Apple kuingiza sokoni simu mpya ya iPhone 12 Oktoba
- Simu hiyo inakuja na matoleo manne ambayo yatakuwa na uwezo mkubwa wa utendaji kuliko matoleo yaliyopita.
- Simu hizo zitakuwa zinauzwa kuanzia Sh1.7 milioni.
- Simu hiyo ina kamera nne za nyuma.
Dar es Salaam. Kwa wadau wa iPhone, bila shaka shauku yao inazidi kupamba moto kulipokea toleo la 21 la simu hizo zinazotengenezwa na kampuni ya Apple ya Marekani.
Shauku hiyo ni kupata simu yenye uwezo mkubwa kuliko matoleo yaliyopita tangu Apple ilipoingiza sokoni toleo la kwanza Juni 2007.
Kwanini uanze kutafuta kibubu chako? Haya ndiyo tuliyoyasikia kuhusu iPhone 12 itakayoingia sokoni mwezi huu wa Oktoba.
Matoleo yanayotarajiwa
Mbali na simu ya iPhone11 ambayo ina matoleo matatu (iPhone 11, 11 Pro na 11 Pro Max), iPhone 12 inatarajiwa kuingia sokoni na matoleo manne; iPhone 12 mini ambayo inatarajiwa kuwa na ukubwa wa inchi 5.4 kwenye skrini yake.
Matoleo mengine ni iPhone 12, iPhone 12 Pro na iPhone 12 Pro Max ambazo zitakuwa na ukubwa wa skrini unaofikia inchi 6.1, 6.1 na 6.7 mtawaliwa.
Kwa muonekano wa iPhone 12, huenda kati ya simu nne zinazotarajiwa, ikawepo ambayo ina hadi lensi au macho manne ya kamera. Picha| Roamingbuzz.
Ukubwa wa uhifadhi wa kumbukumbu
Matoleo hayo manne ya simu yanatarajiwa kuwa na uhifadhi wa RAM (Uhifadhi wa kumbukumbu wa muda mfupi) usiopungua GB 4 kwa kila toleo.
Kwa iPhone 12 mini na iPhone 12 zinatarajiwa kuwa na uhifadhi wa RAM wa GB4.
iPhone 12 Pro inatarajiwa kuwa na RAM ya GB6 sawa na 12 Pro Max. pia simu hizo zinatarajiwa kuwa na uhifadhi wa kumbukumbu wa muda mrefu (ROM) unayoanzia GB128, GB256 na GB512.
Vipi kamera?
Kamera ni kitu cha kingine cha kuangalia kwa wapenda picha wengi na ni hakika kamera za toleo la iPhone hazijawahi kumkata mtu maini.
Kwa toleo la simu la iPhone 11, ziliwavutia watu wengi kwa uwezo wake wa kupiga picha na kurekodi video kwa ubora hadi ndani ya maji huku wadau wakiipenda zaidi kwa kuwa na macho au lensi tatu za kamera.
Kwa muonekano wa iPhone 12, huenda kati ya simu nne zinazotarajiwa, ikawepo ambayo ina hadi lensi au macho manne ya kamera.
Soma zaidi:
- Sababu za wabunifu wa nguo kutumia malighafi za nje
- Kiti cha ofisini: Rafiki au adui wa afya yako?
- Ushindani nguo za mtumba, dukani unavyowafaidisha wanunuzi Tanzania
Bei inayotarajiwa
Ili kuhama kutoka kwenye simu uliyonayo na kumiliki toleo la simu hiyo, sio mbaya ukaandaa walau Sh1.7 milioni kumiliki iPhone 12 mini.
Kama utahitaji toleo kubwa zaidi, sio haba ukaandaa Sh2.7 milioni na huenda bei ikazidi hapo kwani hizo ni bei za makadirio zilizotolewa na Toms Guide ambao ni wadau wa teknolojia ya simu.
Uko tayari kuhama kutoka kwenye simu uliyonayo kufikia iPhone12? Kazi ni kwako.