Hedhi: Ni fahari ya kuwa mwanamke

February 29, 2020 6:41 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link

Hedhi siyo ugonjwa wala ulemavu. Afya ya kisaikolojia inachagiza sana kuwa na hedhi salama. Jamii inayomzunguka binti au mwanamke itambue kuwa hedh ni fahari na jambo la kiafya kwa mwanamke. Picha|Mtandao.


  • Ufahari huu wa mwanamke utaonekana tu iwapo wanaomzunguka watauangalia katika mtazamo chanya.
  • Hedhi huja na dalili tofauti ikiwemo maumivu makali, kuumwa tumbo, kuharisha na kukosa hamu ya kula.
  •  Kipindi hiki ndicho cha kuwa na ukaribu zaidi na muhusika.

Nimejaribu kuangalia na kufuatilia kampeni kadha wa kadha zinazolenga kuielewesha jamii juu ya suala zima la hedhi kwa mwanamke.

Kimsingi bado uelewa haujawa ule wa kutosha, lakini pia hata heshima na mtazamo juu ya kipindi hicho muhimu kwa mwanamke ni hasi.

Wapo ambao wanabeza na kuona kinyaa jambo hili, hali inayomfanya binti aliye katika hedhi kukosa ujasiri pamoja na kutokuwa na uhuru kama siku nyingine.

Hedhi ni kipindi ambacho mwanamke hutokwa na damu ukeni. Hii ni hali ya kawaida ya kifisiolojia ambayo hutokea pale ambapo yai la mwanamke ambalo halikurutubishwa pamoja na mji wa mimba ambao ulikuwa umejiandaa kupokea yai lililorutubishwa hubomoka.

Hii hupelekea tishu ambazo sasa si sehemu tena ya mzunguko kutolewa ndani ya mwili kupitia uke katika mfumo wa kimiminika chenye mchanganyiko wa mabonge na kuitwa hedhi.

Mzunguko huu ni wa kila mwezi na huendelea hadi pale mwanamke atakapofikia ukomo wa hedhi yaani “Menopause”.

Lakini pia wakati wa ujauzito hapana mzunguko wa hedhi maana yai lilirutubishwa na sasa mji wa mimba unalea kiumbe kilichomo ndani yake yaani mtoto. 

Uonapo damu kipindi cha ujauzito ni vyema kumuona daktari na kueleza hali iliyokutokea.

Kipindi cha hedhi huambatana na mabadiliko kadha wa kadha na hutofautiana baina ya mwanamke na mwanamke. Haya huweza kuwa ya kisaikolojia, kimwili au kihisia. 

Ufahari huu wa mwanamke utaonekana tu iwapo wanaomzunguka watauangalia katika mtazamo chanya.

Hedhi huja na dalili tofauti ikiwemo maumivu makali, kuumwa tumbo, kuharisha, kukosa hamu ya kula nk. Kipindi hiki ndicho cha kuwa na ukaribu zaidi na muhusika. 


Soma zaidi: 


Usafi ni mojawapo ya jambo muhimu kipindi cha hedhi. Usafi huanzia katika suala zima la taulo za kike. Tambua ya kuwa, hedhi huweza anza bila dalili au ghafla. Yawezekana muhusika akawa hakujiandaa na kitendo cha damu kutitirika na kuchafua nguo kinafedhehesha.

Uonapo hili, kuwa mtulivu na usioneshe hali ya kushangaa kinachotokea. Msaidie kumuweka katika mazingira ya faragha ili aweze kujisitiri. Kama kuna nguo ya ziada ni wakati wa kumsaidia kumfunga na kuangalia namna ya kumpatia taulo (pedi) za kike. Kumfariji zaidi na msaidie kupata kinywaji cha baridi au moto.

Awapo nyumbani ni vyema kumpunguzia ama kumuondolea majukumu. Kwa wanawake wengi hedhi hudumu kwa siku mbili hadi tano. Katika hiki kipindi, ni vyema kuonyesha upendo na kujali. Ikiwa ni binti yako nyumbani, basi mpunguzie majukumu na mfanye aone hali ni ya kawaida.

Ikiwa ni mwenza wako, kipindi hiki ndicho cha kuchochea afya ya akili kwa matendo ya upendo. 

Kumbuka kuwa akili kuchangamka na kutokuwa na fikra hasi husaidia sana kupunguza msongo na mkazo hii hupelekea kuachiliwa kwa homoni za “endorphins” ambazo husaidia kujisikia furaha na kupunguza maumivu yaambatanayo na hedhi.

Asaidiwe katika kuoga kwa maji ya moto. Husaidia sana kuchochea mzunguko wa damu, misuli kulegea na mikazo kupungua.

Hedhi siyo ugonjwa wala ulemavu. Afya ya kisaikolojia inachagiza sana kuwa na hedhi salama. Jamii inayomzunguka binti au mwanamke itambue kuwa hedh ni fahari na jambo la kiafya kwa mwanamke.

Lakini uonapo dalili za damu kutoka kupita kiasi, maumivu makali kila hedhi, kutoka uchafu sana kipindi cha hedhi ni vyema kufika hospitali na kupata ushauri ama uchunguzi wa kitabibu iwapo kuna shida yoyote.

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Enable Notifications OK No thanks