Falsafa ya michezo kuboresha elimu, afya ya watoto
Mazoezi kwa watoto hasa waliopo shuleni yanawasaidia kuimarisha mifupa na misuli, kupunguza hatari ya kunyemelewa na magonjwa. Picha | Mtandao.
- Watoto wana mda mwingi wa kufanya mazoezi kwa michezo wanayofanya kuliko watu wazima.
- Michezo inawasaidia kuboresha afya ya akili na kufikiri vizuri wawapo darasani.
- Mazoezi yatakuwa na thamani kwa mtoto kama anapata lishe bora na matunzo ya walezi au wazazi.
Mazoezi ni moja ya sehemu muhimu katika makuzi na uimarishaji wa afya ya binadamu kwa ujumla. Mazoezi hayo yanaweza kuwa ya aina tofauti kulingana na upendelea wa mtu ili kuchangamsha mwili na afya ya akili ambayo inahitajika katika mipango ya uzalishaji na maendeleo.
Katika makundi ya watu, basi watoto wamefuzu katika eneo la kufanya mazoezi kwa sababu wana shughuli nyingi ikiwemo michezo ya shuleni na nyumbani inayowasaidia kuimarisha afya zao zinazohitajika zaidi katika kufanikisha ndoto za elimu.
Mazoezi kwa watoto hasa waliopo shuleni yanawasaidia kuimarisha mifupa na misuli, kupunguza hatari ya kunyemelewa na magonjwa na kuwapa changamko na tabasamu wakati wote wakiwa shuleni na nyumbani.
Mtoto ana ratiba ya mazoezi?
Daktari wa watoto katika hospitali ya Premier Care ya jijini Dar es Salaam, John Cartius anasema mtoto hana ratiba maalum ya kufanya mazoezi kama ilivyo kwa mtu mzima kwamba muda fulani lazima afanye mazoezi, hiyo inamsaidia kufanya kitu chenye afya hata pale asipokuwa na uwezo wa kujua umuhimu wake.
“Mkubwa atajua jioni lazima aende ‘Gym’ kufanya mazoezi, mtoto atacheza muda wowote na muda mwingine bila kujua umuhimu wa kucheza kwake japo ndio mazoezi anayofanya kwa namna ya kujifurahisha mwenyewe.
Dk Cartius anasema mtoto ni kiumbe mwenye muda mrefu wa kufanya mazoezi kuliko mtu mzima kwa sababu ni kitu anachokipenda kufanya katika maisha yake.
Anabainisha kuwa kwa siku moja, watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 13, asilimia 65 ya siku yake huitumia kufanya mazoezi kwani atakuwa kwenye michezo mbalimbali akiwa shuleni au nyumbani ambayo kitaalamu ni sehemu ya mazoezi kwa mtoto.
Zinazohusiana:
- Sababu za wazazi kuwaongoza watoto kusoma vitabu
- Wazazi wafanye nini kudumisha mahusiano na watoto wawapo mbali?
- Youtube yajipanga kuzuia matangazo ya biashara kwenye video za watoto
Kupitia michezo hiyo, wanapata wigo mpana wa kufikiri wanapokuwa masomoni na kuimarisha afya inayowasaidia kutimiza ndoto zao za elimu.
Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa mazoezi siyo njia pekee ya kuboresha afya ya mtoto, bali lishe bora, matunzo na upendo kutoka kwa watu wanaomzunguka.
Latest



