefu kwenye orodha hiyo, Shule ya Sekondari ya Meta nayo ni miongoni mwa shule zilizojitokeza mara nyingi katika orodha ya shule za mwisho kwa miaka mitano iliyopita.

Shule hiyo inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), imeingia mara mbili katika orodha ya shule 10 za mwisho katika kipindi hicho.

Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2015 ambapo ilikuwa ya mwisho kitaifa ikiungana na shule za Bariadi  ya mkoani Simiyu, Ilongero (Singida), Lwangwa (Mbeya), Kilangalanga (Pwani), Kaliua (Tabora) na Logoba (Pwani. Nyingine ni Iwalanje (Mbeya), Mtwara Technical (Mtwara) na Kwiro ya Morogoro.

Lakini mwaka uliofuata wa 2016 ilikaza kidogo na  kujinasua katika orodha hiyo licha ya kuwa matokeo yake hayakuwa mazuri sana ambapo 2017 ikarudi tena kwenye kundi hilo ikiungana na mwenzake Ben Bella. 

Mwaka jana ilikaza kidogo na kuondoka kwenye orodha hiyo lakini bado ina kibarua kigumu  katika mtihani mwaka huu wa 2019 wa kuhakikisha hairudi tena kwenye shule za mwisho.

Kwa wanaoifahamu Meta miaka ya nyuma ilikuwa na historia nzuri ya kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa na ingekuwa vigumu kuingia kwenye shule 10 za mwisho enzi zake.


Zinazohusiana:


Shule ya wasichana ya Al-Ihsan ya Zanzibar nayo imeingia mara mbili mfululizo katika shule 10 za mwisho yaani mwaka 2016 na 2017 ambapo iliungana na Ben Bella na Meta na shule nyingine. 

Katika orodha hiyo ya mwaka 2016, shule sita za sekondari zilizoko Zanzibar ambazo ni Mpendae, Ben Bella, Tumekuja, Jang’ombe, Kiembesamaki, na Lumumba nazo zilifanya vibaya.

Lakini mwaka jana, shule hiyo ya  wasichana iliyoanzishwa na shirika Afrika Muslim Agency February 2002 ilijinasua katika orodha hiyo na bado itakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha hairudi tena mkiani mwaka huu.

Nini kimetokea kwa shule hizo hasa Ben Bella ambayo kwa miaka minne ya hivi karibuni imekuwa ikiingia kwenye orodha ya shule 10 za mwisho?

Kwa wanaoifahamu shule ya sekondari Meta miaka ya nyuma ilikuwa na historia nzuri ya kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa na ingekuwa vigumu kuingia kwenye shule 10 za mwisho enzi zake. Picha| Mtandao.

Nini kimezikumba shule hizo?

Kutokana na ufaulu duni wa shule hizo, yapo mambo mbalimbali yanayosababisha shule hizo zishindwe kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ikiwemo sababu sugu kama ukosefu  wa mabweni kuwawezesha wanafunzi kukaa shule muda wote kunatajwa kama sababu inayowafanya wanafunzi wasifanye vizuri katika masomo yao. 

Mathalani, shule ya wasichana ya Al-Ihsan ambayo matokeo yake yamekuwa siyo ya kuridhisha haina mabweni, jambo linalowafanya wanafunzi kukosa muda wa kujisomea katika mazingira mazuri na tulivu. 

Uhaba wa walimu hasa katika shule zinazomilikiwa na Serikali unawanyima fursa wanafunzi kupata maarifa na ujuzi kuwawezesha kujibu mitihani na kukatisha ndoto za kuendelea na masomo ya elimu ya juu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, SMZ ina walimu 5,324 wanaofundisha shule 203 zenye wanafunzi 114,946 ambapo kati ya hizo 20 ni za kidato cha tano na sita. 

Kulingana na idadi ya shule hizo, Zanzibar inahitaji takriban walimu 6,276 ili kuweza kukidhi mahitaji yote ya wanafunzi ambapo kati ya hao 3,610 ni wa kidato cha tano na sita.

Hata hivyo, juhudi za www.nukta.co.tz kuwapata walimu wakuu wa shule za Meta na Ben Bella ili kuelezea walivyojipanga kuongeza ufaulu katika shule zao hazikufanikiwa kutokana na simu zao kuita bila kupokelewa. 

Enable Notifications OK No thanks