Aliyekuwa RC Simiyu apandishwa kizimbani Mwanza kwa mara ya kwanza

July 9, 2024 1:47 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Nawanda amepandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza tangu jeshi la polisi mkoani Mwanza litangaze kumtia nguvuni Juni 13 mwaka huu.
  • Hata hivyo mtuhumiwa amekana kosa na kesi hiyo itasikilizwa tena Julai 16 mwaka huu.

Mwanza. Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Yahaya Nawanda, amefikishwa katika Mahakama ya  Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza na kusomewa shitaka moja la kumwingilia kinyume na maumbile Tumsiime Ngemela (21) katika eneo la Rock City mall jijini Mwanza.

Mshitakiwa huyo amefikishwa katika mahakama hiyo mapema leo Julai 9, 2024 na kusomewa shitaka hilo ambalo anadaiwa kulitenda Juni 2, 2024  kinyume na kifungu cha 154 (a) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022

Waendesha mashitaka wa kesi hiyo ambao ni Wakili wa Werikali Magreth Mwaseba na Martha Mtiti waliitaja kesi hiyo kuwa ni kesi namba 1883 ya mwaka 2024 mbele ya Erick Maley, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo.

Hata hivyo mshtakiwa alikana shitaka hilo na yuko nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti aliyokuwa amewekewa ambayo ni kuwa mtumishi wa Serikali pamoja na bondi  ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh5 milioni.

Mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana hadi Julai 16, 2024 ambapo kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa hoja za awali huku upande wa mlalamikaji ukitakiwa kupeleka mashahidi.

Akizungumza nje ya mahakama, Wakili wa upande wa utetezi, Constantine Mtalemwa amesema kwa sasa wanaiachia mahakama namna itakavyoendeshwa kesi hiyo na kwamba kesi ni ya wazi hivyo watanzania  wote wanaruhusiwa kuifuatilia.

“Jambo linapokuja mahakamani tunaiachia mahakama  hatuwezi kuanza kuongelea ushahidi kwa kuwa kesi haijaanza  na wananchi wanakaribishwa kuja kusikiliza kwakuwa ni kesi ya wazi,” amesema Mtalemwa.

Mshitakiwa  huyo anapandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza ikiwa ni ni takribani wiki tatu tangu akamatwe na kufikishwa kituo kikuu cha polisi cha wilaya ya Nyamagana Juni 13 mwaka huu.


Soma zaidi: Rais Samia: Tunahitaji mapato ili tupunguze kukopa


Alivyoingia mahakamani

Mshitakiwa huyo aliingia mahakamani majira ya saa 4.00 asubuhi akitumia  gari aina ya Toyota landcruiser huku akiwa amezungukwa na ulinzi mkali wa polisi ukiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mwanza Saudi Yessaya.

Enable Notifications OK No thanks