Changamoto zinapokuletea fursa

March 19, 2022 10:21 am · Herimina
Share
Tweet
Copy Link

KUSIKILIZA SIMULIZI YA FILAMU YA  FINE WINE BONYEZA HAPA

                                               


Ni filamu ya Fine Wine, inayomuhusu mwanadada Kaima anayepitia changamoto katika mahusiano.

  • Changamoto hizo zinamkutanisha na moja ya matajiri zaidi Afrika.

Dar es Salaam. Filamu ya “Fine Wine”, inamhusu mwanadada Kaima wa Nigeria. Kwa lugha ya vijana wa Tanzania ya kumuelezea ni “pisi kali”.

Licha ya uzuri na ‘usmati’ alionao binti huyu, mahusiano yake na kijana Tunji ni pasua kichwa kuliko hata majukumu yake ya kazi.

Tunji amekuwa ni mtu wa kutoa sababu muda wote pale ambapo wamekubaliana kukutana na Kaima ili kuwa na muda wa pamoja. 

Leo utasikia shangazi kaniagiza, kesho atasema kuna rafiki yangu amerudi kutoka Uingereza inabidi tumfanyie ‘party’, kesho kutwa kisingizio ni kuna nyaraka inabidi nizifuate mahali. Kwa kweli mimi nisingeweza maana hata kama mapenzi ni uvumilivu, hii ilizidi.

Kinachomuuma zaidi binti huyu, ni kuwa Tunji amekuwa akimdharau mbele za watu bila kujali atajisikiaje.

Maisha ya Kaima yanabadilika siku ambayo wanakubaliana kukutana na Tunji katika mgahawa fulani, lakini kaka huyo anamwambia mpenziwe kuwa amsubiri kwani kuna jambo la ghafla limetokea.

Nusu saa inakata, saa moja, la pili, saa tatu! Wapi Tunji? Kaima wa watu ana kazi ya kuangalia kushoto na kulia utadhani polisi anakagua magari.

Samahani ya Kaima kwa Mr George inajenga ukaribu kati yao, na taratibu ukurasa mpya wa huba kwa wawili hawa unafunguka. Picha| Leisurebyte.

Bwana bwana, mara kaja baba mmoja ambaye anakosea akifikiri kuwa Kaima ni mwandishi wa habari aliyeweka appointment ya kukutana nae hapo.

Huyu bwana ni kusema aliparamia moto wa kifuu kwani hasira zote za Kaima kwa Tunji zikamuishia yeye.

Kaima alimshushia ya kumshushia mzee wa watu bila ya kujua kuwa baba huyo ni Mr George. Mtu mwenye pesa zake atii! George yupo kwenye orodha wa watu 100 matajiri zaidi Afrika. Orodha iliyotolewa na jarida la Forbes.

Kama haitoshi, George ni bosi wa mradi unaofanywa na benki ambayo Kaima na mpenziwe Tunji wanafanya kazi.

Ukisikia kimeumana ndo hapa. Pale Tunji anapofika, moja kwa moja anapeleka makaratasi kwa George.

Macho nje, kidevu chini,  Kaima akihamaki kuwa alichokifanya huenda kikaharibu vibarua vyao. Anapomwambia mpenzi wake yaliyojiri kabla hajaja, Tunji anamwambia akaombe radhi na hapo, ukurasa mpya unafunguka.



Mwanzo wa huba

Samahani ya Kaima ni kama petroli kwenye gari ya huba mpya kati yake na Mr George. Ukaribu wao ni zaidi ya kuvaa sare na kununua viatu vinavyofanana kwani wawili hawa wanaanza kusaidiana changamoto mbalimbali. 

George anamsaidia Kaima kupata mkataba wa kudumu kwenye benki, na pale George anapokuwa kwenye maradhi, Kaima ndiye mtu aliyechukua jukumu la kumuuguza. ‘What a love’.

Unaweza kujiuliza, kwani Mr George hana familia ya kumuuguza? 

Jibu ni kuwa, baba huyu aliachana na mkewe miaka kadhaa iliyopita. Ana watoto wawili ambao wanalingana kwa iumri na Kaima lakini ni watu wenye heka heka zinazowafanya kutokuwa karibu na baba yao.

George alianza kumpenda Kaima tangu awashiwe moto mgahawani. Kaima yeye upendo anaoonyweshwa na baba huyo unamvuta taratibu kama samaki avutwavyo na mnyoo wa kwenye ndoano.

Hayawi hayawi sasa yamekuwa. Relax, ndoa bado, ninachojaribu kusema ni kuwa, huba tayari ipo na wawili hao washaridhiana.

Kinachobaki ni ridhaa ya jamii sasa. binti  mwenye miaka 25 na baba wa miaka 55, ‘does it come come?’

                     

Jamii ya kiafrika huwachukulia mabinti wenye mahusiano na watu waliowazidi umri sana kama ‘wadangaji’ bila ya kujua ni milima gani wanaipanda na hao vijana waliopo.

Kwa upande wa Tunji, ukaribu wa George na Kaima unamshtua. Ili asipokonywe tonge mdomoni anaamua ‘kupropose’, tena katika siku ya birthday ya Kaima.

Binti unayenisikiliza hapa, kama ungekuwa Kaima ungefanyaje? Ungeenda kwa Tunji ambako kuna stress au kwa Mr George na uiache jamii ipambane na hali yake?

Kufahamu  maamuzi anayochukua Kaima, kaitazame filamu ya “Fine Wine” kujua kinaga ubaga.

Filamu hii utaipata Netflix na itakufunza jambo kubwa sana. Siwezi kusema litakubadilisha mtazamo wako, lakini pengine litakupa mwanga kama mtazamo wako ni sahihi au la.

Enable Notifications OK No thanks