Dk. Mpango : AGRF 2023 itumike kuongeza tija ya kilimo barani Afrika
- Asema litumike kujadiliana namna matumizi ya sayansi na teknolojia yatakavyotumika kuchochea uzalishaji wenye tija kwenye kilimo.
- Azirai Serikali kuhamasisha ushiriki wa vijana katika kilimo na kugharamia tafiti.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa Tanzania Dk.Philip Mpango, amewarai viongozi wa Afrika, kuhamasisha matumizi ya teknolojia kwenye kilimo na kugharamia tafiti, ili kuongeza tija na uzalishaji wa chakula barani Afrika utakaosaidia kukabiliana na janga la njaa.
Dk. Mpango aliyekuwa akifungua Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika kwa Mwaka 2023 (AGRF) leo Septemba 5, 2023, amewaambia washiriki watumie jukwaa hilo kujadili namna matumizi ya sayansi na teknolojia katika kilimo yatakavyosaidia kuimarisha mifumo ya chakula katika nchi za Afrika.
“Nadhani Afrika inatakiwa kutumia sayansi na teknolojia iliyopo kuzalisha chakula cha kutosha kwa ajili ya watu wa ndani na soko la Dunia,” amesema Dk.Mpango jijini Dar es Salaam.
Mpango ameongeza kuwa, vijana wanapaswa kuhamasishwa zaidi kushiriki katika shughuli za kilimo ambapo Serikali zina wajibu wa kugharamia tafiti zitakazorahisisha kufanyika kwa kilimo chenye tija.
“Kwa ujumla tunatakiwa kukifanya kilimo kivutie vijana kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa, upatikanaji wa ardhi ya kutosha, upatikanaji wa masoko ya mazao kama mboga mboga ambazo zinalipa kwa haraka,” ameongeza Dk.Mpango.
Soma zaidi
-
Rais Samia asisitiza matumizi ya teknolojia jeshi la polisi Tanzania
-
Kutana na mbunifu wa majiko yanayotumia mawe Tanzania
Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya kilimo katika nchi za Afrika kwa mwaka 2023, iliyozinduliwa leo na Makamu wa Rais Philip Mpango, mifumo ya chakula katika nchi za Afrika inazidi kuharibika hivyo, jitihada za pamoja zinahitajika ili kunusuru nchi za Afrika na janga la njaa.
Siku za hivi karibuni Tanzania imekuwa na mwamko kiasi unaotarajiwa kuchechemua sekta ya kilimo inayochangia asilimia 26 kwenye pato la taifa, huku ikiwa na lengo la kufikisha asilimia 30 ifikapo mwaka 2030.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kuongeza bajeti ya kilimo ambapo kwa mara ya kwanza imefikia zaidi ya Sh900 bilioni huku zaidi ya nusu ya fedha hizo zilielekezwa katika shughuli za maendeleo.
Mathalani mwezi Julai mwaka 2023, Serikali ya Tanzania ilianzisha ushirikiano na nchi ya Korea Kaskazini ili kuimarisha sayansi na teknolojia inayotumika katika kilimo hususani shughuli za utafiti zinazofanywa na Taasisisi yaUtafiti wa Kilimo TARI.
Washiriki wa mkutano wa AGRAF kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya nara la Afrika walipokuwa wakimsikiliza Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.PichalLucy Samson/Nukta
Unyonyaji kwa wakulima kujadiliwa
Aidha, katika mkutano huo unaotarajiwa kufanyika kwa siku nne, vitendo vya kinyonyaji vinavyofanywa kwa wakulima vitatupiwa jicho na kutafutiwa mbinu ya kuvikomesha ikiwemo kuweka sheria zitakazolinda wakulima.
Washiriki wa mkutano huo pia wamekumbushwa kuhusu umuhimu wa ulinzi na usalama unaohitajika na nchi za afrika ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula cha kutosha kwa ajili ya soko la ndani na nje ya Afrika.
Zaidi ya washiriki 3,000 kutoka mataifa 70 ndani na nje ya Afrika wamekusanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano Julius Nyerere (JNCC) jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mkutano mkutano wa AGRF unaolenga kujadili masuala mbalimbali ikiwemo usalama na upatikanaji wa chakula barani Afrika.
Kwa siku tatu zijazo mkutano huo unatarajia kukutanisha mawaziri 38 kutoka nchi 23 watakaojadili utatuzi wa changamoto za mifumo ya chakula na suluhu zitakazotumika kuboresha mifumo hiyo.
Latest



