Choroko, dengu, mbaazi, soya, ufuta sasa kuuzwa kidijitali 

January 8, 2025 12:18 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Msimu rasmi wa mauzo ya kila zao utatangazwa na Copra.
  • Mauzo ya choroko yatakuwa ya kwanza, yakipangwa rasmi kuanza Januari, na kufuatiwa na ufuta utakaoanza kuuzwa Aprili.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Copra) imesema kuanzia Januari 2025, baadhi ya mazao jamii ya mikunde ikiwemo choroko, mbaazi, soya, ufuta pamoja na dengu yataanza kuuzwa kwa minada ya kidijitali.

Mfumo huo mpya wa biashara ya mazao, unasimamiwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), hatua inayolenga kuboresha uwazi, ufanisi, na thamani ya mazao ya wakulima kote nchini.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Copra Irene Mlola Januari 6 mwaka huu imebainisha kuwa mwanzo rasmi wa msimu wa mauzo katika mazao yaliyotajwa utatangazwa na mamlaka hiyo ambapo wafanyabiashara na wadau wa mazao hayo watapaswa kufuata miongozo ya mazao jamii ya mikunde.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo mauzo ya choroko yatakuwa ya kwanza, yakipangwa rasmi kuanza Januari, na kufuatiwa na ufuta utakaoanza kuuzwa Aprili, kisha kufuatiwa na mauzo ya soya ndani ya Mei, na kukamilisha msimu wa ununuzi kwa mauzo ya dengu na mbaazi yatakayofanyika Juni.

Hatua muhimu za kujiandaa na mnada

Kwa mujibu wa Mwongozo wa Biashara ya zao la Dengu, Mbaazi, Soya na Ufuta Toleo la 3-2024, uliotolewa na Copra, TMX, Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo.

Mazao yote yanayohusika yatapokelewa katika maghala yaliyosajiliwa na kusimamiwa na vyama vya msingi vya ushirika ambapo wakulima wanatakiwa kuzingatia kuwa mazao yao lazima yawe safi, yamekauka, na yasiwe na uchafu au mbegu za mazao mengine.

Mazao yatakayo pokelewa yatapangwa katika madaraja yanayotambulika kwa mujibu wa mwongozo wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na yatafungashwa katika mifuko yenye uzito wa kilogramu 50, inayokidhi viwango vya kimataifa (ISO 23560:2015).

Mwongozo huo umeeleza kuwa mfumo wa stakabadhi za ghala unahakikisha kuwa mazao yanapokelewa, kuhifadhiwa, na kusimamiwa kwa uwazi, ambapo wakuu wa maghala watatoa stakabadhi rasmi kwa mazao yote yatakayopokelewa, ambayo itatumika kama hati ya kuthibitisha mali ya mkulima.

Minada ya kidijitali kupitia TMX

Mazao yaliyohifadhiwa ghalani yatauzwa kupitia minada ya kidijitali inayosimamiwa na TMX, mchakato wa mnada utahusisha hatua za wanunuzi kujisajili kwa njia ya kielektroniki na kuweka kinga ya dhamana ya malipo kwenye akaunti ya Copra.

Baada ya hapo, bei za mazao zitatangazwa wakati wa mnada, ambapo wanunuzi wataweza kushindana kununua kwa bei ya juu zaidi.

Baada ya mnada, bei ya juu zaidi itakayofikiwa itatangazwa kwa wakulima kupitia vyama vyao vya msingi, na ridhaa yao itahitajika kabla ya kukamilisha mauzo.

Mnunuzi atakayeshinda mnada atalipa ndani ya siku mbili baada ya kupokea hati ya madai, na malipo yote yatafanywa kupitia vyama vya msingi vya ushirika, ambavyo vitahakikisha kuwa wakulima wanalipwa kwa wakati.

Faida za mfumo huu kwa wakulima na wadau

Kwa mujibu wa mwongozo wa Biashara Zao la Dengu, Mbaazi, Soya na Ufuta Toleo la 3-2024, mfumo huu wa kidijitali umebuniwa kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo nchini. 

Baadhi ya faida zinazotarajiwa ni pamoja na wakulima kuweza kuuza mazao yao kwa bei nzuri sokoni kutokana na ushindani wa wanunuzi.

Unahakikisha kuwa biashara ya mazao inafanyika kwa njia iliyo wazi na inayoweza kufuatiliwa. Mazao kuhifadhiwa kwenye maghala salama kuepuka upotevu au kuharibika.

Mfumo wa stakabadhi za ghala unaruhusu wakulima kutumia stakabadhi kama dhamana ya kupata mikopo ya kuendeleza kilimo chao.

Mfumo wa kidijitali wa biashara ya mazao ni hatua kubwa kuelekea mapinduzi ya sekta ya kilimo nchini Tanzania. Mfumo huu siyo tu utawanufaisha wakulima, bali pia utaimarisha uchumi wa taifa kupitia biashara iliyo wazi na yenye tija.

Hata hivyo, elimu inahitajika zaidi kwa jamii za wakulima na wafanyabiashara kuhusu namna wanavyoweza kunufaika na mifumo hiyo mipya ili kuepukana na changamoto ya migomo baridi kwa wakulima au utoroshaji wa mazao kwa wafanyabiashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks