HESLB yafungua dirisha la maombi ya mikopo 2026/2027
- Waombaji wanatakiwa kuwasilisha maombi ndani ya siku 73 kabla ya Agosti 31, 2026.
Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imefungua rasmi dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2026/2027, huku mchakato huo ukitarajiwa kuhitimishwa Agosti 31, 2026.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, aliyekuwa akizungumza leo Juni 19, 2026 amesema dirisha hilo limefunguliwa sambamba na uzinduzi wa miongozo minne ya utoaji wa mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Kwa mujibu wa Dk. Kiwia miongozo hiyo inawahusu wanafunzi wa shahada za awali, stashahada, Stashahada ya Juu ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo (Postgraduate Diploma in Legal Practice) pamoja na mwongozo wa ruzuku za Samia Scholarship.
“Miongozo hii imeandaliwa ili kuwasaidia waombaji kuelewa sifa, vigezo na taratibu za kupata mikopo na ruzuku. Tunasisitiza wanafunzi wasome na kuzingatia maelekezo yote yaliyomo kabla ya kuanza kujaza fomu za maombi kupitia mfumo wa OLAMS,” amesema Dk Kiwia.
Mambo muhimu ya kuzingatia
Kwa mujibu wa HESLB, mwombaji anatakiwa kutumia namba sahihi ya mtihani wa kidato cha nne wakati wa kuwasilisha maombi ya mkopo ambayo pia itatumika wakati wa maombi ya udahili katika vyuo mbalimbali nchini.
Aidha, mwombaji mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea anapaswa kuwasilisha namba ya utambulisho wa Taifa (NIN) anapojaza fomu za maombi ya mkopo, huku wale ambao bado hawajafikisha umri huo wakiruhusiwa kuendelea na maombi hata kama hawana namba hiyo.
Kuhusu Samia Scholarship, Dk. Kiwia amesema wanafunzi 1,000 watakaofanya vizuri zaidi katika tahsusi za sayansi kwenye mitihani ya Kidato cha Sita ya mwaka 2026 watanufaika na ufadhili huo.
Bodi inasisitiza kuwa waombaji wote wanatakiwa kuwasilisha maombi ndani ya siku 73 kabla ya kufika Agosti 31, 2026 kuanzia leo Juni 19, 2026.
Licha ya kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuwezesha Watanzania wengi kutimiza ndoto zao za kielimu, HESLB imeendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waombaji wanaokiuka masharti na taratibu za utoaji wa mikopo.
Hivi karibuni, bodi hiyo iliwafikisha mahakamani wanafunzi 17 kutoka vyuo mbalimbali nchini kwa tuhuma za kughushi nyaraka na kutoa taarifa za uongo ili kujipatia mikopo ya elimu ya juu. Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa mahakamani.
Hivyo bodi inasisitiza ni muhimu kusoma vigezo na masharti vinavyopatikana kwenye tovuti ya bodi olas.hslb.go.tz ili kuepuka hatua za kisheria zinazoweza kujitokeza kutokana na ukiukwaji wa taratibu.