Airbus yatundika daruga kutengeneza ndege za kifahari za Airbus-A380 Superjumbo
- Kampuni ya Airbus imesema haitatengeneza tena ndege aina ya A380 na toleo la mwisho litatoka mwaka 2021 kutokana na kupungua kwa soko la ndege hizo.
- Ndege ya kwanza ya A380 ilisafiri ikiwa chini ya Shirika la ndege la Singapore mwaka 2007.
- Ndege hizo zinasifika kwa uwezo wake wa kubeba watu wengi na kutua katika viwanja vikubwa duniani.
Kampuni ya kutengeneza ndege ya Airbus imetangaza kusitisha utengenezaji wa ndege aina ya A380 Superjumbo baada ya miaka 12 ya kusafiri angani.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na kampuni hiyo jana (Februari 14, 2019) imeeleza kuwa ndege ya mwisho aina ya A380 itatolewa 2021 na sasa itaelekeza nguvu zake katika utengenezaji wa ndege ndogo zenye gharama nafuu.
Uamuzi huo umekuja baada ya Shirika la ndege la Emirates ambalo ni mteja mkubwa wa ndege za Airbus kusitisha oda ya kununua ndege hizo na kuweka oda ya kununua ndege ndogo 70 aina ya A350 na A330.
Wachambuzi wa masuala ya usafiri wa anga wanasema kampuni hiyo ya Airbus ilikuwa inamtegemea mteja mmoja ambaye ni shirika la ndege la Emirates na kwa mantiki hiyo hawawezi tena kuendelea kutengeneza ndege aina ya A380 zenye uwezo wa kubeba abiria 500 hadi 600.
“Kufuatia uamuzi huu hatuna tena mteja wa A380 na hatuwezi kuendelea na uzalishaji, licha ya juhudi zote za kuuza kwa mashirika mengine katika miaka ya hivi karibuni. Hii inatuongoza kuwa mwisho wa kutoa A380 ni 2021,” ameeleza Ofisa Mtendaji Mkuu wa Airbus, Tom Enders katika taarifa hiyo.
Mpango wa kutengeneza aina hizo za ndege ulianza mwanzoni mwa miaka ya 1990 ambapo zinapendwa kutokana na uwezo wake wa kubeba watu wengi kwa wakati mmoja na kutua katika viwanja vikubwa duniani kama ‘Heathrow cha nchini Uingereza na ‘O’Hare Chicago nchini Marekani.
Kila ndege aina ya A380 inauzwa takribani Dola za Marekani 445 milioni sawa na zaidi ya Sh1 trilioni.
Safari ya kwanza ya kibiashara ya ndege hiyo ilikuwa mwaka 2007 na ilifanywa na shirika la ndege la Singapore kutoka nchini Singapore hadi katika Jiji la Sydney, Australia.
Mashirika ya ndege ya Uingereza, Ufaransa, China na Emirates ni miongoni mashirika 13 yaliyotumia ndege hizo katika safari zake huku mashirika ya ndege ya Marekani na nchi zote za Amerika Kusini na Afrika hayajawahi kununua ndege hizo.
Ndege ya Airbus aina ya A380 yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 500 na uwezo wa kutua katika viwanja vikubwa duniani. Picha|El Español
Kuondoka kwa A380 sokoni sio mwisho wa kampuni ya Airbus kuendelea kutengeneza ndege za aina nyingine ikizingatiwa kuwa imeanza kuiuzia ndege hadi Serikali ya Tanzania. Mwishoni mwa mwaka 2018 na mwanzoni mwa mwaka huu, Serikali ilipokea ndege mbili aina ya Airbus A220-300.
Soma zaidi: Nini kinafuata baada ya Fastjet kusitisha safari zake?
Ndege za Airbus A220-300 ambazo ni za kwanza kuingia barani Afrika, zina urefu wa mita 38.7 na urefu wake kutoka chini kwenda juu ni mita 11.5, na upana wa mabawa yake ni mita 35.1 huku ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 141.
Airbus 220-300 inaweza kusafiri umbali wa kilomita 5,920 safari moja, na inaweza kupaa ikiwa na uzani wa tani 67.6, na kutua ikiwa na uzani wa tani 58.7.
A220-300 ndiyo ndege kubwa miongoni mwa ndege za familia ya A220 na iliundwa kulenga soko la safari za ndege zinazowabeba abiria kati ya 130-160.