Barabara, umeme vyakwamisha kuanza mradi shamba la miwa Morogoro

March 15, 2021 6:48 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama akikagua  eneo la mto  Ruvu litakalotumika kama chanzo cha maji kwa shamba la Mkulazi lililopo eneo la Mkulazi, Morogoro vijijini. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Ni shamba la miwa la Mkulazi lilipo Morogoro ambapo kitajengwa kiwanda cha sukari.
  • Kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza tatizo la sukari Tanzania.
  • Serikali yataka ndani ya wiki mbili shughuli ya kujenga barabara, umeme ianze. 

Dar es Salaam. Serikali imeitaka kamati elekezi inayosimamia mradi wa shamba miwa la Mkulazi lilipo mkoani Morogoro kuanza haraka ujenzi wa barabara na kupeleka umeme katika eneo hilo litakalojengwa kiwanda cha sukari ili kupunguza uhaba wa bidhaa hiyo nchini Tanzania. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ametoa agizo hilo Machi 15, 2021 alipokagua shughuli za mradi huo unaotekelezwa katika shamba namba 217 lililopo Morogoro Vijijini. 

Mhagama ameitaka kamati hiyo ndani ya siku mbili kuanzia Jumanne Machi 16, 2021 kuwasilisha mpango wa namna watakavyotatua changamoto hizo  kwa wiki mbili.

“Maamuzi yalifanyika Novemba na hadi leo Machi hakuna kilichofanyika kwenye kufuatilia. Nataka mwezi huu wa tatu kabla haujaisha mitambo ianze ujenzi wa barabara hapa na nataka majibu ya lini shughuli za kuweka umeme hapa zinaanza. 

“Huu ni mradi wa kimkakati kwani tunao upungufu wa tani 200,000 za sukari ambazo zitazalishwa hapa. Kama hakuna kitakachofanyika nitachukua hatua kwenu, tumekubaliana tunaenda na mwendo wa ujenzi wa viwanda na hiki ni kiwanda muhimu sana,” amesisitiza Mhagama.

Shamba hilo ni sehemu ya kampuni hodhi iliyoanzishwa kwa ubia baina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Taifa  (NSSF) na Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) Septemba 2016, ambayo imepanga kujenga viwanda viwili katika maeneo ya Mkulazi  na Mbigiri wilayani Mvomero.

Viwanda hivyo kwa pamoja vitakapokamilika vinatarajiwa kuzalisha wastani wa tani 250,000 za sukari kwa mwaka na hivyo kupunguza uagizaji wa sukari nje ya nchi.


Soma zaidi: 


Akieleza changamoto zinazosababisha utekelezaji wa mradi huo usianze, Mwenyekiti wa bodi ya mradi Dk Hildelitha Msita, amebainisha kuwa kwenye makubaliano kati ya mradi na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), shughuli ya kupeleka umeme katika eneo hilo haikuwa kwenye bajeti yao. 

Hata hivyo, amesema tayari wamekubaliana na Tanesco kujenga njia ya umeme yenye urefu wa kilomita 3. 

“Mradi umekubali utatoa fedha  ambazo Tanesco itazilipa kupitia  kwenye makato ya ankala za umeme zitakazokuwa  zikihitajika kulipwa na mradi,  badala ya kulipwa gharama hizo kwa fedha ambazo zingelipwa na wananchi wenye uhitaji wa kujengewa njia  za umeme,” imeeleza taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu. 

Kujengwa kwa viwanda hivyo, kutaufanya mkoa wa Morogoro kuwa na viwanda vinne ukilinganisha na viwili vilivyopo sasa vya Mtibwa na Kilombero. 

Viwanda vingine vya bidhaa hiyo Tanzania ni Kagera Sugar cha mkoani Kagera na TPC kilichopo Mkoa wa Kilimanjaro. 

Meneja mradi, Abdul Mwankemwa ameeleza kuwa kutokuwepo kwa miundombinu mizuri ya barabara ya kuelekea shamba la Mkulazi, imesababisha mitambo ya kilimo, kazi ya kusafisha mashamba na kupanda kitalu cha miwa kushindwa kufanyika. 

Aidha, amefafanua kuwa mradi umekamilisha kufanya upembuzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 42 na matokeo ya upembuzi huo yametumika kuomba Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuchukua jukumu la kujenga barabara hiyo inayopitia Chalinze-Seregeta kuelekea kwenye shamba.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI, WIZARA YA MADINI IKIWASILISHWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI, WIZARA YA MADINI IKIWASILISHWA BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: RAIS SAMIA ANAZINDUA MELI YA KWANZA YA UVUVI WA BAHARI KUU

🔴LIVE: RAIS SAMIA ANAZINDUA MELI YA KWANZA YA UVUVI WA BAHARI KUU

Nukta TV

Nukta Africa kuzindua Nukta AI, siku ya uhuru wa vyombo vya habari

Nukta Africa kuzindua Nukta AI, siku ya uhuru wa vyombo vya habari

Nukta TV