Aidan Eyakuze aondoka Twaweza kujiunga na OGP
- Ni baada ya kufanya kazi kama Mkurugenzi Mtendaji kwa miaka 10.
- Aahidi kuendeleza jitihada za kujenga Serikali zenye uwazi Afrika.
Arusha. Shirika la Twaweza Afrika Mashariki limetangaza kuondoka kwa Aidan Eyakuze, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo ambaye anatarajia kujiunga na Open Government Partnership (OGP).
Eyakuze aliyehudumu Twaweza kwa miaka 10 anakuwa miongoni mwa viongozi waliowezesha shirika hilo kufanikisha miradi ya mabadiliko iliyowawezesha wananchi na kuimarisha sauti zao katika utawala.
Chini ya uongozi wake, Twaweza imepiga hatua kubwa katika kutekeleza dhamira yake ya kukuza Serikali inayotokana na nguvu za wananchi na kufanikisha matokeo chanya Afrika Mashariki.
Atakumbukwa kwa mchango wake uliofanikisha kuimarisha ushirikiano wa asasi za kiraia kupitia shughuli kama Wiki ya Asasi za Kiraia nchini Tanzania, ‘People Dialogue Festival’ nchini Kenya, na juhudi za upatikanaji wa taarifa nchini Uganda.
Akizungumza baada ya kuaga nafasi hiyo Aidan amesema anaimani kiongozi anayefuata ataendeleza kasi ya utendaji kazi ya shirika hilo katika miaka ijayo.
“Imekuwa heshima kubwa kuhudumu na Twaweza kwa miaka kumi iliyopita…Kazi muhimu ya Twaweza inaendelea na nina imani kamili kwamba Mkurugenzi Mtendaji anayefuata ataendeleza kasi hii.”
Baada ya kutumika katika Shirika hilo Aidan anatarajiwa kujiunga na shirika la Open Government Partnership (OGP) atakapotumika katika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na shirika hilo Aidan anatarajiwa kuongeza nguvu katika kujenga Serikali zenye uwazi, na ushirikishwaji wa wananchi barani Afrika na kwingineko, hali inayoliweka OGP katika nafasi nzuri ya kuimarisha dhamira yake.
Baada ya kujiunga na OPG Aidan amesema atashirikiana na jumuiya hiyo kuendeleza masuala muhimu ikiwemo kujenga Serikali zenye uwazi Afrika na duniani kwa ujumla.
“ kipindi hiki chenye changamoto na fursa kubwa, dhana ya Serikali yenye uwazi ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Kwa pamoja, tutaendelea kuvunja mipaka, kuleta ubunifu, na kutekeleza mageuzi yenye maana ambayo yataboresha maisha ya watu na kurejesha imani kwa Serikali.” amesema Aidan.
Baada ya kutolewa kwa taarifa rasmi ya kiongozi huyo kuhamia OPG, baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamempongeza Aidan huku wakielezea mchango wake katika jamii.
Khalifa Said,mwandishi na mhariri wa The Chanzo kupitia ukurasa wake wa X amemuelezea Aidan kama kiongozi bora, mlezi na mwalimu bora kwa wakati wote aliomfahamu.
“Hili ni jambo gumu kukubali, binafsi nimemfahamu Aidan kwa takriban miaka saba. Amekuwa rafiki mzuri, mshauri, chanzo cha msukumo, na mwalimu kwa miaka yote hii. Namshukuru sana na ninamtakia kila la heri.” amesema Khalifa.
Naye Mary Goreth Nakabungo, mtumiaji mwingine wa mtandao wa X amemshukuru Aidan kwa miaka yote ya uongozi iliyowezesha kuzaliwa kwa mashirika mengine ikiwemo Twaweza Kenya na Uganda.