Ajali, magonjwa ya kazini yanaua watu milioni 2 kila mwaka-WHO
- Vifo hivyo husababishwa na kufanya kazi muda mrefu na mazingira yasiyo rafiki ya kazi.
- Serikali duniani zatakiwa kuimarisha sera na sheria mahala pa kazi.
Dar es Salaam. Takribani watu milioni 2 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ajali na magonjwa yanayowapata wakiwa kazini ikiwemo ya mfumo wa hewa na moyo, jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi kuboresha mazingira ya kazi.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa makadirio ya kwanza kabisa ya mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la afya ulimwenguni (WHO) na lile la ajira duniani (ILO) katika ripoti yao ya utafiti wa kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2016.
Ripoti hiyo iliyotolewa Septemba 17, 2021 mjini Geneva, Uswisi imesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yalichangia asilimia 81 ya vifo hivyo.
Mathalan, magonjwa sugu ya njia ya hewa yalisababisha vifo 450,000, mshtuko wa moyo vifo 400,000 na ajali kazini vifo 360,000 .
Utafiti huo ulizingatia vigezo 19 vya mazingira hatarishi kazini ikiwemo kufanya kazi muda mrefu kupindukia, kufanya kazi katika mazingira yenye hewa chafuzi, mazingira yenye hewa au vitu vya kusababisha saratani na sauti kupindukia.
Kufanya kazi kwa saa nyingi kupindukia kulihusishwa na vifo 750,000 huku kukumbwa na hewa chafuzi na moshi vifo 450,000.
“Inashtusha sana kuona watu wengi wanauawa na kazi zao. Ripoti yetu ni kengele ya kuamsha serikali na sekta ya biashara kuboresha na kulinda usalama wa afya kazini kwa wafanyakazi wao kwa kuzingatia ahadi za kuwapatia wafanyakazi huduma za afya kazini na usalama katika maeneo yao ya kazi,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedros Ghebreyesus wakati akizungumzia ripoti hiyo.
Mazingira yasiyoridhisha ya kazi ni chanjo cha magonjwa na vifo kwa wafanyakazi. Picha| Mariam John.
Ripoti hiyo imesema kuwa magonjwa yahusianayo na kazi sambamba na majeraha ya ajali kazini yanazidishia mzigo sekta ya afya, yanapunguza tija na yanaweza kuwa na athari kubwa katika kipato cha familia.
Vifo vitokanavyo na ajali kazini au mazingira ya kazi vilipungua kwa asilimia 14 katika kipindi hicho cha mwaka 2000 hadi 2016 kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya usalama kazi duniani.
Hata hivyo, ripoti hiyo imesema bado vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo na mshtuko wa moyo vilivyohusishwa na kufanya kazi kwa muda mrefu viliongezeka kwa asilimia 41 na 19 mtawalia.
Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Ryder amesema “ Serikali, waajiri na waajiriwa wanaweza kuchukua hatua kupunguza vihatarishi kazini. Mazingira hatarishi kazini yanaweza kupunguzwa kwa kubadili mfumo wa utendaji kazi.”
Ripoti hii ya pamoja ya WHO na ILO ni ya kwanza na itawezesha watunga sera kufuatilia hasara ambayo Tanzania inapata kutokana na ajali kazini kitaifa, kikanda na kimataifa.
Kila kisababishi cha ajali kazini au vifo kimewekewa pendekezo lake la kudhibiti ambapo mwajiri na muajiriwa wanapaswa kuingia makubaliano.
Mathalan, kuzuia mfanyakazi kufanya kazi kwa saa nyingi kupindukia kunaweza kudhibitiwa kwa makubaliano ya muda unaokubaliwa kiafya kufanya kazi huku kule kupata magonjwa kutokana na kuvuta hewa chafuzi, kunapendekezwa wafanyakazi kupatiwa barakoa.
Latest
