‘Boni Yai’ aachiwa kwa dhamana
- Ni baada ya kukidhi masharti ya dhamana.
- Aahidi kutoa msaada wa kisheria kwa watu 20.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, na Kinondoni jijini Dar es Salaam Boniface Jacob maarufu kama ‘Boni Yai’ amepata dhamana, baada ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na upande wa Jamhuri kupinga dhamana yake.
Jacob amepata dhamana baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wenye barua za Serikali za Mitaa na kusaini bondi ya Sh saba milioni saba na pia ametakiwa asitoke nje ya nchi bila kibali cha Mahakama.
Uamuzi huo, umetolewa leo Oktoba 7,2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga aliyesema kuwa kiapo cha RCO wa Mkoa wa Polisi Kinondoni, Davis Msangi hakina maelezo ya ziada ya kutosha kuzuia dhamana hiyo ya Jacob.
Kwa mujibu wa Peter Kibatala aliyekuwa akiongoza jopo la mawakili wa kumtetea Jacob, RCO Msangi alikula kiapo cha kuweka zuio la dhamana kwa Boni yai kwa kuwa usalama wake utakuwa hatarini ikiwa atakuwa uraiani jambo ambalo mahakama imelipinga.
Boni yai ambaye pia ni Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anatuhumiwa kwa mashtaka mawili likiwemo la kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wake wa kijamii.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka ilidaiwa kuwa Septemba 12, 2024 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam alichapisha taarifa kwenye mtandao wa X zamani Twitter wenye jina la Jacob ex Meya Ubungo uliyosema”Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji ya moja kwa moja katika kuwapoteza watu wa baadhi ya familia zoa, Kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, kupotea kwa Deo Mugasa, kupotea kwa Adnandi Hussein Mbezi na kupotea kwa vijana watano wa Aggrey”.
Boni Yai alikamatwa na Jeshi la Polisi Septemba 18, 2024, maeneo ya Sinza jijini Dar es Salaam ambapo alipandishwa mahakamani Septemba 23, mwaka huu kusomewa mashtaka yanayomkabili ambayo upelelezi wake bado unaendelea.
Mara baada ya mahakama kutoa uamuzi huo Jacob ambaye amekaa jela kwa siku 20 amewashukuru wote waliohusika kuhakikisha anapata dhamana wakiwemo mawakili wake na huku akiahidi kutoa msaada wa kisheria kwa wafungwa 20 na kulipia faini ya wafungwa kumi ambao amekutana nao gerezani.