Alama za vidole zinavyotumika kusajili laini kinyemela
- Baadhi ya mawakala wamelalamikiwa kukosa uaminifu na kutumia namba ya NIDA za watu kusajili namba kwa wateja tofauti.
- Uhakiki wa mara kwa mara wa usajili wa laini husaidia.
- TCRA yawataka watumiaji kuhakiki laini zao mara kwa mara kukabiliana na uhalifu.
Dar es Salaam. Joseph Richard, mkazi wa Ununio jijini Dar es Salaam alikutana na wakala wa usajili wa namba za simu kwenye daladala aliyemshawishi amsajilie laini ya simu kwa haraka.
Kama ilivyo ada katika kufuata usajili wa sasa, Richard aliweka alama ya kidole kwenye mashine ya wakala ili kuweza kunakili na kuthibitisha taarifa zake wakati safari yao ikiendelea kutoka Makumbusho kwenda Ununio.
Hata baada ya kuweka alama hizo, wakala huyo alimwambia warudie upya hatua za usajili kwa sababu wa awali haukukamilika.
Baada ya kuweka tena alama ya kidole aliambiwa mchakato umekamilika hivyo anaweza kuendelea kutumia laini yake, lakini alipofika kwake alishindwa kuitumia sababu ya kufungiwa na mtoa huduma.
“Nilisajiliwa kwenye daladala, yule wakala aliponisajilia mara ya kwanza akaniambia kwamba bado haijakaa (laini) sawa, akanisajilia mara ya pili, aliposhuka laini yangu ikajifunga, ikabidi niende kwa wakala mwingine akanielekeza kwamba kitambulisho changu kimesajiliwa namba nyingine” ameeleza Bw. Joseph
Hii ni kwa sababu aliidhinisha matumizi ya NIDA yake mara mbili kwa alama ya kidole kwa usajili wa laini moja na hivyo kubatilisha’ usajili wa laini yake ya awali.
Joseph ni miongoni mwa wengi wanaokumbwa na kadhia ya taarifa zao binafsi kutumika kufanya usajili wa laini nyingine za simu bila ridhaa yao na kuwaachia matokeo hasi kama kutumika kiutapeli.
Baadhi ya watumiaji wamejikuta wakiibiwa pesa mtandao au namba zao kutumika katika matukio ya ulaghai bila yao wa kujua jambo linaloongeza hatari zaidi za kisheria na kuharibu jina la mwenye namba ya NIDA.
Baadhi ya mawakala wasiowaaminifu hutumia fursa hiyo kwa ajili kujiingizia kipato kwa kusajili laini nyingi au kutumia mbinu za kijanja kulaghai fedha wanapotoa huduma.
Abaini namba tatu zimesajiliwa kinyemela
Dereva wa bodaboda Makambusho jijini Dar es Salaam, Aaron Kamdangi anasema aliwahi kubaini usajili wa laini saba zilizotumia namba yake ya NIDA baada ya kufanya zoezi la uhakiki, tofauti na idadi ya laini nne alizosajili mwenyewe.
Alipowasiliana na wenye namba hizo, Kamdangi anasema wahusika hao walimweleza kuwa wameuziwa laini zilizokamilishwa usajili na wakala.
Baadhi ya mawakala wameeleza kuwa ni mawakala wachache ambao wanachafua taswira ya kazi hiyo na kwamba kwa sehemu kubwa mteja anaweza kuzuia jambo hilo lisitokee.
Mwaka 2023 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilizipiga faini ya jumla ya zaidi ya Sh2 bilioni kampuni za Airtel, Tigo, Vodacom, Halotel, na TTCL kwa kusajili laini zaidi ya tano kwa kutumia kitambulisho kimoja kama inavyopaswa kwa mujibu wa kanuni ya 37 ya usajili wa laini.
Wakala wa usajili laini maeneo ya Morocco Catherine Samwel anasema kiuhalisia ni ngumu kwa wakala kuchukua namba yako ya NIDA na kwenda kumsajilia mwingine kwa sababu alama za vidole huitajika kwenye kila usajili.
“Utakapoona wakala anaekusajilia laini anazuga (anapoteza muda) mpaka dakika 30 zimepita jua kabisa lazima atakupitishia laini ya pili, huo ndio umakini unaohitajika,” anasema Catherine.
Baadhi ya mawakala wanawatupia lawama wateja kwa kuwa na umakini mdogo kiasi cha kujikuta wakiingia katika mitego ya watu wanaojifanya ni mawakala kumbe ni walaghai au mawakala ambao si waaminifu.
“Suala la kumsajilia laini mtu zaidi ya mmoja kwa namba ya NIDA linasababishwa na mteja kukosa umakini kwani kitambulisho kimoja kinapotumika kusajili namba tofauti mfumo hutumia takribani nusu saa kukamilisha usajili wa namba inayofuata,” amesema Theresia Samwel, Wakala wa kusajili laini za mtandao wa Tigo jijini Dar es Salaam.
Mbinu za kubaini wakala mjanjajanja
Teresia, ambaye hufanya shughuli zake eneo la Morocco, anasema ili kudhibiti uhalifu huo mteja anapaswa kuepuka kurudia rudia kuweka alama ya kidole chake zaidi ya mara moja na endapo kuna tatizo kwenye mfumo wa usajili na kulazimika kurudia zoezi la usajili wakala anapaswa kumwonesha mteja ujumbe utakaotumiwa kwenye kishikwambi chake kutoka kwa mtoa huduma.
Sheria ya mawasiliano ya kielektroniki na posta kupitia mwongozo wa usajili wa laini kwa alama za vidole (kibiometria) uliotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) 2020 kwenye kanuni ya nne inazuia mtu yeyote kufanya usajili wa laini za simu kwa kutumia kitambulisho cha taifa cha mtu mwingine.
Ili kuhakikisha unalinda na kuzuia kabisa namba yako ya simu isitumike, mamlaka na watalaamu wa Tehama wanasisitiza kutumia njia mbalimbali ikiwemo kuhakiki mara kwa mara iwapo namba yako ya NIDA imetumika kusajili laini nyingine ama la ili kuzisitisha kabla ya kuleta madhara.
Hakiki mara kwa mara usajili wako
Mtumiaji anapaswa kufanya uhakiki wa laini zake mara kwa mara ili kumwezesha kubaini namba za simu zilizosajiliwa kwa jina lake bila yeye kutambua na kurahisisha hatua za kubaini wakala anaeweza kuwa ametenda kosa hilo.
“Laini ikipita hakikisha anakuonesha ujumbe kwenye kifaa chake cha kazi unaosema uwasilishaji wako umefanikiwa, usimruhusu wakala achukue simu yako mwambie akuelekeze taratibu za kufuata ufanye mwenyewe,” ameongeza Catherine.
Watoa huduma za mawasiliano ya simu wana wajibu wa kisheria kuwalinda watumiaji wao dhidi ya uhalifu wa mtandaoni, mtandao wa Tigo hutoa taarifa ya jina na wakala na idadi ya namba zote za simu zilizosajiliwa kwa kutumia kitambulisho cha mtumiaji punde anaposajili laini mpya kumwezesha kubaini endapo kuna namba za simu asizozitambua.
Faida za kuhakiki usajili mara kwa mara
Kuimarisha ulinzi wa taarifa zako binafsi zisitumike vibaya na watu wasio na nia njema wanaofanya usajili wa kadi za simu na kuzitumia kufanya majaribio ya kitapeli kwa njia ya kupiga simu au kutuma ujumbe.
Kuzuia mwanya wa ulaghai na matendo ya jinai kwa njia ya mtandao kwa kuhakikisha kila kadi ya simu inamilikiwa na mtu sahihi dhidi ya watu wanaotumia mbinu ya kununua kadi zilizosajiliwa kikamilifu bila ya utambulisho wao.
Kuhakiki usajili wa laini kunamaanisha kukagua kama taarifa zako binafsi zilizosajiliwa zinazotumika na watoa huduma wa simu zinawiana na zilizo kwenye mfumo wa NIDA kwa lengo la kuhakikisha kila laini ya simu inamilikiwa na mtu halisi na kuzuia matumizi mabaya ya mtandao.
Mkuu wa Mawasiliano wa TCRA Rolf Kibaja anawataka Watanzania kutumia namba maalumu za USSD yaani USSD Code ili kuhakiki usajili wao mara kwa mara kuepuka kadhia ya namba zao kutumika kitapeli hususan kipindi hichi ambapo majaribio ya ulaghai kupitia mtandao yanzidi kuongezeka.
Majaribio ya ulaghai nchini yameongezeka kwa asilimia 57 kwenye kipindi cha miezi sita kutoka Januari mpaka Juni 2024.
Kampuni zote za mawasiliano nchini wana huduma ya USSD codes maalum kwa ajili ya kuangalia hali ya usajili wa laini za wateja wao.
Kuhakiki kwa USSD Code, Piga *106# kisha chagua, namba zilizosajiliwa mitandao yote kwa NIDA yako, mtoa huduma atakuletea namba zote zilizosajiliwa.
Wasiliana na mtoa huduma wako kwenye namba ya huduma kwa wateja ambayo ni 100 kwa mitandao yote ili wakusaidie kuangalia hali ya usajili wa laini yako na ikibidi kuboresha taarifa zako binafsi kama nywila.
Endapo kuna ulazima wa kuondoa namba ya simu iliyosajiliwa kwa namba yako ya NIDA unahitajika kutembelea duka lolote la mtoa huduma wa mtandao wako lililopo karibu
Mbinu nyingine ya ziada kutumia portal ya TCRA kuangalia namba zilizosajiliwa mitandao yote kwa kujaza namba ya kitambulisho cha taifa na nambari ya simu yako.
Ukitapeliwa nenda polisi
Iwapo mtu atatapeliwa, Kibaja amesema ni vema mtu huyo akaenda kuripoti polisi ili waweze kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kuwakamata wahusika.