EU, Butiku waongeza shinikizo Serikali kuchunguza matukio ya utekaji, mauaji Tanzania 

September 10, 2024 6:47 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kifo cha kiongozi mwandamizi wa Chadema Ally Kibao.
  • Wakuu wa vyombo vya ulinzi watakiwa kuwajibika kwa matukio hayo.
  • Rais Samia asema Serikali yake haivumilii vitendo vya ukatili.

 Dar es Salaam. Jumuiya za kimataifa na viongozi mashuhuri wamendelea kuishinikiza Serikali kufanya uchunguzi wa kina wa matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea baada ya kifo cha kiongozi mwandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Ally Kibao aliyetekwa na kuuawa na watu wasiojulikana siku tatu zilizopita. 

Kwa mujibu wa Chadema Kibao, aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Taifa na Mshauri wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, alitekwa na watu wawili wenye silaha ndani ya basi la Tashrif eneo la Tegeta akiwa safarini kutokea Dar es Salaam kwenda Tanga Ijumaa iliyopita.

Siku moja baadaye Chadema na Jeshi la Polisi walieleza kuwa mwili wa kiongozi huyo ulikutwa umetupwa eneo la Ununio, Kaskazini Mashariki mwa Dar es Salaam kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala. 

Mauaji ya Kibao ni mwendelezo wa matukio ya utekaji na mauaji yanayoendelea kuripotiwa kwa nyakati tofauti na maeneo mbalimbali nchini huku mamia ya watu wakitaka Serikali kuchunguza kwa kina jambo hilo linalotishia usalama wa raia.   

Katika mkutano wake na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Rais wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, Joseph Butiku, amehoji utendaji wa viongozi wa serikali katika kushughulikia matukio ya utekaji na mauaji huku akishangazwa na viongozi wenye dhamana kutowajibika. 

“Ni kweli tatizo la mauaji, kuteka watu, kunyanyasa watu halikuanza leo wala halikuanza na huyu limeanza wakati wa Magufuli yupo na huko nyuma kabla wakati wa mwalimu lilikuwepo ila hili la kuwajibika naona kama linafifia huwezi kuwa na watu wanakufa wanaenea kila mahali kwenye bahari, kwenye maji halafu wewe ni waziri upo tu,” amehoji Butiku. 

Kiongozi huyo wa zamani wa Serikali amesema haiwezekani nchi ikawa na miaka 62 ya uhuru halafu ikashindwa kujua waharifu ndani ya jamii walioingia kwenye gari na kumchukua Kibao. 

Kwake, viongozi wa vyombo vya usalama, akiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillus Wambura, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa Suleiman Mombo, na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Jacob Mkunda wanapaswa kuwajibika na kutoa majibu kwa wananchi.

“IGP asituambie hajui, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa asituambie hajui CDF ndio mkuu wao wote na mule kuna idara za habari wasituambie wote hawajui ndio maana unaona wanafuatana na Rais wakati wote, sifuatani na Rais mimi wala wewe hufuatani na Rais wako wao wapo karibu yake wamemzingira lazima wajue la sivyo hawana sababu ya kuwepo pale,” amesema Butiku.

Mauaji hayo, yaliyotokea siku mbili zilizopita, yameibua mjadala mzito nchini huku viongozi mbalimbali wakitoa maoni yao kuhusu hali ya usalama baada ya uchunguzi wa  awali wa mwili wa marehemu kubaini alipigwa na kumwagiwa tindikali.

Umoja wa Ulaya (EU)na mabalozi wa Uingereza, Canada, Norway, na Uswisi, kupitia tamko la pamoja leo wameitaka Serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi wa haraka juu ya mauaji na matukio mengine ya utekaji yanayotia hofu wananchi.

“Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kwa makubaliano na Mabalozi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Ubalozi wa Canada, Ubalozi wa Norway, Ubalozi wa Uswisi na Ubalozi wa Uingereza, unasikitishwa na taarifa za hivi karibuni za vitendo vya ukatili, kupotea kwa watu, na vifo vya wanaharakati wa kisiasa na haki za binadamu. 

Tunatoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina kuhusu matukio haya. Tunatoa pole kwa familia zote zilizoathiriwa,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kupitia akaunti yake ya X, ameandika kuwa ameviagiza vyombo vya uchunguzi kuhakikisha wanatoa ripoti sahihi juu ya matukio hayo ingawa tamko lake bado limetiliwa shaka na baadhi ya watu katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Katika chapisho lake hilo Rais Samia alisema Serikali yake haivumilii vitendo vya ukatili kwa kuwa Tanzania ni Nchi ya kidemokrasia na kila raia ana Haki ya kuishi.

Muendelezo wa matukio haya unazua maswali mengi kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali, huku watu mashuhuri na wananchi wa kawaida wakionyesha masikitiko yao na kutilia shaka uwezo wa serikali katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

Miongoni wa watu hao ni pamoja na Fatma Karume aka shangazi, Rostam Azizi, Lady Jaydee, Mnyika John John, Ado Shaibu, Zitto MwamiRuyagwa Kabwe,Godbless E.J Lema, Flaviana Matata, Sauti ya Watanzania na wanasiasa wengine.  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks