Dk Mpango achukizwa barabara kufungwa kupisha misafara ya viongozi

April 13, 2023 5:58 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuzingatia maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwapanga wafanyabiashara wadogo yaani Machinga katika maeneo yanafikika na watu ili waweze kufanya biashara kwa urahisi. Picha | Ofisi ya Makamu wa Rais.


  • Asema inawaletea wananchi usumbufu usio wa lazima.
  • Aagiza barabara kufungwa kwa dakika 10 tu kupisha misafara ya  viongozi.
  • Wabunge, wananchi nao wachukizwa. 

Mwanza. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amechukizwa na tabia ya baadhi ya watendaji wa Jeshi la Polisi kufunga barabara muda mrefu ili kupisha misafara ya viongozi akisema inawaletea usumbufu wananchi na kusimamisha shughuli za maendeleo. 

Dk Mpango ametoa kauli hiyo baada ya Mkuu wa Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza kufunga barabara ya Misungwi-Mwanza kwa saa nne Aprili 11, 2023 kusubiri msafara wa Makamu wa Rais upite. 

Hali hiyo ilisababisha shughuli za usafiri na uchumi katika mkoa huo wa Kanda ya Ziwa kusimama kwa muda. 

Kiongozi huyo wa Serikali aliyekuwa akizungumza jana Aprili 12, 2023 katika Mtaa wa Kisesa wilayani Magu amesema amechukizwa na kitendo hicho kwa sababu kinasababisha wagonjwa na wasafiri kushindwa kuendelea na majukumu yao wakisubiri “mtoto wa masikini kama Philip Mpango apite.”

“Niwaombe msamaha sana wananchi wa Kisesa na Mkoa wa Mwanza kiujumla, kitendo kilichofanyika jana (Aprili 11) cha barabara kufungwa kwa zaidi ya masaa 4 ili tu kupisha mtoto wa masikini kama Philip Mpango apite hakikunifurahisha na  suala la kufunga barabara nishazungumza.

“Naomba nirudie tena sio vizuri kufunga barabara kwa zaidi ya masaa mengi wekeni utaratibu vizuri dakika 10 tu zinatosha kabisa kufunga barabara kisha kuruhusu wananchi waendelee na majukumu yao,” amesisitiza Dk Mpango. 

Naye Mbunge wa Viti Maalum, Kunti Majala ameshauri mamlaka zinazosimamia misafara ya viongozi, kuwasiliana ili kupunguza muda wa watu kusimama njiani wakati wakiwasubiri wapite.

“Tunasema muda ni mali, wakati ni mali kusimamisha wananchi zaidi ya masaa matatu barabarani kiongozi hajatoka atokako tuna wagonjwa, tuna watu wanatekeleza majukumu yao mbalimbali. Mimi niombe viongozi wetu hususan Wizara ya Mambo ya Ndani wawe wanawasiliana kwa kadiri muda unavyosogea,” amesema Majala. 

Mbunge huyo ameyasema leo Aprili 12,2023 wakati akichangia mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/24.

Ameshauri kuwa kwa safari ndefu hasa za mikoani, viongozi watumie ndege ili kuwaruhusu wananchi kuendelea na majukumu yao.

Wananchi nao wachukizwa

Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Mwanza wamesema wanawaheshimu viongozi lakini kufunga barabara kwa muda mrefu na wakati mwingine bila taarifa kunawapa usumbufu mkubwa hasa kusimamisha shughuli za maendeleo kwa muda husika. 

“Mfano kama jana tumelala njaa yaani wamefunga barabara kwa muda mefu hivyo kushindwa kufanya biashara lakini pia linaathiri watu wanaosafiri na wanaopeleka wagonjwa hospitali,” amesema John John, mkazi wa Mwanza. 

George Marwa, mkazi wa jijini hapa amesema utaratibu mzuri ukiwekwa hakutakuwa na haja ya barabara kufungwa muda mrefu na kusababisha foleni isiyo ya lazima. 

Enable Notifications OK No thanks