Ukatili mtandaoni wapungua kwa 53%, wanaume hatarini zaidi

- Kati ya matukio yote 213 yaliyorekodiwa, wanaume walikuwa wahanga katika matukio 161, sawa na asilimia 75.6, huku wanawake wakiwa wahanga katika matukio 52, sawa na asilimia 24.4.
Dar es Salaam. Matukio ya ukatili mtandaoni nchini Tanzania yamepungua kwa asilimia 53 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja huku wanaume wakiripotiwa kuathirika zaidi.
Kwa mujibu wa Ripoti ya hali ya uhalifu na matukio ya usalama barabarani mwaka 2025 inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha kuwa matukio ya ukatili mtandaoni yalishuka kutoka 453 mwaka 2024, hadi 213 mwaka 2025.
Hii ina maana kuwa zaidi ya matukio 240 yalipungua ndani ya miaka miwili, ikiwa ni sawa na asilimia 53.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukatili huo unahusisha vitendo mbalimbali vinavyofanyika kupitia majukwaa ya kidijitali, ikiwemo kutoa taarifa za uongo, kutumia lugha ya matusi, udanganyifu unaohusiana na kompyuta na vitendo vya ubaguzi.
Wanaume hatarini
Mbali na kupungua kwa matukio hayo, ripoti ya NBS inaonyesha kuwa wanaume ndio wahanga wakubwa wa vitendo hivyo ikilinganishwa na wanawake.
Kati ya matukio yote 213 yaliyorekodiwa, matukio 161, sawa na asilimia 75.6 yaliwahusu wanaume na matukio 52, sawa na asilimia 24.4 wanawake.
Hii ni sawa na kusema katika kila matukio 10 ya ukatili mtandaoni saba yaliwahusu wanaume na matatu wanawake.