Hivi ndivyo unavyoweza kufurahia kutazama filamu nyumbani
- Ni kupitia programu tumishi ya Netflix, YouTube na chaneli zilizopo kwenye ving’amuzi kama DSTV.
- Utahitaji kutoboa mfuko kidogo kuona filamu hizo.
Dar es Salaam. Kama kawaida, lazima upate nyenzo za kufurahia wikiendi yako hasa baada ya Serikali kushauri kupunguza matembezi na safari zisizo za lazima.
Kwanini usibaki nyumbani na kufurahia filamu wewe na familia yako? Kama umewahi kusikia kuhusu programu ya Netflix, leo ninataka kukujuza zaidi.
Mambo yakoje huku?
Netflix ni programu ya kuonyesha filamu za muendelezo (TV Series) na filamu za kawaida (Movies) kwa njia ya mtandao itakayokuhitaji kuunganishwa na intaneti na pia utoboe mfuko kidogo kwa gharama kuanzia Sh18,489 hadi Sh27,746 kwa mwezi.
Kupitia programu hiyo unayoweza kutumia kwenye simu au kompyuta, utapata vifurushi vitatu kikiwemo cha chini (Basic) kati (Standard) na kikubwa (Premium) ambavyo vyote vina bei yake.
Kifurushi cha chini kinagharimu Sh18,489 huku ukiwa hauna uwezo wa kuangalia filamu zenye ubora wa hali ya juu (High definition-HD) na unaweza kuangalia filamu kwenye skrini moja tu.
Pia, kifurushi cha kati kinagharimu Sh23,117 huku kikiruhusu skrini mbili kutazama filamu kwa wakati mmoja.Yaani kama una “Bae” anaweza kutazama filamu kwa kutumia simu yake huku kifurushi kikubwa kinachogharimu Sh27,746 kikiwezesha skrini nne.
Zinazohusiana
- Filamu zitakazokusaidia kumalizia wiki kwa furaha
- Kama ni mahaba basi filamu ya “The Photograph” ni mwisho wa reli
- Vin Diesel arejea na filamu ya “Bloodshot” kumbi za sinema
Kwa lugha rahisi ni kwamba, siyo lazima ulipe peke yako. Unaweza jichanga na masela watatu wanaojielewa Sh6,936.5 kwa kila mmoja na kisha mkafurahia filamu za kawaida na zile za muendelezo kwa kipindi cha mwezi mzima bila kikomo.
Humo kuna kila aina ya filamu ni wewe tu kuchagua unataka kuangalia ipi, wakati huu ambao kumbi za sinema zimefungwa ili kuwakinga watu na maambukizi ya Corona.
Mbali na Netflix, mtandao wa Youtube nao una filamu nyingi ambapo huku ni intaneti yako tu ndiyo itakuwezesha kuangalia filamu unazotaka hasa zile ambazo zinatazamwa na kila mtu.
Pia unaweza kulipia kifurushi chochote cha king’amuzi unachotumia ambacho kinakuwezesa kupata chaneli zinazoonyesha filamu.
Mfano kwa Dstv, vifurushi vyote kuanzia Sh19,000 vina chaneli za M-Net na zinginezo zinazoonyesha filamu.
Kuna nini kinaendelea huko Netflix? Kaa chonjo, kujuzwa na Nukta (www.nukta.co.tz) juu ya filamu zinazoonyeshwa kwenye chaneli mbalimbali na hata programu hiyo.
Maamuzi mkononi mwako.