Samia apiga kura Chamwino, Ndejembi akisubiri mrithi wake
- Uchaguzi huo unafanyika ikiwa ni takribani siku 76 tangu Ndejembi kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais, Agosti 26, 2026.
- Ndejembi asema ana matumaini mrithi wake ataendeleza shughuli za maendeleo zilizotekelezwa Chamwino.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameshiriki katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Chamwino, mkoani Dodoma, unaofanyika kumtafuta mrithi wa Deogratius John Ndejembi, aliyeteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.
Rais Samia amepiga kura leo, Novemba 4, 2026, katika kituo namba tano cha kupigia kura kilichopo Ofisi ya Kijiji cha Chamwino, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Uchaguzi huo unafanyika ikiwa ni takribani siku 76 tangu Ndejembi kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais, Agosti 26, 2026 hatua iliyosababisha jimbo la Chamwino kuwa wazi kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.
Akishiriki katika zoezi la kupiga kura mapema leo, Ndejembi amesema ana matumaini mrithi wake ataendeleza shughuli za maendeleo zilizotekelezwa katika jimbo hilo, akisisitiza kuwa licha ya tofauti za vyama, wananchi wana lengo la pamoja la kujenga Chamwino na Tanzania.
“Wananchi wa Chamwino wana matumaini makubwa kwamba hata mrithi wangu Dk. Netho Ndilitho ataendeleza kazi kwa kasi hiyo hiyo. Ndiyo maana tunatarajia mwamko mkubwa kutoka kwa wapigakura wa vyama vyote,” amesema Ndejembi.
Awali akitoa taarifa kuhusu uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele, alisema kuwa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Chamwino, mkoani Dodoma, unaenda sambamba na uchaguzi wa madiwani katika kata 11, ukiwa na jumla ya vituo 665 vya kupigia kura.
Ambapo Jimbo la Chamwino lina jumla ya wagombea 16 wa nafasi ya ubunge, wanaume wakiwa wanane na wanawake wanane sawa na asilimia 50 kwa 50
Kwa upande wa uchaguzi wa udiwani katika kata 11, amesema jumla ya wagombea ni 51, ambapo wanaume ni 43 sawa na asilimia 84.3, huku wanawake wakiwa wanane sawa na asilimia 15.6.
Huku idadi ya wapiga kura ikiwa ni 213,024 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanatarajiwa kushiriki uchaguzi huo, ambapo kati yao 133,864 wapo Jimbo la Chamwino na wapiga kura 79,160 wanatoka katika kata 11 zinazofanya uchaguzi mdogo.