China yaipatia Tanzania msaada wa Sh35.4 bilioni
- Fedha hizo huenda zikatumika kupanua ujenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
- Pia kupandisha hadhi Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuwa chuo kikuu.
- Serikali yaahidi kutumia vizuri fedha hizo kwa maendeleo ya Taifa.
Dar es Salaam. Serikali ya China imeipatia Tanzania msaada wa Yuan za China milioni 100 sawa na Sh35.4 bilioni utakaotumika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni moja ya hatua inayolifanya taifa hilo la Asia kuendeleza mizizi ya urafiki na Tanzania.
China, ambayo ni moja ya mataifa makubwa ulimwenguni kwa nguvu ya kiuchumi, ni rafiki wa Tanzania kwa zaidi ya miaka 50 sasa.
Mkataba wa makubaliano ya msaada huo umesainiwa Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa China nchini Tanzania, Wan Ke, kwa niaba ya Serikali ya China.
Fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi itakayokubaliwa na pande zote mbili.
Tutuba alipendekeza msaada huo utumike kupanua ujenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kupandisha hadhi Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuwa chuo kikuu, kutekeleza mradi wa uhifadhi wa Miamba katika eneo la Ngorongoro (Geopark) na miradi mingine itakayoafikiwa na Serikali zote mbili.
“Nachukua fursa hii kukuhakikishia kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itachukua hatua zote muhimu kuhakikisha kwamba miradi itakayotekelezwa kwa fedha za msaada huu inakamilika kwa wakati ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” amesema Tutuba.
Ameishukuru China kwa misaada na mikopo yenye masharti nafuu inayoipatia Tanzania kuanzia mwaka 2010 na kutumika kujenga miundombinu ya reli, elimu, afya, tehama, nishati, maji, sekta ya viwanda, kilimo, usalama, na misaada ya kitaalam, iliyofikia Dola za Marekani bilioni 1.8 sawa na Sh4.2 trilioni.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Emmanuel Tutuba (kulia) na Balozi wa China, Wan Ke (kushoto), wakisaini Mkataba wa msaada wa kiasi cha Sh35.4 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, Jijini Dar es Salaam. Picha| Wizara ya Fedha.
Balozi wa China hapa nchini, Wan Ke, amesema kuwa msaada huo ni matokeo ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi aliyoifanya mwezi Januari mwaka huu na ni mwendelezo wa ushirikiano mwema kati ya China na Tanzania uliodumu kwa zaidi ya miaka 57 sasa.
“Tangu wakati huo China imeisaidia Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ikiwemo ujenzi wa reli ya TAZARA, Uwanja wa Michezo wa Benjamin Mkapa, Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNCC), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, na Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” amesema Balozi Ke.
Zinazohusiana:
-
Tanzania yapata heshima ya kushiriki maonyesho ya biashara China
- Serikali yajipanga kuongeza mapato ya utalii kutoka China
Aidha, Ke, amesema kuwa China imeipatia Tanzania msaada wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.3 (Sh3.1 bilioni) kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid 19 zilizotumika kununulia barakoa, vitakasa mikono, vifaa tiba na dawa na kwamba nchi yake imetia saini kushiriki kwenye mpango wa kuahirisha ulipaji wa madeni (DSSI) ili kuruhusu Serikali kuelekeza fedha hizo kwenye maeneo mengine katika kupambana na maradhi hayo yanayoendelea kuitikisa dunia.
Balozi huyo amesema kuwa ana imani na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameahidi kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini pamoja na kulinda uwekezaji.
Amesema matumaini hayo ya Rais yamewaongezea kujiamini zaidi na uamuzi huo unaungwa mkono na kampuni za China zilizowekeza hapa nchini na utawavuta wawekezaji wengi zaidi kutoka China kuja kuwekeza mitaji na teknolojia hapa nchini.
Latest
