Lissu aingia tatu bora tuzo ya Sakharov, akisubiri hukumu Novemba 6
- Sherehe za utoaji wa tuzo hiyo zinatarajiwa kufanyika Desemba 16, 2026, mjini Strasbourg, Ufaransa.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameorodheshwa miongoni mwa wagombea watatu wa mwisho wa Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo 2026.
Tuzo hiyo, iliyoanzishwa mwaka 1988 na Bunge la Ulaya, ni miongoni mwa tuzo zenye hadhi kubwa zaidi duniani zikilenga kutambua mchango wa watu, makundi au mashirika yaliyojitolea kutetea haki za binadamu, demokrasia na uhuru wa mawazo duniani.
Kuteuliwa kwa Lissu kunakuja wakati akiendelea kukabiliwa na kesi ya uhaini, huku Mahakama Kuu ya Tanzania ikitarajiwa kutoa hukumu ya shauri hilo Novemba 6, 2026.Â
Lissu, ambaye aliyekamatwa Aprili 9 mwaka jana anashtakiwa kwa kosa la uhaini kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023 linalotokana na tuhuma za matamshi aliyoyatoa Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam ya kutoshiriki na kuzuia Uchaguzi Mkuu 2025.

Hatua hiyo imeongeza uzito wa uteuzi wake katika kipindi ambacho macho ya jumuiya ya kimataifa yanaendelea kuelekezwa nchini Tanzania kutokana na maendeleo ya kesi hiyo.
Uteuzi wa Lissu umeitishwa baada ya kura zilizopigwa na Kamati za Mambo ya Nje na Maendeleo za Bunge la Ulaya, zilizopunguza orodha kutoka kwa waliopendekezwa sita hadi watatu bora.
Wateule wengine wanaowania tuzo hiyo ni Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) pamoja na maafisa wake, pamoa na wanawake wawili mapacha kutoka Iran, (Taraneh na Romina Rahimi), ambao wanaotajwa katika kampeni ya kutetea haki za wanawake na kupinga hukumu kali nchini humo.
Wagombea wengine waliokuwa kwenye orodha ya awali lakini hawakufanikiwa kuingia tatu bora ni Rais wa El Salvador Nayib Bukele, Daktari wa watoto kutoka Gaza Dk Hussam Abu Safiya, pamoja na harakati za amani za Kiyahudi na Kiarabu nchini Israel.
Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola, anatarajiwa kumtangaza mshindi rasmi wa tuzo hiyo baada ya matokeo ya maamuzi ya Mkutano wa Marais wa Bunge.
Sherehe za utoaji wa tuzo hiyo zinatarajiwa kufanyika Desemba 16, 2026, mjini Strasbourg, Ufaransa, wakati wa kikao kikuu cha Bunge la Ulaya.
Tuzo hiyo inaambatana na zawadi ya Euro 50,000 takriban Sh148.2 milioni za kitanzania.