Chadema, CCM vyaahidi kukuza uchumi wa kidijitali Tanzania

October 24, 2020 8:04 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • CCM inalenga kuimarisha mifumo ya kidijitali ili kurahisisha utendaji wa Serikali kujenga uchumi.
  • Chadema inakusudia kushirikiana na sekta binafsi kutengeneza mifumo itakayorahisisha malipo na biashara ya mtandaoni.
  • ACT-Wazalendo haijazungumzia uchumi wa kidijitali katika ilani yake. 

Dar es Salaam. Tangu dirisha la kampeni za Uchaguzi Mkuu lifunguliwe Agosti 26 mwaka huu kila chama cha siasa kimekuwa kikitafuta fursa ya kujiuza kwa wananchi ili kiweze kuchaguliwa. 

Wagombea wa vyama hivyo vya siasa wanaendelea kunadi sera zao kwa wananchi ili kupata nafasi za urais, ubunge na udiwani katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Katika kipindi hiki hiki cha mapinduzi ya nne ya viwanda yanayoendeshwa zaidi na teknolojia ya dijitali, hapana shaka Watanzania wengi hususan vijana na wajasiriamali wanasubiria kuona vyama na wagombea wao wanavyoainisha namna watavyochochea uchumi wa kidijitali ili kuongeza ajira na kuchagiza maendeleo. 

Kwa kawaida ilani za uchaguzi hubeba mambo mengi ambayo chama husika kitayafanya na ili kubaini kama uchumi wa kidijitali (digital economy) umeanishwa na vyama vya siasa Tanzania kutoa mwelekeo wa mambo watakayoyafanya katika kukuza jambo hilo. 

Hadi sasa kuna ilani tatu ambazo ni gumzo nchini za vyama vya CCM, Chadema na ACT-Wazalendo. Baadhi ya vyama ilani zake imekuwa ni ngumu kupatikana.

Uchumi wa kidijitali ni nini?  

Ni mfumo wa kibiashara unaohusisha matumizi mapana ya teknolojia ya simu na kompyuta katika uuzaji na ununuzi wa bidhaa, ubunifu na ugunduzi wa mbinu za mtandaoni zinazorahisisha utendaji wa shughuli mbalimbali ili kukuza uchumi wa nchi. 

Mifumo hiyo ni pamoja na biashara ya mtandaoni (E-commerce), programu za simu za manunuzi na malipo ya bidhaa. 

CCM katika ilani yake imeeleza kuwa inatambua kuwa uchumi wa kidigitali ni muhimu katika kuleta maendeleo kwa kuongeza ufanisi katika uzalishaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali na kutoa fursa za kuongeza vipato vya wananchi na Taifa kwa ujumla. Picha| Mwana Halisi.

Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wa ilani tatu za vyama vya CCM (Chama Cha Mapinduzi), Chadema (Chama Cha Demokrasia na Maendeleo) na ACT-Wazalendo (Alliance for Change and Transparency) za mwaka 2020-2025 kuhusu uchumi huo na namna zitakavyoujenga ili ulete manufaa kwa wananchi wa Tanzania. 

CCM katika ilani yake kimeeleza kuwa kinatambua kuwa uchumi wa kidigitali ni muhimu katika kuleta maendeleo kwa kuongeza ufanisi katika uzalishaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali na kutoa fursa za kuongeza vipato vya wananchi na Taifa kwa ujumla. 

“CCM itaendelea kusimamia Serikali kuhakikisha kuwa teknolojia mpya za kidijitali zinatumika kuongeza ufanisi katika sekta za uzalishaji na kuepuka madhara yanayoweza kutokea,” inasomeka sehemu ya ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025. 

Ili kufanikisha uchumi huo, chama hicho tawala kimeeleza kuwa kinakusudia kudhibiti athari hasi zinazoweza kutokea kutokana  na matumizi ya  teknolojia  mpya za  kidijitali na kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali za Serikali kwa umma kwa kuanzisha vituo vya Huduma Pamoja (One Stop Centre) ili kuongeza ufanisi na kurahisisha  upatikanaji  wa  huduma  za Serikali.

“Kuimarisha kituo cha utafiti, ubunifu na uendelezaji wa Tehama ikiwemo kujenga uwezo na kuongeza matumizi ya teknolojia mpya za kidijitali na artificial intelligence (akili bandia),” inaeleza ilani hiyo. 

Sambamba na hilo,  CCM imeahidi kuwa Serikali itakayochaguliwa itaendeleza mitandao  inayozingatia  usalama  wa mifumo na taarifa za Serikali na kuwarahisishia watumishi wa umma utendaji kazi na  wananchi  kupata  huduma  kwa urahisi  na  ufanisi.

Wakati CCM wakieleza hayo, chama kikuu cha upinzani Tanzania Chadema kinaamini kuwa uchumi wa kidijitali ni kutengeneza mifumo ya biashara mtandaoni inayoshirikisha sekta binafsi kwa kutumia teknolojia ya simu na kompyuta  katika uuzaji na ununuzi wa bidhaa.

“Kutokana na kasi kubwa ya ukuaji na mabadiliko makubwa ya kiteknolojia yanayoendelea ulimwenguni kwa sasa, ni lazima Tanzania ianze kujipanga ili iweze kunufaika na ukuaji huo kwa kuweka mikakati thabiti na endelevu ya kuwa na uchumi wa kidijitali,” inaeleza sehemu ya ilani ya Chadema kwa mwaka 2020-2025. 


Zinazohusiana 


Serikali ya Chadema itakayoongozwa na mgombea wake wa urais Tundu Lissu iwapo itachaguliwa, itashirikiana na sekta binafsi, itaratibu upatikanaji wa miundombinu ya kisasa ya mitandao ya kompyuta na simu ya 4G na 5G ili kufanikisha azma ya kushiriki katika uwanda wa uchumi wa kidigitali. 

“Kwa kushirikiana na sekta binafsi, serikali ya Chadema itawezesha upatikanaji wa taarifa za mitaji, masoko, na uwekezaji kupitia jukwaa la biashara mtandaoni ili kuwawezesha wakulima, wafugaji, wavuvi na wafanya biashara wadogo kwa wakubwa kuuza na kununua bidhaa zao ndani na nje ya nchi kwa kuanzisha mifumo ya kidigitali (Application- app) za umma na za binafsi,” inasomeka sehemu ya ilani ya chama hicho. 

Kwa kushirikiana na sekta binafsi, ilani hiyo inaeleza kuwa serikali ya Chadema itaanzisha mfumo wa malipo kwa kila huduma inayotolewa na sekta zitoazo huduma hapa nchini kupitia mfumo wa malipo mtandaoni (online payment) utakao kuwa ukitumia kadi janja (smart card) au programu maalum.

Kwa kushirikiana na sekta binafsi,  Chadema imeahidi kuwa italinda haki zote za wabunifu na wazalishaji mali kupitia mtandao wa simu au kompyuta ili kukuza uzalendo na kuliongezea pato Taifa. 

Pia itaanzisha mafunzo rasmi ili kuwajengea Watanzania uwezo wa kufanya biashara kupitia mitandao ya simu na kompyuta ambapo mafunzo hayo yatalenga utoaji huduma, uuzaji wa bidhaa na ununuzi wa bidhaa kupitia mifumo ya wavuti za intaneti na simu janja.

“Kwa kushirikiana na sekta binafsi, serikali ya Chadema itapeleka muswada rasmi wa uchumi wa kidigitali ili kutunga sheria, kanuni na taratibu za kuratibu uchumi wa kidigitali,” inaeleza ilani hiyo. 

Chadema imeahidi kuwa italinda haki zote za wabunifu na wazalishaji mali kupitia mtandao wa simu au kompyuta ili kukuza uzalendo na kuliongezea pato Taifa. Picha| Mwana Halisi.

Uchumi kwa ujumla

Hata hivyo, ilani ya ACT-Wazalendo haijazungumzia lolote kuhusu uchumi wa kidijitali, licha ya kuwa imeainisha mambo yatakayofanywa na Serikali ya chama hicho kukuza uchumi wa nchi ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwapa watu uhuru wa kununua na kuuza bidhaa halali. 

Kwa upande wa Chama Cha Wananchi (CUF) kimesema kitahakikisha kuwa shughuli za biashara na uwekezaji zinakua nyepesi zaidi kuliko hivi sasa ili kujenga uchumi utakaoweza kuzalisha ajira kwa vijana. 

“Chama Cha Wananchi (CUF) ambayo misingi yake ni haki sawa kwa wananchi wote, kimejikita kuweza kujenga uchumi unaokuwa kwa kasi na unaoongeza ajira,” alisema Mwenyekiti na mgombea wa urais wa chama hicho, Prof Ibrahim Lipumba wakati akichukua fomu ya urais katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Agosti 10, 2020.  

Prof Lipumba alisema ilani ya chama chake imeeleza bayana kuwa hawahitaji sera za kukurupuka, kila kitu kiwe kimepimwa na kuweza kutazama athari zake zilizo bora katika uchumi wa nchi.

Hata hivyo, mgombea huyo wa urais kwa mara ya tano sasa tangu uchaguzi wa vyama vingi uanze mwaka 1995, hakuelezea kiundani namna watakavyotumia dijitali kukuza uchumi.  

Wakati CUF wakijipanga kuongeza kasi ya uchumi, chama cha NCCR-Mageuzi (The National Convention for Construction and Reform – Mageuzi) kimesema kinataka kufanya mageuzi ambayo yataufanya uchumi wa kati ambao Tanzania imeingia kuleta maana kwa wananchi katika misingi ya haki na uhuru. 

Sisi NCCR-Mageuzi, ‘we  want to transform Tanzania into real development’ (Tunataka kufanya mageuzi ya kweli ya maendeleo Tanzania), siyo hadithi kwamba uchumi wa kati, hapana! Tunataka kuuona huo uchumi wa kati, haki za kijamii, haki za kisiasa na haki za kiuchumi zikitendeka,” alisema mgombea wa urais kupitia chama hicho, Yeremia Maganja wakati akichukua fomu ya urais Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC)  jijini Dodoma Agosti 10, 2020. 

Umevutiwa na mikakati gani ya kukuza uchumi wa kidijtali? Kazi kwako kupiga kura na kuchagua mgombea wa chama atakayetekeleza ilani uliyovutiwa nayo. 

Ilani ya ACT-Wazalendo haijazungumzia lolote kuhusu uchumi wa kidijitali, licha ya kuwa imeainisha mambo yatakayofanywa na Serikali ya chama hicho kukuza uchumi wa nchi ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwapa watu uhuru wa kununua na kuuza bidhaa halali. Picha| DW.

Enable Notifications OK No thanks