Ahueni: Zaidi ya watu 64,000 watoka kwenye ukame wa maji Mwanza

June 14, 2021 3:11 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Waanza kupata maji safi na salama baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua mradi mkubwa wa maji wilayani Misungwi.
  • Awataka kutunza vyanzo vya maji na kulipa bili zao maji kwa wakati kurejesha mkopo.

Mwanza. Wakazi zaidi ya 64,000 mkoani Mwanza sasa wameanza maisha mapya baada ya kuzinduliwa mradi mkubwa wa maji utakaowapatia uhakika wa maji safi na salama.

Mradi huo wa maji wenye thamani Sh13.77 bilioni utawahudumia wakazi hao wa wilaya ya Misungwi ambao kwa muda mrefu sasa walikuwa wakihaha kupata huduma hiyo muhimu kwa maisha ya mwanadamu na shughuli za maendele.

Katika uzinduzi wa mradi huo leo Juni 14, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wakazi wa wilaya hiyo ya Kaskazini mwa Tanzania kutunza vyanzo vya maji na kutoa tozo za matumizi ya maji ipasavyo ili kuhakikisha mradi huo unadumu kwa muda mrefu zaidi.

Mradi huo umejengwa kwa ufadhili wa nchi wahisani ikiwemo Tanzania, Shirika la Maendeleo la Ufaransa pamoja na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya.

Mradi huu ni miongoni mwa mingine mitano inayotekelezwa kupitia programu  ya majisafi na usafi wa mazingira ambayo hadi kukamilika kwake itagharimu zaidi ya Sh276 bilioni.

Kukamilika kwa miradi hii itanufaisha zaidi ya wakazi 64,000 wanaoishi maeneo ya vijijini.

Rais Samia amesema kwa sasa miradi inayozinduliwa imeunganishwa kwenye chanzo cha Ziwa Victoria ambacho huko baadae kinaweza kukauka.

“Niwaombe wananchi waendelee kutunza mazingira na kutoharibu rasilimali muhimu ya vyanzo vya asili vya maji, “amesema kiongozi huyo wa juu wa nchi akiwa katika siku ya pili ya ziara yake katika mkoa wa Mwanza. 

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Misungwi mkoani Mwanza 14 Juni, 2021 ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani humo. Picha|Ikulu. 

Kumekuwa na hofu kubwa miongoni mwa wadau wa mazingira ulimwenguni kuwa iwapo vyanzo vya maji vya sasa havitatunzwa ipasavyo, vizazi vijavyo vitaishi katika dunia yenye uhaba mkubwa wa maji.  

Rais Samia pia amesisitiza pia suala la wananchi kuendelea na taratibu za kuvuna maji ya mvua ili kuendelea kuwa na maji mengi nchini.

Uvunaji wa maji ya mvua husaidia kupunguza utegemezi wa maji yanayotoka katika vyanzo vya ardhini na ni moja ya njia inayosaidia kutunza maji mengi. Maji hayo huvunwa wakati msimu wa mvua na huifadhiwa katika visima hususan katika maeneo kame.

“Niagize mamlaka ya maji kuacha kubambikiza wananchi bili za maji na wananchi wasiache kulipa bili na hili na kuagiza Waziri (wa Maji) kuhakikisha suala hili linatekelezwa ili tuweze kulipa deni ambalo wabia wametupatia, ” amesema Samia.

Ili kuhakikisha miradi hiyo inadumu, Waziri wa Maji  Jumaa Aweso amewaagiza madiwani kusimamia miradi huo na mingine ili iweze kuwanufaisha wananchi

Amesema endapo madiwani hao watasimamia kwa weledi kutapunguza changamoto inayojitokeza ya uharibifu wa miundombinu.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW