Hapana! Waziri Ummy Mwalimu hajawahi kuambukizwa corona
- Imebainika pia kuwa akaunti ya Twitter na twiti inayodaiwa kuwa ni waziri Ummy vyote ni famba.
Dar es Salaam. Tangu Mei 8 2020 taarifa mtandaoni zimekuwa zikisambaa kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Tanzania Ummy Mwalimu ameambukizwa corona, jambo ambalo si kweli.
Taarifa hizo zilizosambaa kupitia Twitter, Instagram pamoja na tovuti ya habari ya UCR World News zilianza kuzua mjadala katika jamii ya watumiaji wa majukwaa hayo ya mtandaoni licha ya kuwa famba au uzushi.
Uchunguzi wa Nukta Fakti umebaini kuwa chanzo kikuu cha habari hiyo potofu ilikuwa ni tovuti ya habari inayoitwa UCR World News (www.urtv.com) ambayo ilichapisha taarifa hizo kwa Kiingereza ikiwa na kichwa cha habari “Tanzania’s health minister test positive for coronavirus” (Waziri wa Afya wa Tanzania akutwa na virusi vya corona).
Mwandishi wa habari hiyo alidai kuwa habari hiyo imetokana na twiti ya waziri huyo aliyoiambatanisha na picha ya akaunti aliyodai ni ya Ummy.
Ukweli ni upi?
Licha ya kuwa ugonjwa wa corona unaweza kumpata yeyote, habari hiyo haikuwa ya kweli na ni muendelezo wa habari za uzushi zinazochapishwa mtandaoni juu ya watu maarufu.
“Mimi kupata Corona sio ajabu wala aibu. Hata hivyo, taarifa hii sio ya kweli, ipuuzwe,” aliandika Ummy katika ukurasa wake wa Twitter @umwalimu.
Uchunguzi zaidi wa chanzo cha habari hiyo umebaini kuwa tovuti hiyo ambayo imeanza kuchapisha mara kwa mara ndani ya miezi minne iliyopita ina tabia ya kuchapisha habari za uzushi kwa kuwazushia viongozi wengi mashuhuri duniani.
Historia ya kidijitali inabainisha kuwa tovuti hiyo ilianza kutengenezwa mwaka 2011 lakini hakuwa chapisha habari yeyote ya msingi hadi Machi 2020 ambapo sehemu kubwa ya habari zake zinahusu corona.
Zinazohusiana:
Kunani twiti iliyotumika kutengeneza hiyo habari?
Imebainika pia kuwa akaunti ya Twitter na twiti inayodaiwa kuwa ni waziri Ummy vyote ni famba.
Twiti hiyo indaiwa kuchapishwa Saa 11:34 alfajiri si ya kweli kwa siku hiyo kiongozi hakuwa ametwiti kitu kama hicho. Twiti ya kwanza ya waziri huyo siku huyo ilihusu shukran kwa chama cha mitindo kwa kuchangia vifaa kwa ajili ya mapambano ya COVID-19.
Uamuzi wa mwisho
Habari za kuwa waziri Ummy ana virusi vya corona ni famba na twiti inayodaiwa ni yake imetengenezwa ili kuunda uzushi huo.
Endelea kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya ugonjwa wa virusi vya corona kwa kunawa mara kwa mara na maji tiririka na sabuni, vaa barakoa kila utokapo nje, jizuie safari zisizokuwa na sababu.