Shilingi ya Tanzania yaendelea kuwa tulivu dhidi ya Dola ya Marekani
- Sarafu nyingine zimeonyesha mabadiliko kiduchu ukilinganisha na viwango vilivyotumika wiki iliyopita.
Dar es Salaam. Shilingi ya Tanzania imeendelea kuonesha utulivu dhidi ya Dola ya Marekani, huku viwango vya kubadilisha fedha katika Benki za CRDB na NMB vikibaki vilevile kati ya Novemba 5 na Novemba 9, 2026.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, CRDB imeendelea kununua dola moja kwa Sh2,600 na kuuza kwa Sh2,680, huku NMB ikinunua kwa Sh2,590 na kuuza kwa Sh2,670. Hivyo, CRDB ina viwango vya juu kwa Sh10 katika ununuzi na uuzaji ikilinganishwa na NMB.
Kwa upande wa sarafu nyingine, Euro na Pauni ya Uingereza zimeonesha kushuka kiduchu kwa viwango dhidi ya Shilingi ya Tanzania katika benki zote mbili.
Kwa Yuan ya China, mabadiliko yamekuwa madogo zaidi. CRDB imeshusha kiwango cha ununuzi kutoka Sh373.96 iliyotumika Novemba 5,2026 hadi 373.89, huku NMB ikidumisha kiwango cha Sh389.
Utulivu wa Shilingi una umuhimu katika kusaidia wafanyabiashara na wawekezaji kupanga shughuli zao, hasa uagizaji wa bidhaa, mafuta, mashine na malighafi kutoka nje.
Aidha, unaweza kusaidia kupunguza kutokuwa na uhakika wa gharama za biashara ya kimataifa na shinikizo la mabadiliko ya bei za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
