Bunge lapendekeza maboresho ya sheria kukabiliana na mapenzi ya jinsia moja

April 14, 2023 5:50 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na jambo hilo kujadiliwa bungeni kwa siku nne mfululizo.
  • Utafiti kufanyika kubaini mapungufu kwenye Sheria ya Makosa ya Kujamiiana.
  • Bunge litaidhinisha mabadiliko hayo yanayokusudia kuilinda jamii dhidi ya vitendo hivyo.

Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limeishauri Serikali kufanya utafiti na kuainisha mapungufu yaliyopo katika Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998  na kuwasilisha muswada wa marekebisho hayo bungeni ili yaidhinishwe kwa minajili ya kukabiliana na wimbi la mapenzi ya jinsia moja.

Spika wa Bunge la Tanzania Dk Tulia Ackson aliyekuwa akijibu ombi la Mbunge wa Arumeru Mashariki Noah Lembris la kuomba mwongozo juu ya kauli  rasmi ya Bunge kuhusu suala la mapenzi ya jinsia moja, amebainisha kuwa Bunge litaidhinisha mabadiliko yatakayofanyika baada ya utafiti na kubaini mapungufu ya sheria iliyopo.

“Hapa bungeni kumekuwepo na mjadala mrefu kwa zaidi ya siku tatu kuhusiana na mapenzi ya jinsia moja, na taasisi mbalimbali zimeshasema kauli zao ikiwemo za dini, Rais na makamu wa Rais, hata mahakama.

“Naomba mwongozo wako, huoni ni wakati muafaka Bunge lako kuielekeza Serikali kulivalia njuga suala hili, na kuja na muswada mahususi kutokana na mapungufu ya sheria yetu ya makosa ya kujamiiana, ili itungwe sheria mahususi kama Uganda ili kuhakikisha nchi yetu inasalimika,”  amesema Mbunge Lembris huku akipigiwa makofi.

Pamoja na kukiri uwepo wa mjadala juu ya  jambo hilo bungeni hapo, Spika Tulia amezishauri Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Ndani, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kufanya utafiti kupitia tume ya kurekebisha sheria ili kuondoa mapungufu yaliyopo sasa. 

“Yapo mapungufu ya dhahiri ambayo yameelezwa na wabunge, yale mapungufu yazibwe mianya, kashirikianeni na tume hii, hatutaki kutunga sheria kwa mihemko, tutunge sheria tukiwa tunaelewa tatizo ni kubwa kiasi gani..,” amesema Tulia.

Spika Tulia ameongeza kuwa utafiti huo utaisaidia Serikali kufanya marekebisho mahususi kisha kuwasilisha muswada bungeni ambapo Bunge litaidhinisha maboresho hayo ili kuwalinda wananchi pamoja na watoto.


Soma zaidi


Licha ya kuwahi kujadiliwa mara kadhaa siku za nyuma suala la mapenzi ya jinsia moja limejadiliwa kwa kina katika michango ya wabunge mara baada ya Waziri Mkuu kuwasilisha mapendekezo ya bajeti ya ofisi yake na taasisi zilizo chini yake Aprili 5 2023.

Miongoni mwa maboresho yanayotajwa na wabunge ni kuongeza ukali wa adhabu kwa watu watakaobainika kujihusisha na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na kutambua vitendo vya usagaji kama kosa la jinai.

Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kifungu cha 154 kimebainisha adhabu ya Makosa ya kinyume cha maumbile  Sheria Na. 47 ya 1954 kifungu cha tatu na  Sheria ya Makosa ya Kujamiiana  ya 1998 kifungu cha 16 kuwa ni kifungo cha miaka 30 jela au kifungo cha maisha.

“Mtu yeyote ambaye anamuingilia mtu yeyote kinyume cha maumbile au, anamuingilia mnyama kimwili au anamruhusu mwanaume kumuingilia yeye mwanaume au mwanamke kinyume cha maumbile, atakuwa ametenda kosa, na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha na wakati mwingine kifungo kisichopungua miaka thelathini.

Ikiwa kosa limetendwa chini ya kifungu kidogo cha (1) cha kifungu hiki dhidi ya mtoto wa chini ya miaka 10, mkosaji atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha,” inasomeka sehemu ya sheria hiyo.

Spika wa Bunge la Tanzania Tulia Ackson akiongoza kikao cha sita cha Mkutano wa 11 wa Bunge la 12.PichalBunge

Ripoti ya Haki za binadamu nchini Tanzania ya mwaka 2022 iliyoandaliwa na kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) imeitaja mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, na Singida kuwa ya  kutupiwa macho kutokana na uvunjaji wa haki za binadamu ikiwemo vitendo vya ulawiti.

Hivi karibuni, Uganda ilipitisha sheria ya kudhibiti vitendo vya mapenzi ya jinsia moja ambapo mtuhumiwa akithibitika kujihusisha navyo anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 10 jela.

Nchini Tanzania, mijadala imekuwa ikiendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikidaiwa kufanyika maeneo mbalimbali hata katika taasisi za elimu ikiwemo shule za sekondari.

Wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakikosoa hatua zinazochukuliwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuzuia vitabu vyenye ishara za kufundisha mapenzi ya jinsia moja pamoja na kufungia taasisi zisizo za kiserikali ambazo zimebainika kujihusisha na masuala hayo.

Kupitia mtandao wa Twitter, Fatma Karume ambaye ni mwanasheria nguli katika baadhi ya machapisho yake amekuwa akiwasisitiza watu kuwa licha ya kupinga vitendo vya mapenzi ya jinsia moja wanapaswa pia kuheshimu faragha kwani ni haki ya binadamu.

“Pingeni ushoga ni haki yenu lakini msipinge kuwa mashoga ni binadamu kama binadamu wana haki ya faragha hamuoni kuna tofauti baina ya kupinga ushoga na kupinga uhai wao na haki yao ya faragha?, “ linasomeka chapisho hilo la Fatma ambaye ni Rais mstaafu wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mapenzi ya jinsia moja siyo sehemu ya haki za binadamu bali ni makosa ya jinai.

Enable Notifications OK No thanks