HESLB kuboresha mfumo wa utoaji, ukusanyaji mikopo elimu ya juu
- Mfumo huo utaonyesha mwenendo wa fedha anazopokea mwanafunzi kila mwaka.
- Waombaji wa mikopo kufungua akaunti kabla ya kujiunga chuo.
- Kudhibiti udanganyifu wa taarifa za waombaji.
Dar es Salaam. Wakati wanafunzi wanaotarajia kujiunga elimu ya juu wakisubiri majibu ya maombi ya kupatiwa mikopo ya kugharamia masomo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema iko kwenye mchakato wa kuboresha mfumo wa utunzaji kumbukumbu utakaowawezesha wanafunzi kujua kiasi cha mkopo wanachopata na madeni wanayodaiwa.
Mfumo huo ni mwendelezo wa uboreshaji wa taarifa na kumbukumbu za wanafunzi wa elimu ya juu ili kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa kwa wakati na kuwanufaisha wanafunzi wengine wanaojiunga vyuoni kila mwaka.
Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa HESLB, Veneranda Malima amesema katika mfumo uliopo sasa mwanafunzi hawezi kuona mwenendo wa fedha za mikopo anazopata kila mwaka, jambo ambalo limekuwa likiwanyima fursa ya kujiandaa kurejesha mikopo hiyo baada ya kumaliza chuo.
“Tumeingia katika mitandao mwaka 2010 lengo likiwa moja kuboresha jinsi ya utunzaji wa kumbukumbu za wanafunzi ambao wanapata mikopo kwasababu utakumbuka mtu unapofanya kitu kwa kutumia mkono uwezekano wa kufanya makosa ni mkubwa kuliko ukiruhusu mifumo ikafanya kazi,” amesema Malima.
Maboresho hayo yatahusisha wanafunzi kufungua akaunti na kujaza taarifa zao zote kwenye mfumo wa kompyuta hata kabla ya kujiunga na vyuo, kuziona taarifa za mienendo ya fedha wanazopata kwa ajili ya ada, vitabu, kujikimu, na mafunzo ya vitendo wakati wote wakiwa chuoni.
.“Tumekuwa tukizidi kuboresha siku hadi siku, mwanafunzi afungue akaunti tangu anaomba mkopo huko ndiko tunakoelekea kuanzia mwaka huu (2018/2019) ule mfumo umeboreshwa zaidi wanafunzi watakuwa wanaweza kuona kiasi cha mkopo anachokuwa amepangiwa kwa mwaka na vilevile atakuwa anaweza kuona kiasi gani atakuwa anadaiwa mwaka hadi mwaka,” amesema Malima.
Kupitia maboresho inayofanya HESLB malalamiko na makosa yanayofanyika wakati wa kujaza taarifa za kuomba mikopo ambapo imekuwa sababu kubwa ya wanafunzi wengi kukosa mikopo.
Malima amewakumbusha wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu kujaza taarifa za kweli wakati wanaomba mikopo kwani kushindwa kufanya hivyo kunawaondolea uhalali wa kupata mikopo unaoendana na hali ya kipato cha wazazi wake.
“Tunawahamasisha wanafunzi kwamba unapojaza taarifa za kuomba mkopo ziwe ni taarifa za kweli. Mwanafunzi anaweza kuwa ni yatima lakini ni kweli amethibitisha?” amefafanunua Malima.
Kwa mujibu wa HESLB katika mwaka 2017/2018 Serikali ilitenga bajeti ya 427 bilioni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ambapo waliopata mikopo hiyo walikuwa 33,244 kati ya zaidi ya 66,000 waliotuma maombi.
Akizungumzia kuhusu wanafunzi kukosa mikopo licha ya kuwa na sifa zote, Afisa Mikopo Mwandamizi wa HESLB, Daudi Elisha amesema wanafunzi wengi wanashindwa kuthibitisha taarifa wanazojaza ikiwemo kuambatanisha vyeti vya elimu, cheti cha kuzaliwa na hata vifo vya wazazi kwa watoto ambao ni yatima.
Amebainisha hata kama mwanafunzi amekosa mkopo kwa kushindwa kutimiza masharti yaliyowekwa, ana nafasi ya kukata rufaa ili apate haki yake.
Moja ya jengo la Chuo Kikuu cha Dodoma. Picha|
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwakilishi wa taasisi ya Universities Abroad, Tony Kabetha amesema changamoto inayowakabiliwa wanafunzi wengi ni uelewa mdogo wa matumizi ya teknolojia na kufanya makosa wakati wa ujazaji wa fomu za maombi ya mikopo.
“Wanafunzi wengi ambao tunawasaidia kwenye taasisi yetu bila upendeleo wengi wa hawa vijana tunawasaidia namna ya kuomba mkopo hawajui na wanaona shida, bodi ya mikopo tuanze kutoa hii elimu ya kuomba mikopo.” amesema Kabetha.
Kulingana na taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru aliyoitoa Julai 31, mwaka huu inaeleza kuwa wamepokea maombi ya waombaji mikopo zaidi ya 76,000 kwa njia ya mtandao kwa mwaka wa 2018/2019 ambapo bodi inaendelea kuchambua maombi yaliyowasilishwa na hadi kufikia Oktoba 15 itakuwa imetoa majina ya waliofanikiwa kupata mikopo.
Kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi walioomba mikopo, Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Siti Ngwali ameiomba Serikali kuongeza bajeti ya wanafunzi wanaotarajia kujiunga mwaka huu na kuwawezesha kupata nafasi ya kusoma ili kuongeza nguvu kazi ya taifa.
Katika Hotuba ya 2018/2019 ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako aliyoisoma bungeni April mwaka huu alinukuliwa akisema bodi (HESLB) imepanga, “ kutoa mikopo ya Shilingi billioni 427 kwa wanafunzi wapatao 123,285, kati yao wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa kwanza 40,544 na wanafunzi wanaoendelea na masomo wapatao 82,741.”