Haviruhusiwi: Ubalozi wa Marekani Tanzania wapiga marufuku vifaa vya kielektroniki, mikoba mikubwa
- Ubalozi wasema kuanzia Mei 15, 2018 walinzi hawatahifadhi vifaa vya wageni hivyo ni marufuku kabisa kwenda navyo vikiwemo vifaa vya kielektroniki kama simu za mkononi.
- Washauri wageni kuacha vifaa hivyo majumbani ama watafute njia mbadala za kuhifadhi na si ubalozini hapo.
Dar es Salaam. Iwapo una mpango wa kwenda ubalozi wa Marekani nchini kuanzia Mei 15, chagua moja: kuacha vifaa vyako vya kielektroniki ikiwemo simu ya mkononi ama usiende kabisa kupata huduma unayohitaji.
Hali hiyo imekuja baada ya ubalozi huo kutangaza masharti mapya ya kiusalama kwa wageni wanaoenda kupata huduma mbalimbali za kibalozi kuwa kwa sasa vifaa walivyokuwa wakikatazwa kuingia navyo na kuviacha kwa maofisa wa usalama katika ofisi hizo hawataruhusiwa kwenda navyo kabisa.
“Kuanzia Mei 15 2018 ubalozi hautakuwa ukihifadhi vifaa vya watu ambao wanahitaji huduma za kibalozi. Wageni wote watapaswa kuacha vifaa vyote vilivyokatazwa majumbani kwao au watafute njia mbadala zilizo salama kuhifadhi vifaa hivyo,” inasomeka sehemu ya tangazo hilo lilochapishwa katika tovuti ya ubalozi huo.
Orodha ya vifaa ambavyo wageni wa Ubalozi wa Marekani Tanzania hawataruhusiwa kwenda navyo kwa ajili ya usalama. Picha na Ubalozi wa Marekani.
Vitu vilivyokatazwa mtu kuingia navyo ubalozini ni pamoja na simu, kompyuta na vifaa vyote vya kielektroniki nana fitness trackers,pia vitu habari kama CD, spika, flashi, viberiti, silaha au chochote ambacho kinaweza kutumika kama silaha, kisu au kitu chenye ncha kali. Vingine ni kamera au vifaa vyote vinavyohusiana na video ,tochi, ‘Memory card’ na spika za kuvaa masikioni. Kwa wabeba mabegi, ubalozi umepiga marufuku pochi na mabegi yenye ukubwa wa zaidi ya nchi 10 x 10 (25cm x 25cm) na vimiminika kama mafuta ya kupaka mwilini kama losheni.
Vitu vilivyoruhusiwa mgeni kuingia navyo ubalozini ni vifaa vya urembo vidogo (make-up ndogo), mkanda, kiasi kidogo cha chakula cha mtoto au maziwa, funguo sambamba na saa isiyokuwa ya Bluetooth au yenye uwezo wa kuchukua video. Vingine ni kiasi kidogo cha taulo ndogo za watoto (pampas), dawa zisizo za maji (Non-liquid medication) pia vitu ua kiti cha kubebea watoto ambacho kitaweza kupita katika mitambo ya xray
Pia tangazo hilo limesema mgeni atawajibika kuelezea kifaa chachote cha ugonjwa kabla ya ukaguzi wa kiusalama.