Fursa kilimo cha machungwa, soko lafunguka nje ya nchi
- Machungwa yanasindikwa na kusafirishwa hadi Marekani.
- Wakulima watakiwa kulima kwa wingi zao hilo ili kupata soko.
- Asema ujenzi wa viwanda utafungua fursa za ajira kwa vijana na wanafunzi.
Dar es Salaam. Huenda wakulima machungwa Tanzania wakafaidika zaidi kimapato baada ya Serikali kuhimiza ujenzi wa viwanda vitakavyosindika zao hilo linalolimwa zaidi katika mikoa ya Mashariki mwaka Tanzania ukiwemo Tanga.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuchangamkia kilimo cha machungwa ili kujipatia kipato kwa sababu viwanda vya kusindika zao hilo vipo nchini.
Mama Samia ambaye yuko mkoani Tanga katika ziara ya siku tano amesema machungwa ya wakulima hayatapotea kwa sababu wana uhakika wa kupata soko kwenye viwanda kikiwemo cha wilayani Korogwe mkoani humo ambacho kinafanya usindikaji.
“Chungwa la Tanga sasa halipotei isipokuwa kokwa na nadhani hata kokwa watakuja na utaalamu wa kuja na kitu kinachohusu hizo kokwa,” amesema Mama Samia akisema viwanda vya mkoani humo ni ushahidi wa uchumi wa viwanda.
Soma zaidi:
- Apps 10 za kilimo zinazoweza kuwanufaisha wakulima Tanzania
- Fursa lukuki kwa vijana kilimo cha “stroberi” Tanzania
- Teknolojia, suluhu za asili kuokoa kilimo 2020
Amesema kiwanda cha machungwa mkoani humo kimefanikiwa kutumia kikamilifu zao hilo maana sasa kinasindika na kusafirisha machungwa hayo kwenda nje ya nchi ikiwemo Marekani.
“Kwa yale machungwa ambayo wenzetu wa Ulaya na Marekani wanahisi hayakufikia vigezo, yanarudishwa tena, yanamenywa maganda yale yanaanikwa yanapelekwa tena ulaya katika viwanda vya madawa lakini nyama inayotolewa ndani ya maganda yale inakwenda kufanywa juisi,” amesema Mama samia.
Zao hilo la bustani hutumiwa na binadamu kama tunda kuongeza vitamini C mwilini hulimwa katika mikoa ya Pwani, Dar es salaam, Tanga, Mtwara, Lindi, na Morogoro.
Aidha, makamu wa Rais amewasisitiza uongozi wa mkoa huo kuendelea kuvutia wawekezaji ili kuongeza idadi ya viwanda na fursa za ajira hasa kwa vijana.
Mama samia amesema mkoa wa Tanga kwa sasa una viwanda vya kati zaidi ya 300 na viwanda vidogo zaidi ya 500, jambo ambalo ni muhimu katika upatikanaji wa ajira hasa kwa wakazi wa Tanga na wanafunzi waliopo masomoni.
“Viwanda ndiyo mkombozi wa watoto wetu wanaotoka mashuleni. Ajira iko pale, ustawi wa wananchi uko pale lakini kodi za wananchi pia ziko pale,” amesisitiza.
Latest
