Corona yatangazwa janga la dunia, mwongozo kuwalinda watoto watolewa
Ikiwa watoto wanapaswa kufundishwa njia sahihi za kujikinga na virusi vya Corona ili kuwawezesha kuendelea na masomo. Picha|Mtandao.
- Mwongozo huo unatoa masuala muhimu na vigezo vya kuzingatia ili maeneo ya shule yawe salama.
- Pia unatoa ushauri kwa mamlaka za kitaifa kuhusu jinsi ya kutekeleza mipango ya dharura kwa ajili ya maeneo ya shule.
Dar es Salaam. Wakati ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) ukitangazwa kuwa ni janga la dunia kwa kuwa umesambaa duniani kote, mashirika ya Umoja wa Mataifa yametangaza mwongozo mpya wa kusaidia kulinda watoto na shule dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo.
Mashirika hayo ni lile la afya duniani (WHO) na Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Shirikisho la Msalaba na Hilal Nyekundu duniani (IFRC) wamesema hayo kupitia taarifa yao iliyotolewa Jumanne katika miji ya Geneva, Uswisi na New York, Marekani.
“Mwongozo huo unatoa masuala muhimu na vigezo vya kuzingatia ili maeneo ya shule yawe salama. Pia unatoa ushauri kwa mamlaka za kitaifa na manispaa kuhusu jinsi ya kutekeleza mipango ya dharura kwa ajili ya maeneo ya shule,” imeeleza taarifa hiyo.
Mashirika hayo yamesema ingawa mwongozo huo ni kwa nchi ambazo zimeshathibitisha kuwa na wagonjwa wa COVID-19, bado ni muhimu katika mazingira mengine.
Yamesema miongozo ya shule salama iliyotumika huko Guinea, Liberia na Sierra Leone wakati wa mlipuko wa Ebola mwaka 2014 hadi 2016, ilisaidia kuzuia maambukizi ya virusi hivyo shuleni.
Soma zaidi:
- Ugonjwa wa Corona unavyopukutisha mifuko ya wanunuzi Kariakoo
- Serikali yamuhoji Nabii aliyedai kugundua dawa ya kutibu virusi vya Corona
Mambo mengine ya kuzingatia, mashirika yametaka afya ya mtoto ifuatiliwe na iwapo anaugua abakie nyumbani, kuhamasisha watoto kuuliza maswali na kuelezea shaka na shuku zao, kukohoa na kupiga chafya kufanyikie kwenye kitambaa au kwenye kona ya kiwiko na kuepusha kugusa uso, macho, mdomo na pua.
“Watoto wapatiwe taarifa ya jinsi ya kujilinda, wafundshwe jinsi ya kunawa mikono vizuri sambamba na kupatiwa vifaa vya kujisafisha. Kuwepo pia na mfumo mzuri wa kupitisha hewa,” unaeleza mwongozo huo.
Mashirika hayo yameongeza kuwa “majengo ya shule yawe yanafanyiwa usafi kwa kutumia dawa za kuua vijidudu.”
Kwa mujibu wa WHO, mpaka jana (Machi 13, 2020) watu 125, 048 walikuwa wameambukizwa ugonjwa wa virusi vya Corona ulimwenguni na vifo vilivyoripotiwa ni 4,613 huku China na Italia zikiathirika zaidi.
Mpaka sasa hakuna Mtanzania yoyote aliyeripotiwa kuambukizwa virusi hivyo, licha ya kuwa wananchi wanakumbushwa kuchukua hatua muhimu kujikinga.