Azam yaibuka na App inayoweza kukomboa wafanyabiashara
- Inaondoa usumbufu wa usafiri na ulazima wa kufunga duka
- Haitoi huduma za Azam pekeyake kwani bidhaa za makampuni mengine zinapatikana
- Gharama za manunuzi zinajumuisha kodi na huduma ya risiti inapatikana
Dar es Salaam. Mara nyingi kufanya manunuzi ya jumla kwaajili ya dukani imeikuwa ni pasua kichwa kwa mfanya biashara yeyote ikiwemo usafiri au hata kulazimika kufunga duka tu ili kuifuata bidhaa hiyo.
Praxeda Mathias ni mhasibu kwenye hoteli ya Nothern Breeze Dar es Salaam. Yeye amesema katika kufanya manunuzi ya vitu vya jikoni vikiwemo unga, sukari na mafuta, inamlazimu kutenga muda walau mara moja kwa wiki ili kufanya manunuzi ya moja kwa moja.
Endapo vitu vikiisha kabla ya siku iliyopangwa, basi huwa anapata changamoto kwani anatumia pesa ya ziada kwenye usafiri na muda mwingine inasababisha baadhi ya vitu kupatikana kwa uchache vikiwemo vyakula..
Changamoto anazokutana nazo Mathias huenda zinawakumba wafanya biashara mbalimbali hata hivyo, huenda suluhisho la manunuzi likawa limepatikana na kurahishishwa baada ya kampuni ya Azam ambayo inazalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo maji ya kunywa na sharubati kuamua kungiza sokoni programu tumishi ya Sarafu.
Azam ambayo imeingiza sokoni programu tumishi (App) hiyo ya Sarafu ambayo inamuwezesha mtu kununua bidhaa siyo tuu za azam bali na zingine muhimu kama sabuni, sukari, mafuta na mengineyo na kufanya kurahisisha manunuzi ya jumla.
Nukta imejaribu kuiangalia App hiyo na kwa mtazamo wa kwanza, ni rahisi kutumika na mtu yeyote kwani kinachovutia zaidi ni kuwa inatumia lugha ya kiswahili.
App hiyo na kwa mtazamo wa kwanza, ni rahisi kutumika na mtu yeyote kwani kinachovutia zaidi ni kuwa inatumia lugha ya kiswahili. Picha| Rodgers George
Kwa kufanya manunuzi kwa App hiyo, inamuondolea mfanyabiashara umuhimu wa kufunga duka kwani baada ya manunuzi, bidhaa ilizonunua zinaletwa hadi kwenye duka lako. Kwa manunuzi yote utakayofanya, kodi zinakuwa zimeshajumuishwa.
Uzuri mwingine wa App hii ni kuwa unafanya malipo kwa njia ya simu ama kwa njia ya benki hivyo inampa mnunuzi mawanda mapana zaidi ya kufanya malipo.
Zinazohusiana
Apps 10 za kilimo zinazoweza kuwanufaisha wakulima Tanzania
Mbali na mazuri yote ya App hii, jambo ambalo huenda ni la kiusalama zaidi ni kwamba unalazimika kuingia kwenye akaunti yako ila mara kwani siyo kama App zingine ambazo ukishaingia kwenye akaunti yako mara moja unakuwa umemaliza.
Kwa mtumiaji wa Sarafu kuingia kwenye akaunti kila mara huenda ikawa kero kwa baadhi ya watumiaji wake.
Zaidi, App hii ni kwa manunuzi ya jumla yaani huwezi kununua sabuni moja bali katon au dazani kwa kila bidhaa utakayo nunua huku usafiri wa kufikisha bidhaa hizo ukiwa ni bure.