Bajeti mikopo elimu ya juu yapaa, kuwanufaisha zaidi ya wanafunzi 160,000
- Imeongezeka kwa asilimia 18.5 hadi kufikia Sh570 bilioni kwa mwaka 2021/22.
- Kuwanufaisha wanafunzi zaidi ya 160,000.
- Dirisha la maombi kufunguliwa Julai 9 mwaka huu.
Dar es Salaam. Bajeti ya kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka 2021/22 imeongezeka kwa asilimia 18.5 hadi kufikia Sh570 bilioni, jambo linaloongeza uhakika kwa wanafunzi ngazi hiyo ya elimu kupata fedha za kugharamia ada na malazi wawapo chuoni.
Ongezeko hilo ni sawa na Sh106 bilioni ikilinganishwa na bajeti ya Sh464 bilioni iliyotumika mwaka 2020/21.
Kwa mujibu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) fedha hizo zilizotengwa kwa mwaka 2021/22 zinayotarajia kuwanufaisha zaidi ya wanafunzi 160,000.
Kati ya wanafunzi hao 160,000, wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanatarajiwa kuwa 62,000 wakati wanaoendelea na masomo watakua 98,000.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako aliyekuwa akizungumza leo Julai 2, 2021 jijini Dar es salaam katika hafla ya uzinduzi wa msimu mpya wa uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2021/22, amesema kiwango cha fedha kilichotengwa kwa 2021/22 kimevunja rekodi katika miaka 16 ya uhai wa HESLB.
“Niwaibie siri tu. Hadi mwezi uliopita, bajeti ya mikopo kwa mwaka 2021/2022 ilikua Sh500 bilioni. Lakini katika siku zake 100 za uongozi kama Rais wetu, Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan ameongeza Sh70 bilioni na kufikia hizi Sh570 bilioni kwa mwaka 2021/22 sawa na ongezeko la Sh106,” amesema Prof Ndalichako.
Mikopo hiyo husaidia wanafunzi kuweza kumudu gharama za masomo na maisha wakati wakiendelea na masomo ya elimu ya juu.
Hata hivyo, mikopo hiyo haiwafikii wanafunzi wote wanaojiunga na vyuo vikuu kila mwaka kwa sababu idadi ya wanafunzi inakuwa kubwa kuliko bajeti inayotengwa.
Mathalan, mwaka 2020/21, wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliotuma maombi ya mikopo walikuwa zaidi ya 70,000 lakini waliopata ni 55,287.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akipokea nakala ya mwongozo wa uombaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2021/2022 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdful-Rzaq Badru mara baada ya kutangaza mwongozo huo Ijumaa Julai 2, 2021 katika Ofisi za Heslb, Tazara Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe. Picha| HESLB.
Utaratibu wa utoaji mikopo 2021/22
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema kuanzia Julai 12 mwaka huu, maafisa wa HESLB wataanza kuendesha programu za elimu ya uombaji mikopo kwa usahihi chini ya kampeni ya #WeweNdoFuture.
“Tunakamilisha utaratibu na uongozi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili tuwafikie vijana wote waliopo katika kambi 19 za JKT kuanzia Julai 12 … tutaendesha pia programu hizi kupitia televisheni, redio, mitandao ya kijamii na mikutano na wadau,” amesema Badru.
Kuhusu utaratibu na muda wa kuomba, Badru amesema Mwongozo wa Uombaji mkopo unaoeleza sifa na utaratibu wa kuomba mkopo unapatikana katika tovuti ya HESLB.
“Mwongozo upo katika tovuti kuanzia leo, Julai 2 na tunawashauri waombaji wausome kabla ya kuomba. Aidha, mfumo wa kupokea maombi kuwa wazi kwa siku 53 kuanzia, Julai 9 hadi Agosti 31, 2021,” amesema Badru.
Latest