Ukatili mtandaoni wapungua kwa 55%, wanaume hatarini zaidi

- Kati ya matukio yote 213 yaliyorekodiwa, wanaume walikuwa wahanga katika matukio 161, sawa na asilimia 75.6, huku wanawake wakiwa wahanga katika matukio 52, sawa na asilimia 24.4.
Dar es Salaam. Matukio ya udhalilishaji mtandaoni (cyberbullying) yameripotiwa kupungua nchini Tanzania hadi kufikia asilimia 55 mwaka 2025, huku wanaume wakiwa hatarini zaidi.
Ripoti ya Hali ya Uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani inayotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania inabainisha kuwa mwaka 2025 kulikuwa na matukio 213 ya ukatili mtandaoni.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matukio hayo yayohusisha vitendo kama vile kutoa taarifa za uongo, lugha ya matusi, udanganyifu unahusiana na komputa na ubaguzi yalipungua kwa asilimia 55.2 kulinganisha na matukio 453 yaliyoripotiwa mwaka 2024.
Hata hivyo, mbali na kupungua kwa matukio takwimu zikionyesha kuwa wanaume ndio wanaongoza kwa kuwa wahanga wakubwa wa vitendo hivyo ikilinganishwa na wanawake.
Kati ya matukio yote 213 yaliyorekodiwa, wanaume walikuwa wahanga katika matukio 161, sawa na asilimia 75.6, huku wanawake wakiwa wahanga katika matukio 52, sawa na asilimia 24.4.
Licha ya kupungua kwa matukio hayo, jeshi la polisi linasisitiza bado kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu juu ya athari za matumizi ya mtandao, ulinzi wa taarifa binafsi, utambuzi wa udanganyifu, matumizi sahihi ya mitandao na namna ya kuripoti vitendo vya uhalifu wa kidijitali.