Hatua kwa hatua jinsi ya kufanya Forex
- Ni pamoja na kujifunza misingi ya biashara hiyo ikiwemo kuelewa soko na mambo yanayoathiri bei
- Anza kuwekeza kidogo kidogo, na ongeza mtaji kutokana na uzoefu.
Dar es Salaam. Mara baada ya kuangazia maana ya Forex na jinsi unavyoweza kupata faida katika makala iliyopita, sehemu hii ya pili inaangazia hatua za kufuata ili uweze kufanya biashara ya Forex kwa mafanikio.
Anza kwa kujifunza
Derick Paul mmoja ya vijana wa Tanzania wanaofanya biashara ya Forex ameiambia Nukta Habari kuwa kabla ya kuanza kuwekeza kwenye Forex ni lazima kuwa na unelewa wa misingi ya biashara hiyo ikiwemo istilahi zake na jinsi soko la Forex linavyofanya kazi inayojumuisha mifumo ya soko, na mambo yanayoathiri bei za sarafu.
“Haya mambo sio ya kukurupukia kwa sababu hata mimi wakati naanza, niliingia sana hasara, ni vizuri ujipe muda wa kupata ujuzi kwanza kabla ya kuwekeza” amesema Paul.
Mbali na kujifunza, Paul ameeleza kuwa unatakiwa kutengeneza mikakati ya biashara kwa kujifunza mbinu mbalimbali za biashara ya Forex, kama vile uchambuzi wa kiufundi (technical analysis), uchambuzi wa msingi (fundamental analysis), na biashara ya habari (news trading).
Paul anayefanya Forex kwa muda wa miaka miwili sasa ameongeza kuwa ni muhimu kwa mtu anayetaka kuanza kufanya Forex kutafuta mtu mwenye elimu ya juu na uzoefu mkubwa kuhusiana na biashara hiyo ambaye atamsaidia kuepukana na baadhi ya changamoto.
“Wapo watu wanajifunza kupitia YouTube, lakini ukweli nikwamba unaweza usiondoke na elimu ya kutosha kwa sababu hata kama hauta elewa huwezi kuuliza na kupata ufafanuzi, lakini pia wengi wanatumia lugha ya Kiingereza kwa hiyo unaweza pata shida sana kuelewa” ameeleza Paul huku akitaja hatua alizopitia ili kuanza rasmi biashara ndani ya Forex.
Fungua akaunti ya uwakala (Brokerage Account)
Ili kuanza kufanya biashara ya Forex ni lazima uchague wakala (Broker) ambaye utakuwa ukifanya nae biashara.
Kutokana na kuwa Tanzania bado haijatambua rasmi kisheria biashara ya Forex mawakala wengi ni wa kutoka nchi za nje hususan Nigeria na Afrika kusini ambao husimamia mchakato wako wa kufungua akauti na ndiye atakuwa anakulipa faida unazopata kutokana na biashara ya Forex.
Paul amesisitiza kuwa katika hatua hii ni muhimu kuwa makini kwa sababu ndiyo hatua ambayo watu wengi hutapeliwa hivyo unatakiwa kuchagua wakala ambae ana masharti rahisi ambayo yatakuwezesha kufanya biashara kwa urahisi akionya kuepuka mawakala ambao wanashauri kupewa akaunti husika ili wamfanyie biashara mwekezaji.
“Hapa mtu anatakiwa kuwa makini sana kwa sababu kuna mawakala wanajifanya wanataka kumfanyia mwekezaji biashara kwa kupewa akaunti kwa madai ya kukupatia faida kubwa. Wengi wa mawakala wa aina hiyo ni matapeli hakikisha wakala anatoa vigezo rahisi kutumia, huduma nzuri kwa wateja, na ada ndogo” amesisitiza Paul.
Mara baada ya kufanikisha zoezi la kufungua account yako, unaweza kufanya muamala wa kuweka pesa zako kwa kutumia namba ya malipo uliyoipata katika tovuti au programu tumishi ya wakala ambae umefanya usajili kupitia mitandao ya kawaida ya simu au benki.
Fanya mazoezi kwa akaunti ya ‘demo’
Baada ya kufanikiwa kuweka fedha zako kwenye akaunti Paul anaeleza kuwa majukwaa mengi ya Forex yanatoa uwezo wa kufanya biashara kwa mazoezi (paper trade) kabla ya kutumia pesa halisi.
Hivyo ni muda mzuri wa kujifunza mbinu za biashara na kuhakikisha mikakati yako inafanya kazi. Ni bora kugundua makosa yako katika hali ya mazoezi badala ya wakati unapotumia pesa halisi ingawa baadhi wa watu wanakiri kuwa kufanya biashara kwenye demo ni rahisi kuliko akaunti halisi.
Anza taratibu
Ukishahisi kuwa na ujasiri baada ya kufanya mazoezi ya kutosha unaweza kuanza kufanya biashara ingawa Paul anaeleza kuwa ni vema kuanza na kiasi kidogo cha pesa ili kudhibiti hatari, ukubwa wa mtaji unaweza kuongezeka kadri unavyopata uzoefu.
Kikawaida majukwaa mengi ya uwakala hupendekeza kiasi cha Dola 100 za Marekani au Sh250,000 kama kiwango cha kuanzia, ingawa yapo majukwaa yanayopokea kiasi cha chini yake.
Fuatilia na zoea kuendana na hali ya biashara
Mara baada ya kupata uzoefu kutoka kwenye mazoezi ya akaunti pamoja kuanza kwa kuwekeza kidogo kidogo unaweza kuendelea kufuatilia habari za soko, viashiria vya kiuchumi, na matukio ya kijiografia yanayoweza kuathiri bei za sarafu.
Pia ni muhimu kwa mwekezaji kuwa tayari kurekebisha mikakati kulingana na hali ya soko inavyobadilika.
“Katika hatua hii sasa ndiyo muda wa kupiga pesa na kutengezeza faida, kwa sababu unakuwa umeshapata uzoefu hivyo ni wewe tu na kulisoma soko linaendaje” ameeleza Paul.
Kweli pesa ipo ingawa si rahisi
Forex si biashara ya kupata pesa haraka kama watu wengi wanavyodhani, inahitaji muda kujifunza, kufanya mazoezi ya nadharia na vitendo ndipo uanze kuona matunda yake.
Miongoni mwa vijana waliochelewa kuona matunda ya Forex ni Frank Deo Magegere (23)ambaye amekuwa akifanya biashara ya Forex tangu mwaka 2019 akianza kwa mtaji wa Sh37,500.
Magegere anaeleza kuwa alipata faida ya Sh2,500,000 miaka miwili baadae yani mwaka 2021.
Magegere anaamini kiasi cha fedha alichokipata ni kidogo sana kulinganisha na kiasi ambacho wenzake alishuhudia wanatengeneza kupitia Forex huku akitaja ukosefu wa ujuzi na elimu kuhusiana na biashara hiyo kama kikwazo kikuu cha yeye kupata kiasi hicho cha pesa.
“Kilicho niponza sikuwa na elimu kuhusu Forex kwa maana nimeliwa sana pesa zangu, kwaiyo nimetumia muda mwingi sana kufanya lakini sijui mambo mengi kwa sababu nilifanya kwa mihemko baada ya kusikia kuna pesa nyingi sana naweza kupata kupitia Forex” anaeleza Magegere.
Hata hivyo, Magegere anaeleza kuwa baada ya kupata kiasi hicho aliamua kusitisha kabisa kufanya biashara hiyo na kuamua kujikita zaidi kwenye kuifahamu biashara ya Forex ambapo anatarajia kurejea tena kufanya biashara hiyo baada ya miaka minne ya kupata mafunzo.
Usikose kusoma sehemu ya tatu itakayoangazia mambo ya kuepuka unapofanya biashara ya Forex ili kutopoteza pesa zako.
Je wewe umewahi kujihusisha na Forex? Tuandikie maoni kwenye namba yetu ya WhatsApp 0750881888