Hivi ndivyo mali inavyoweza kumbadilisha binadamu mwenye moyo wa malaika

May 1, 2020 10:36 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kisa cha filamu yenye kusimulia maisha ya Binti aliyepata zari la mentali baada ya kurithi mali za bosi wake.
  • Furaha ya milele aliyoidhani baada ya kuona maisha yanamnyookea inabadilika kuwa msiba baada ya sintofahamu kuanza kutokea.
  • Vifo, mate ya fisi na uroho wa fedha unabadilisha maisha ya Katie ambaye ndiyo kwanza,utamu wa penzi la mume wake unamkolea.

Dar es Salaam. Ni ijumaa nyingine ambayo hauna budi kuvuta pumzi mpya na kuangalia vipi unaweza kuondoa mawazo ya wiki nzima huku ukiendelea kuwa salama na kujiburudisha kwa msaada wa simu au kompyuta yako.

Utajisikiaje kama utanunua intaneti ya jigabaiti moja (GB1) tu kwenye kifurushi chako cha kila siku ili kuondoa mawazo ya wiki nzima kwa kutazama filamu moja? 

Ungana na mimi kwenye safari hii ya kukutoa kwenye ulimwengu wako wa sasa na kuingia katika filamu ya “Dangerous Lies” kupitia mtandao wa Netflix.

“Asante Katie, nisingeweza kufikia hapa bila wewe. Mwangalizi wangu mpya, mwenzi na rafiki,” ni maneno ya Leonard (Elliott Gould) kwa mwangalizi wake Katie (Camila Mendes). 

Huenda muda huu usingeweza kujirudia kwani Leonard anafariki. Ni habari ambazo hakika siyo za kufurahisha kwa Katie hasa baada ya mzee huyo kutokuwa na watu wengi nyuma yake na akimfahamu kwa miezi minne na nusu tu kabla ya jina lake kuwa marehemu.

Unaweza kutabasamu na kuhamaki baada ya Leonard ambaye enzi za uhai wake alimiliki mali za kutosha na jumba la kifahari kuchukua maamuzi ya kuandikisha mali zake zote kwa jina la Katie.

Ndiyo ni zali la mentali lililo mwangukia binti huyo ambaye pamoja na mpenzi wake aliyesaidia shughuli za usafi za hapa na pale kwa mzee Leonard pesa kwao zilikuwa ni za manati.


Zinazohusiana


Yaweza kuonekana kama ni baraka iliyojificha lakini hakuna kizuri kinachokuja bila gharama kwani hata pepo ina gharama yake. Kwanini nimesema hivyo?

Baada ya Katie na mpenzi wake kuhamia kwenye Jumba hilo la kifahari wanajikuta wakiikumbuka amani waliyokuwa nayo enzi za ukabwela baada ya visa kuanza kuwanyemelea huku watu waliozitolea udenda mali za mzee Lonard wakianza kuibuka.

Kufungua mabegi yaliyojaa pesa, visa na vifo ni sehemu ya filamu hiyo inayoshauriwa kutazamwa na watu wenye miaka zaidi ya 13. 

Bado haujanunua bando lako la intaneti kufuatilia kisa hiki kipya cha mwaka 2020? Kazi ni kwako kuamua kuiangalia filamu ya Dangerous Lies kupitia mtandao wa Netflix.

Enable Notifications OK No thanks