Gharama za vifurushi vya intaneti zinavyowanyima wanafunzi haki ya kutumia mtandao
- Baadhi wanashindwa kuzifikia fursa za mtandaoni.
- Gharama hizo zinaweza kuchelewesha au kukatisha ndoto zao.
- Wadau wameshauri kutumia njia mbadala kwa sasa.
Dar es Salaam. “Nilihitaji sana kujiendeleza kimasomo nje ya nchi kwa ufadhili lakini inafika mahala nashindwa hata “kuapply” hivyo vyuo vyenyewe. Gharama za vifurushi nimezinyooshea mkono” amesema Trice Ludayela, mwanafunzi wa mwaka wa tatu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Morogoro.
Kwa mujibu wa binti huyo, inamlazimu kutumia hadi Sh5,000 kwa siku kujiunga kifurushi cha intaneti na kwa kuwa hana ajira yoyote, mbio zake za sakafuni zinaelekea ukingoni.
Ludayela mwenye ndoto ya kusoma shahada ya uzamili katika masuala ya uhifadhi mazingira amesema gharama za vifurushi zinaweza kusababisha ndoto hiyo kuyeyuka hasa kwa kuwa, familia yake haina uwezo wa kumuendeleza.
“Ninatumia kompyuta hivyo inabidi niunganishe intaneti kwa kutumia simu yangu. Kama natumia hadi Sh5000 kwa siku, ni sawa na Sh35,000 kwa wiki na Sh150,000 kwa mwezi. Naitoa wapi mimi na kazi sina?” amesema Ludayela akiweka wazi kuwa siku zingine akiwa hana pesa inabidi akae “offline”.
Changamoto ya Ludayela, huenda inawakumba Watanzania wengi ambao wanatafuta fursa mtandaoni. Inaweza kwenda mbali zaidi na kusababisha watu kupitwa na habari, kukosa mawasiliano kwa kutokuwa mtandaoni muda wote.
Safari bado ndefu
Licha ya mafanikio yaliyopo katika ongezeko la matumizi ya simu nchini, gharama za vifurushi hasa vya intaneti zimebaki kuwa changamoto miongoni mwa baadhi, jambo linalowanyima haki ya kutumia mtandao kwa ajili ya kuwasiliana, kutafuta fursa na hata kujieleza baadhi ya Watanzania.
Takwimu za mawasiliano za robo mwaka za mwezi Juni mwaka 2022 (Quarterly Communications Statistics June, 2022) zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini, (TCRA) zinazeleza, Watanzania waliosajili namba za simu wamefikia milioni 56.2, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.8 ikilinganishwa na Watanzania milioni 55.7 wa mwezi Mei mwaka huu.
Huduma za uhakika na zenye gharam anafuu zinaweza kusaidia wanafunzi na vijana kufaidika na fursa mbalimbali za mtandaoni. Picha| Rodgers George.
“Tunasajili laini nyingi kutafuta unafuu wa bando”
Huenda ongezeko la kusajili laini za simu likawa limechangiwa na gharama za vifurushi kutokana na mtu mmoja kumiliki laini zaidi ya mbili sababu ikiwa ni kutafuta wepesi wa vifurushi.
Akizungumza na Nukta, Mkazi wa Tabata Kinyerezi, Mike Roosevelt amesema yeye alikuwa anamiliki laini tatu kabla ya moja kufungiwa.
Kwa sasa ambapo ana laini mbili, moja ameisajili kutokana na unafuu wa vifurushi vya dakika na meseji huku nyingine ikiwa ni kwa ajili ya intaneti tu.
Roosevelt amepishana na fursa kadha wa kadha anazotumiwa na rafiki zake kwa njia ya WhatsApp kwa sababu ya kutokuwa mtandaoni.
“Nilikuta rafiki yangu amenitumia fursa ya shindano la kubuni nembo, nimekuja kuiona jana na muda wa shindano ulikuwa umeshapita. Nimepishana na uwezekano wa kushinda hadi Sh1 milioni,” amesema Roosevelt.
Soma pia
Suluhu za kuangaziwa
Kutokana na gharama za intaneti, wadau mbalimbali wametoa baadhi ya suluhu ambazo wanafunzi wanaweza kuziangazia kukabiliana na changamoto hiyo.
Mamlaka husika ziingilie kati
Baadhi ya wadau wa mawasiliano wamesema ni muhimu mamlaka zinazohusika moja kwa moja na watoa huduma kuangalia namna ya kutatua changamoto hizo ili kuleta ahueni kwa wananchi.
Mratibu wa maudhui ya dijiti wa taasisi ya LaunchPad, Angella Karashani ameshauri mamlaka husika zizungumze na watoa huduma za intaneti ili kutafuta suluhu kwani watoa huduma wakipunguziwa gharama za kodi, bei za vifurushi vya data zinaweza kupungua.
“Kwa sasa, vifurushi vya ofa vinavyosemekana kuwa kwa ajili ya mwanafunzi ni Sh3,000 ili aweze kupata GB1. Hii sio sawa. Mtandao ni data maana bila data, hakuna mtandao,” amesema Karashani.
Mdau huyo ameshauri pia kuongeza wigo wa kutoa elimu kwa Watanzania juu ya faida za mtandao ili hata gharama zinaposhuka, wengi zaidi wajiunge nao.
Tangazo

Vijana waangazie njia mbadala
Naye Balozi wa vijana kwenye Jumiya ya Afrika Mashariki, Jessica Mshama ameshauri vijana kutumia njia mbadala wakati wakiendelea kuishauri Serikali kushughulikia suala hilo.
“Wakati wakiendelea kuihamasisha Serikali kutafuta suluhu, kuna mambo wanaweza kufanyia baadhi ya kazi zao kwenye migahawa inayotoa huduma za intaneti au kununua huduma za intaneti bila kikomo zinazotolewa na watoa huduma mbalimbali,” ameshauri Mshama.
Ametolea mifano watoa huduma kama Zuku ambao kwa Sh50,000 unaweza kuunganishwa na intaneti bila kikomo kwa mwezi mzima.
“Tuseme mkiwa nyumbani mpo watatu mkachanga mkapata Sh50,000 mkaunganisha intaneti yenu, mnatumia bila wasi wasi,” amesema Mshama.
Latest