Dhana, tafsiri Jiji la Dar kufanya kazi saa 24

January 14, 2019 5:04 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Tafsiri hutofautiana kulingana na muda, kazi au aina ya biashara inayofanyika katika eneo husika.
  • Mambo ya kuzingatia ni pamoja maboresho ya miundombinu, usafiri wa umma na huduma za fedha na usalama. 

Dar es Salaam. Kama umewahi kutembelea majiji makubwa ya New York, Paris au Tokyo tayari utakuwa unajua nini maana ya jiji kuishi kwa saa 24. 

Ikiwa na maana kuwa shughuli za uzalishaji, burudani na biashara zinapatikana usiku na mchana. Unaweza ukaenda kwenye maduka makubwa, kumbi za sinema, kufanya miamala na kupata usafiri wakati wote. 

Hiyo ndiyo ndoto ya viongozi wa jiji la Dar es Salaam ambayo imeanza kuwekewa mikakati kuhakikisha jiji hilo la kibiashara linakua hai usiku na mchana ili kuchochea shughuli za maendeleo. 

Katika hatua za awali, Mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda amesema atakutana na wafanyabiashara ili kuangalia namna ya kufunga taa na kamera za usalama katika maduka yote. 

Lakini ni mambo gani muhimu yanayohitajika kuliwezesha jiji kufanya shughuli zake saa 24 bila kumpumzika? 

Ni muhimu kufahamu kuwa tafsiri ya jiji kufanya kazi saa 24 inatofautiana kulingana na shughuli na eneo moja hadi lingine. 

Utafiti wa vitu vinavyounda jiji la saa 24 (Components of 24-hour city) uliochapishwa katika mtandao wa ‘Marked by Teachers’ wa nchini Uingereza unaeleza kuwa mtazamo wa jiji la London kufanya kazi saa 24 ni kupatikana kwa huduma za kijamii na kitamaduni ikiwemo mgahawa, klabu, kumbi za muziki na makumbusho wakati wote.

Pia inaeleza kuwa kwa nchi nyingi za bara la Amerika wanafikiri ni kupatikana kwa huduma hasa za usafiri na uzalishaji zinazosaidia uchumi wa mji husika kukua kwa haraka. 

Utendaji wa shughuli za kiniashara nyakati za usiku unategemea zaidi usalama na huduma muhimu kama za fedha na usafiri wa umma. Picha| Ramada Resort.

Pamoja na tofauti hiyo, yapo mambo ya msingi ya kuzingatia ili kuwezesha jiji kufanya shughuli zake kwa saa 24 kwa wiki:

Uboreshaji wa miundombinu

Mtalaam wa kujitegema wa mipango miji, Raheli Emmanuel anasema suala la kwanza la kushughulikia ni kufuata kanuni za upangaji mitaa na barabara ili kurahisisha usafirishaji wa watu, huduma na bidhaa katika makazi ya watu. 

Sambamba na hilo ni uboreshaji wa miundombinu ya barabara hasa katika maeneo ya viwanda ili kurahisisha usafirishaji wa malighafi na bidhaa hadi sokoni. 

“Kinachotakiwa kufanyika ni regulazation (uboreshaji wa miundombinu) hasa katika mitaa ili kuwahakikishia wafanyabiashara usalama wao wakati wa usiku,” amesema. 

Wakati miundombinu ikiboreshwa, suala la kufunga taa na kamera (CCTV Camera) linapaswa kuwekewa mikakati ili kuwalinda watu dhidi ya vibaka na majambazi ambao wanaweza kutumia mpenyo huo kuwadhuru watu na mali zao. 

Uboreshaji wa miundomnu hasa barabara zinazounganisha maeneo ya viwanda na masoko ni muhimu kukuza biashara jijini Dar es Salaam. Picha| Michuzi.  

Upatikanaji wa usafiri wa umma

Hatua nyingine ni kuhakikisha usafiri  wa umma unapatikana muda wote ili kuwarahisishia wasafiri wasio na magari binafsi nyakati za usiku. 

Kwa jiji la Dar es Salaam ambalo watu wake wanategemea zaidi daladala na mabasi ya mwendo wa haraka (BRT) wamewekewa mikakati ipi kuhakikisha huduma hizo zinapatikana wakati wote? Ikizingatiwa kuwa mbasi hayo hufunga shughuli zake kabla ya saa 6:00 usiku. 

Hata kama yatatoa huduma hiyo, idadi ya watu wanaofanya biashara wakati usiku itakuwa toshelevu?


Zinazohusiana: Makonda aagiza taa, kamera za usalama zifungwe kwenye maduka Dar


Huduma za fedha

Mtaalamu wa programu za kompyuta kutoka taasisi ya Code for Africa (CFA), Clemence Kyara anasema huduma na biashara zinategemea mzunguko wa fedha hasa nyakati za usiku ikiwemo miamala inayofanyika kwa njia ya benki na  simu za mkononi. 

Anabainisha kuwa kama huduma hizo zitaimarishwa zitachochea watu kufanya shughuli zao wakati wa usiku na kuongeza wigo wa upatikanaji wa mapato kwa wafanyabiashara na Serikali. 

Pamoja na uwepo wa huduma hizo, anaamini usalama ni jambo muhimu lakini nani atahakikisha shughuli za kibiashara haziathiriwi na hatari yeyote ya uhalifu? 

Upatikanaji wa huduma za kibenki na fedha jumuishi utasaidia kuchochea shughuli za biashara nyakati za usiku. Picha| indaressalaam

Mabadiliko ya sheria na kanuni

Wakati mipango ya kulihuisha jiji la Dar es Salaam zikiendelea, mabadiliko ya sheria ni muhimu ili kukidhi mahitaji ya watu kutembea huru na kufanya shughuli zao wakati wote. 

Shughuli nyingi za kuuza vinywaji, kumbi za starehe na burudani hufungwa kabla ya saa 6:00 usiku. 

Vibali na leseni zikibadilishwa ili kuruhusu huduma wakati wote haitaathiri maisha ya kawaida watu? Tuna nguvu kazi ya kutosha kusimamia kanuni hizo zisivunjwe? 

Tathmini ya kina inahitajika ili kufahamu kama shughuli za kibiashara jijini hapa zikiruhusiwa kufanyika saa 24 zitaongeza gharama ya uzalishaji au kuleta faida kwa pande zote zitakohusika?

Pamoja na hayo baadhi ya wanazuoni wanasema nadharia ya jiji kufanya kazi saa 24 haipo lakini ni mfumo tu wa watu wa jamii fulani kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika, jambo linaweza kuwa na matokeo hasi katika ukuaji wa uchumi hasa kama nguvu kazi sio kubwa.

 

Enable Notifications OK No thanks