Ahueni kwa wanunuzi, bei ya maharage ikishuka Dar
- Gunia la kilo 100 la maharage limeshuka hadi Sh280,000 kutoka Sh300,000 ya ijumaa Februari 21, 2020.
- Bei hiyo ya maharage ni ya juu zaidi kuliko mazao yote ya chakula yanayouzwa leo katika masoko mbalimbali nchini.
- Bei ya chini kabisa ya maharage imeshuhudiwa katika masoko ya Halmashauri ya Musoma mkoani Mara ambapo gunia la kilo 100 limeuzwa kwa Sh100,000.
Dar es Salaam. Wanunuzi wa maharage katika jiji la Dar es Salaam leo watapata ahueni baada ya bei ya gunia la kilo 100 la zao hilo kushuka kwa Sh20,000 ikilinganishwa na bei iliyorekodiwa ijumaa Februari 21, 2020.
Mazao makuu ya chakula hujumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano.
Takwimu za bei za mazao makuu ya chakula zinazotumika katika maeneo mbalimbali nchini zilizotolewa leo (Februari 28, 2020) na Wizara ya Viwanda na Biashara zinaeleza kuwa gunia la kilo 100 katika soko la Kinondoni jijini humo linauzwa kwa Sh280,000 kutoka Sh300,000 ya wiki iliyopita.
Hiyo ni sawa kusema bei ya maharage ya gunia la kilo 100 imeshuka kwa asilimia 6.6 ndani ya wiki moja.
Hiyo itawapa ahueni wanunuzi na kuwaletea maumivu wafanyabiashara wa zao hilo ambao walitegemea bei ingeendelea kupanda ili kupata faida maradufu.
Licha ya kuwa bei ya maharage imeshuka, bado bei hiyo inayotumika leo ndiyo bei ya juu zaidi kuliko mazao yote ya chakula yanayouzwa leo katika masoko mbalimbali nchini Tanzania.
Zinazohusiana
Bei ya chini kabisa ya maharage imeshuhudiwa katika masoko ya Halmashauri ya Musoma mkoani Mara ambapo gunia la kilo 100 limeuzwa kwa Sh100,000.
Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa viazi mviringo ndiyo vinauzwa kwa bei ya chini kabisa kuliko mazao yote makuu ya chakula yaliyopo sokoni leo.
Bei hiyo imeshuhudiwa katika soko la Mwanjelwa mkoani Mbeya ambapo gunia la kilo 100 linauzwa kwa Sh46,000, wakati bei ya juu ya zao hilo ikiwa ni Sh120,000 katika mkoa wa Lindi.

Latest
