Ahueni, maumivu ya kodi bajeti ya 2019-2020 kuanza leo

July 1, 2019 8:14 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni ya kodi mpya, zilizofutwa, zilizopunguzwa na zilizopata msamaha ambazo zinaanza kutumika leo (Julai 1,2019) mwaka mpya wa fedha.
  • Maumivu yako zaidi katika ushuru wa mawigi yanayotengenezwa na kuingizwa Tanzania.
  • Zinatarajia kuchangia mapato ya Serikali ya Sh33.11 zinazohitajika kutekeleza Bajeti Kuu. 

Dar es Salaam. Utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2019/ 2020 unaanza leo (Julai 1,2019) ukiambatana na viwango mbalimbali vya kodi vilivyoongezwa au kupunguzwa na Serikali, jambo linaloleta ahueni au maumivu kwa wafanyabiashara na watumiaji wa bidhaa na huduma husika Tanzania. 

Viwango hivyo vinajumuisha kodi mpya, zilizopata msamaha, zilizopunguzwa na zile zilizofutwa kabisa.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipendekeza viwango hivyo vya kodi Juni 13, 2019 wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2019/2020 kabla ya Wabunge kuijadili na kisha kuipitisha ambapo utekelezaji wake unaanza rasmi leo. 

Hata hivyo, zipo baadhi ya kodi ziliibua mjadala mkubwa kwa wabunge na wananchi ikiwemo kufuta msamaha wa kodi kwenye taulo za kike ambapo baadhi ya wachangiaji wamedai kuwa kodi hiyo inazidi kumuumiza mwanamke. 

Lakini Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisisitiza kuwa kodi hiyo haikuwasaidia walengwa na kwamba dhamira ya Serikali ni njema kwa kuwa kodi ina mchango mdogo kwenye bei ya mwisho ya bidhaa hiyo.


Zinazohusiana: 


Wakati wadau wakilia kuhusu kodi kwenye taulo za kike, maumivu mengine yapo kwa watumiaji na wafanyabiashara wa nywele bandia (mawigi) ambao wanatakiwa wajipange kulipa viwango vipya vya ushuru katika bidhaa hiyo.

Kuanzia leo, Serikali inaanza kutoza ushuru wa asilimia 10 kwenye nywele za bandia zinazotengenezwa ndani ya nchi na asilimia 25 kwenye nywele bandia zinazoagizwa kutoka nje ya nchi. 

Licha ya ushuru huo kupata upinzani kwa madai kuwa utawaumiza wanawake ambao ndiyo watumiaji wakubwa wa bidhaa hiyo, Serikali imesisitiza kuwa ushuru huo ni muhimu kwa sababu ni chanzo kizuri cha mapato. 

Hapana shaka utekelezaji wa viwango hivyo vipya vya kodi kwa nywele bandia utachangia kuongezeka kwa  bei ya bidhaa hizo zinazotumiwa zaidi na wanawake nchini kwa ajili ya urembo.

Pia tozo ya leseni ya udereva sasa inatozwa kwa Sh70,000 badala Sh40,000 ya awali, huku ada ya kadi ya usajili wa magari ikiwa ni Sh50,000 kutoka Sh10,000 ya mwaka uliopita. Hata hivyo, tozo hizo mpya za leseni ya udereva inaenda sanjari na kuongezwa kwa muda wa upatikanaji wa leseni kutoka miaka mitatu ya awali hadi miaka mitano.

Wamiliki wa pikipiki nao kuanzia leo wanatakiwa kulipa ada ya usajili ya Sh20,000 huku wa pikipiki za matairi matatu (bajaj) wakilipa Sh30,000. 

“Lengo la mapendekezo haya ni kupunguza gharama za kuchapisha leseni kwa kipindi cha miaka mitatu kwani leseni hizo zinaweza kudumu zaidi ya miaka mitano,” alisema Dk Mpango wakati akitoa ufafanuzi wa viwango vipya vya kodi kwa vyombo vya usafiri.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akiingia Bungeni Juni 13, 2019 na kuwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2019/2020. Picha|Mtandao.

Wakati wengine wakipata maumivu, baadhi ya bidhaa na huduma zimepata msamaha na kupunguziwa kodi, jambo linalowapa ahueni wazalishaji na watumiaji. 

Mathalani, kuanzia leo wafanyabiashara wapya wanapata nafuu ya kutolipa kodi kwa kipindi cha miezi sita kuanzia wakati wanapopewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN). 

Hatua hii inatofautiana na hali ya awali iliyokuwa inamfanyia tathmini ya kodi (tax assessment) mfanyabiashara na kumtaka kulipa kodi sehemu ya kodi husika mara tu anapopewa TIN.

Wawekezaji wa wapya wa viwanda vya kuzalisha taulo za kike wanatakiwa kulipa kodi ya mapato ya makampuni (Corporate Income Tax) ya asilimia 25 badala ya asilimia 30 iliyokuwepo mwaka wa fedha uliopita. 

Aidha, waagizaji wa sukari ya kawaida toka nje wanatozwa ushuru wa asilimia 35 badala ya asilimia 100 wakati vifaa vinavyotumika katika kukata, kung’arisha na kuongeza thamani ya madini ya vito vitatozwa ushuru wa asilimia sifuri badala ya asilimia 10 kwa mwaka mmoja. 

Ahueni nyingine ni kuondolewa kwa tozo 54 kutoka kwa taasisi mbalimbali za umma zikiwemo za ukaguzi wa maduka mapya ya kuuzia vyakula; usajili wa maduka ya reja reja ya dawa za mifugo; ukaguzi wa viwanda vya samaki; maombi ya alama ya ubora (TBS mark); na tozo ya usajili wa kampuni ya wakala wa worodha (Clearing Agent).

Hata hivyo, ahueni na maumivu ya kodi hizo, yanatarajia kutunisha mfuko wa Serikali ili kufanikisha upatikanaji wa Sh33.11 trilioni zitakazotumika katika kipindi cha mwaka mpya wa fedha unaoanza leo katika shughuli mbalimbali za maendeleo. 

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV