Hivi ndivyo gesi asilia inavyopunguza ukali wa maisha kwa wamiliki wa magari

January 15, 2020 11:32 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalamu waeleza kuwa inapunguza gharama za uendeshaji magari kwa takriban asilimia 50.
  • Nishati hiyo ni safi na salama kwa mazingira. 
  • Mfumo wa gesi asilia unaweza kutumika sambamba na wa mafuta kwenye gari.

Dar es Salaam. Wamiliki wa vyombo vya moto wanaweza kupunguza gharama za uendeshaji wa vyombo hivyo kwa takriban asilimia 50 ikiwa watageukia matumizi ya gesi asilia kuendesha magari yao na kuchangia katika utunzaji wa mazingira. 

Gesi asilia ni nishati safi na salama kwa magari ambapo bei yake iko chini ukilinganisha na petroli na humuwezesha dereva kutembea umbali mrefu kwa kutumia kiwango kidogo cha gesi.

“Ukitumia gesi asilia unashusha gharama za uendeshaji wa gari. Mfano kwa sasa hivi, gesi asilia kilo moja inauzwa Sh1,500 wakati petroli ni Sh2,200. 

“Hii gesi ya kilo moja ya 1,500 unaweza ukatembea kilomita 20 wakati petroli unaweza kutembea kilomita 12. Ukitumia gesi asilia unatembea umbali mrefu zaidi,” anasema Mratibu wa mradi wa ufungaji wa mifumo ya gesi asilia (CNG) kutoka Taasisi ya Teknolijia ya Dar es Salaam (DIT), Dk Esebi Nyari.  

Kwa mtu anayejaza mtungi wa gesi asilia wa kilo 15 ambao gharama yake ni Sh22,500 katika kituo cha Ubungo jijini Dar es Salaam anaweza kutembea zaidi ya kilomita 200. 

Iwapo dereva huyu atatumia petroli kwa gharama hiyo ya Sh22,500, atajaza wastani wa lita 10.2 kwenye gari lake ambazo zitamwezesha kutembea wastani wa kilomita tu 123 iwapo gari hilo linatumia lita moja kwa kilomita 12. 

Kwa hesabu hizo, matumizi ya gesi asilia ni nafuu zaidi kwa kuwa yatamsaidia kwenda wastani wa kilomita zaidi 80 ya yule wa petroli kwa gharama hiyo achana na nafuu nyingine ya kuwa kila kilo moja ya gesi asilia gari litatembea umbali wa zaidi ya kilomita 20 tofauti na kilomita 12 za mafuta.  

Dk Nyari aliyekuwa akizungumza na www.nukta.co.tz anasema nishati hiyo inamuwezesha dereva kupata huduma zote ambazo zinatolewa na mafuta ikiwemo kuwasha kiyoyozi na redio wakati unaendesha gari. 

Gesi asilia ni rafiki wa mazingira, kwa sababu ina kiwango kidogo cha  hewa ukaa ikilinganishwa na ile inayozalishwa na petroli inayosambaa angani na kusababisha ongezeko la joto na kuyeyuka kwa barafu, jambo linaloongeza kina cha bahari na kuathiri afya za watu na wanyama.

Mafundi wakiendelea na kazi ya kufunga mfumo wa gesi asilia kwenye magari ya wateja katika karakana ya DIT ya jijini Dar es Salaam. Picha|Daniel Samson.

Dk Nyari ambaye pia ni Mhadhiri wa DIT, anasema mfumo huo wa gesi unaongeza uhai wa gari kwa sababu ni salama kwa injini ya gari, ikizingatiwa kuwa gesi haina kemikali nyingi zinazoweza kuharibu kwa haraka vifaa vya gari kama ilivyo kwa mafuta ambayo yanachomwa kwa wingi. 

Rasilimali hiyo inaweza ikatumika katika kipindi ambacho bei za mafuta katika soko la dunia ziko juu ambazo husababishwa na ongezeko la gharama za usafirishaji na mizozo ya kisiasa katika nchi zinazozalisha nishati hiyo. 

Utumiaji kwa wingi wa gesi hiyo hasa katika vyombo vya moto, utasaidia kuinua uchumi wa wananchi na Taifa, kwa kuwa rasilimali hiyo iko nchini na mapato yanayopatikana yanataelekezwa katika shughuli za maendeleo. 

Ili kuhakikisha nishati hiyo inawafaidisha wamiliki wote wa vyombo vya moto, DIT wanaendelea na utafiti wa jinsi gesi asilia inavyoweza kutumika kuendeshea magari ya umma (daladala) na pikipiki za matairi matatu maarufu kama Bajaj

Kwa sasa wamefanikiwa kufunga katika magari binafsi hasa yale yanayohusika na kusafirisha watu katikati ya jiji la Dar es Salaam yakiwemo ya Uber na Bolt .


Zinazohusiana:


Unafungaje mfumo wa gesi asilia kwenye gari lako?

Ni muhimu kufahamu kuwa wakati unatumia mfumo wa gesi asilia huhitaji kubadilisha mfumo wa mafuta wa gari lako na wakati wa ufungaji hautaguzwa bali mifumo yote miwili itafanya kazi kwa kupokezana kutokana na uhitaji wa mtumiaji.

Kabla mtumiaji kufungiwa mfumo huo kwenye gari lake, Dk Nyari anaeleza, gari lake hukaguliwa katika karakana maalum iliyopo DIT jijini hapa ili kujiridhisha ubora wake na kama linafaa kuwekewa mfumo wa gesi asilia au la! 

“Tukishajiridhisha kama linaweza likawekewa mfumo, tunamwambia alipie ili tumuwekee mfumo. 

“Kule nyuma (kwenye buti) tunaweka mtungi kwa ajili ya kubebea gesi, halafu panakuwa na mpira unaopeleka gesi kwenye injini. Mbele kwenye injini kuna vifaa vya kudhibiti kiasi cha gesi kinachotumika kwenye injini,” ameeleza mtaalamu huyo wa ufundi wa magari. 

Vifaa vingine vinavyotumika katika mfumo huo ni pamoja na swichi, pampu za gesi (filling pump) ambazo hufanya kazi tofauti tofauti. 

Ni muhimu kufahamu kuwa wakati unatumia mfumo wa gesi asilia huhitaji kubadilisha mfumo wa mafuta wa gari lako na wakati wa ufungaji hautaguzwa bali mifumo yote miwili itafanya kazi kwa kupokezana kutokana na uhitaji wa mtumiaji. Picha|Mtandao.

Unatakiwa kuvunja kibubu kiasi gani kufunga mfumo huo?

Licha ya kuwa mfumo huo wa gesi asilia kuwa na faida nyingi, mtu anayetaka kufungiwa itabidi atoboe mfuko wake kulingana na mahitaji ya gari yake.

Gharama za ufungaji wa mfumo wa gesi asilia hutofautiana kulingana na aina ya injini na gari analotumia mmiliki wa chombo cha moto. 

Kwa magari madogo yenye injini ya C4 (chini ya cc1,800) yakiwemo aina ya Toyota IST, Spacio na Passo hugharimu Sh1.8 milioni huku magari yenye injini ya C6 ni Sh2.2 milioni, C8 (Sh2.5 milioni). 

Dk Nyari amesema kiasi hicho fedha kinachotolewa kinajumuisha gharama za vifaa, ufundi, na kumlipa mtu anayethibitisha (certify) mfumo uliofungwa, “kwa sababu hili gari likifungwa mfumo huo linapelekwa kukaguliwa kuangalia kama mfumo huu unakidhi vigezo vya kimataifa  au la.”

Hata hivyo, gharama hiyo haziyahusu magari yanatumia injini za GDI (Gasoline direct injection) yakiwemo magari aina ya Brevis, Crown, Vox na baadhi ya magari aina ya RAV 4 ambayo gharama zake ziko juu kidogo.

Kwa mmiliki wa magari hayo hutozwa kati ya Sh2.5 milioni hadi Sh5 milioni kulingana na upatikanaji wa vifaa ambavyo vingi huagizwa nje ya nchi.

Pia mifumo ya magari hayo iko tofauti kidogo na magari mengi, jambo linalohitaji umakini kuhakikisha gari linakuwa salama mara baada ya mfumo wa gesi asilia kufungwa.

Licha ya kuwa gharama za ufungaji kuonekana kubwa kidogo, iwapo yatafanywa mahesabu ya matumizi ya mafuta, matumizi ya gesi asilia kwa vyombo vya moto yanakuwa ni nafuu zaidi kwa mmliki kuliko mafuta. 

Unataka kupunguza gharama za uendeshaji na matengenezo ya gari lako ni wakati sasa wa kugeuki gesi asilia yenye usalama na uhakika kwa sababu inapatikana nchini. 

Katika makala ijayo tutaangazia muitikio wa Watanzania na dunia kutumia rasilimali hiyo, changamoto za usalama, sera na mikakati ya Serikali ya Tanzania kuendeleza rasilimali hiyo kwa manufaa ya wananchi. 

Enable Notifications OK No thanks