Bosi wa UN Tanzania aanza kuwaaga viongozi wa Serikali

August 21, 2019 2:04 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Leo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.
  • Ni Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), Alvaro Rodriguez aliyemaliza muda wake.
  • Alianza kufanya kazi Tanzania mwaka 2014 na kuwa mstari wa mbele kuchagiza ajenda za maendeleo za vijana. 

Dar es Salaam. Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) anayemaliza muda wake, Alvaro Rodriguez ameanza kuwaaga viongozi wa Serikali ya Tanzania huku akiipongeza kwa namna inavyotumia vizuri rasilimali zake za ndani kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo sambamba na kupunguza utegemezi kutoka nje.

Rodriguez ambaye ametumikia nafasi hiyo kwa miaka mitano,  leo (Agosti 21, 2019) amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.

Rodriguez, aliyekwenda kumuaga Majaliwa, amesema kuwa Tanzania imeendelea kutumia vizuri mapato yake ya ndani kwa kuimarisha miundombinu na huduma za kijamii kama ujenzi wa hospitali na vituo vya afya.

“Katika kipindi changu cha miaka mitano ambacho nimefanya kazi Tanzania, nimeshuhudia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yanayofanywa na Serikali, ikiwemo kuimarika kwa mahusiano kati ya Serikali na Umoja wa Mataifa na taasisi zake nchini,” amesema Rodriguez. 

Katika kipindi cha uongozi wake nchini Tanzania, bosi huyo wa UN amekua mstari wa mbele katika kuchagiza masuala ya vijana hasa ujasiriamali na teknolojia ili kuondokana changamoto za ajira. 


Soma zaidi: Kiswahili ndiyo mpango mzima wa kusaka wateja Tanzania: Ripoti


Rodriguez tayari amekutana na kumuaga Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Mohammed Shein. 

Katika ukurasa wake wa Twitter, Rodriguez ameandika kuwa anawashukuru Watanzania na jumuiya za kimataifa kwa ushirikiano waliompa kufanikisha shughuli za UN nchini. 

Amesema baada ya kuondoka Tanzania, anakwenda kuwa Mwakilishi wa UN nchini Uturuki kwa miezi sita ijayo. 

Nafasi alizowahi kushika UN

Kabla ya kuanza kazi Tanzania mwaka 2014, alianza kufanya kazi na UN tangu mwaka 1991 katika  Shirika la maendeleo la umoja huo nchini Kenya.

Akiwa Tanzania ametoa mchango mkubwa katika mapitio ya Mpango wa kwanza wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa Tanzania (UNDAP I 2011-16) na kutengeneza mpango wa pili wa maendeleo (UNDAP II 2016-21). 

Mpango huo umejikita zaidi katika vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania hasa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030. 

Pia ameanzisha uhusiano na muingiliano wa karibu kati ya mifumo ya UN na mikoa, wilaya na jamii za Tanzania huku akisikiliza sauti za watu kuhusu masuala ya maendeleo. 

Akitumia taaluma yake amewahi kuwa Mkurugenzi Mkaazi wa UNDP nchini za Afghanistan, Pakistan na Somalia na amebobea katika masuala ya usimamizi wa chaguzi, kujenga uwezo wa maendeleo, uzuiaji wa migogoro na majanga, usimamizi wa mazingira na upunguzaji wa hatari za majanga. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akutana na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa,anaye maliza muda wake hapa Nchini Tanzania, Alvaro Rodriguez kwa ajili ya kumuaga ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam leo Agosti 21,2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW